Venezuela yaripoti tetemeko jingine, vifo vikifikia 1,700
Muktasari:
- Vifo katika tetemeko la Venezuela vimefikia zaidi ya 1,700 baada ya mitetemeko mikubwa miwili huku tetemeko jingine dogo la 4.6 likizua hofu mpya wakati uokoaji ukiendelea.
Dar es Salaam. Idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na matetemeko makubwa yaliyolikumba taifa la Venezuela imefikia zaidi ya watu 1,700 huku operesheni za uokoaji zikiendelea katika maeneo yaliyoathirika zaidi hasa karibu na mji mkuu Caracas na jimbo la pwani la La Guaira.
Kwa mujibu wa Shirika la Jiolojia la Marekani (USGS) Venezuela ilikumbwa na mitetemeko miwili mikubwa yenye ukubwa wa 7.2 na 7.5 katika kipimo cha Richter, iliyotokea kwa muda mfupi kati ya tukio moja na jingine, na kusababisha uharibifu mkubwa wa majengo na miundombinu.
Katika hatua iliyoongeza hofu zaidi, tetemeko jingine dogo la ukubwa wa 4.6 limeripotiwa kutokea kilomita takribani 10 kaskazini mwa Caracas jana.
Hata hivyo, Spika wa Bunge la Venezuela, Jorge Rodríguez amenukuliwa na vyombo vya habari akisema hakuna vifo vipya au uharibifu wa ziada ulioripotiwa kufuatia mtikisiko huo mpya.
Wakati huohuo, operesheni za uokoaji zinaendelea huku hali ya taharuki ikiongezeka miongoni mwa wananchi waliopoteza makazi na wanaolazimika kulala nje kutokana na hofu ya majengo kuporomoka.
Rais wa mpito, Delcy Rodríguez amesema Serikali bado ina matumaini kuhusu juhudi za uokoaji na misaada ya dharura, ingawa ukosoaji unaongezeka kuhusu kasi ya msaada na usimamizi wa janga hilo.
Ripoti zinaonyesha zaidi ya watu 65,000 hawajulikani walipo, huku maelfu ya wengine wakijeruhiwa na hospitali zikikabiliwa na msongamano mkubwa wa waathirika.
Mashirika ya kimataifa na timu za uokoaji kutoka nchi mbalimbali zimeendelea kuwasili kusaidia, huku baadhi ya vifaa vya dharura na hospitali za muda vikitumwa kusaidia waathirika katika maeneo yaliyoathirika zaidi.
Tangu matetemeko ya awali, maeneo ya pwani hasa La Guaira na mji mkuu wa Caracas yameathirika zaidi.
Mbali na vifo vya watu, maelfu ya majengo yameharibiwa au kuporomoka huku huduma za afya na maji zimekuwa na msongamano mkubwa na maelfu ya wananchi bado wapo mitaani wakihofu mitikisiko inayoendelea kusababisha majengo kuporomoka.