Walinzi wa mama yake Kenyatta waondolewa
Mama Ngina Kenyatta. Picha na Taifa Leo
Muktasari:
- Walinzi wa mama wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, Mama Ngina Kenyatta, wameondolewa jana Jumanne ya Julai 18, 2023.
Kenya. Walinzi wa Mama mzazi wa Rais mstaafu wa Kenya Uhuru Kenyatta, Mama Ngina Kenyatta maarufu kama Mama Ngina, wameondolewa jana Jumanne ya Julai 18, mara baada ya kuwasili eneo la ulinzi ambalo ni nyumba za mama huyo.
Walinzi hao wanaolinda nyumba za Mama Ngina zilizopo Gatundu Kaunti ya Kiambu na Muthaiga jijini Nairobi, waliondoshwa jioni mara baada ya kuwasili kwenye malindo yao na kuarifiwa wakaripoti vituo vya polisi vilivyopo karibu.
Vyombo mbalimbali vya habari nchini humo vimeripoti taarifa hiyo huku ikiarifiwa kwamba Mama Ngina hakuambiwa hapo awali kuhusu kuondolewa kwa maofisa hao.
"Tuliondoa walinzi hapo kwa ajili ya mazungumzo lakini watarejea. Ana haki ya kupata usalama,” ofisa mmoja wa polisi aliiambia tovuti ya Star ya nchini humo huku akiomba kutotajwa jina lake.
Mama Ngina, (90) ambaye ni mke wa Rais kwanza wa nchi hiyo, Jomo Kenyatta kabla ya kuondolewa alikuwa na jumla ya walinzi 30 waliokuwa wakilinda majengo yake yote.