Prime
Kwa nini baadhi ya Gen Z hawaogopi kuacha kazi?
Muktasari:
- Ripoti ya Deloitte Global Gen Z and Millennial Survey 2026, iliyochapishwa Mei 13, 2026 inaonesha kuwa asilimia 31 ya Gen Z walioajiriwa wanatarajia kuondoka kwa mwajiri wao ndani ya miaka miwili ijayo, hali inayoashiria kwamba, uhamaji wa wafanyakazi bado ni mkubwa.
Dar es Salaam. “Nikiacha kazi leo, nitapata nyingine.” Hiyo ndiyo fikra inayosemekana kuongoza sehemu ya kizazi cha Gen Z, ambacho kimebadili namna soko la ajira linavyofanya kazi.
Tofauti na wazazi wao walioweza kukaa miaka mingi kwa mwajiri mmoja, vijana wengi wa kizazi hiki hawahofii kuondoka wanapoona kazi haiwapi fursa ya kujifunza, kukua au kuishi maisha wanayotamani.
Mwelekeo huo umefanya kampuni nyingi zikabiliane na changamoto ya si tu kuajiri vipaji, bali pia kuvihifadhi huku waajiri wengi wakikiri kupata wafanyakazi kutoka kizazi cha Gen Z si tatizo kubwa, changamoto inaanza baada ya kuwaajiri.
Tofauti na vizazi vilivyotangulia vilivyotanguliza usalama wa ajira, Gen Z huweka mbele mazingira bora ya kazi, ukuaji wa taaluma, usawa kati ya kazi na maisha binafsi, pamoja na mshahara unaoendana na mchango wao.
Matokeo yake ni ongezeko la wafanyakazi wanaoondoka ndani ya muda mfupi baada ya kuajiriwa, jambo linaloongeza gharama kwa waajiri na kuzua mjadala kuhusu namna bora ya kuwahifadhi kazini.
Hali ilivyo
Katika moja ya duka la mahitaji ya nyumbani, mmiliki akiwa bado anaweka uangalizi wa karibu kwa kijana aliyemuajiri hivi karibuni baada ya aliyekuwapo kuondoka, anasema kuwafanya vijana hao wabaki kazini si jambo rahisi.
“Huyu ni mpya, yule aliyekuwapo ameondoka baada ya kuona kuwa anabanwa na kukosa muda wa kulala kwa sababu anatakiwa kufungua duka saa moja asubuhi na kufunga saa tano usiku,” anasema Gilbert Mushi, mmiliki wa Duka Tabata.
Gilbert anasema ndani ya miezi miwili ndani ya duka lake la Chang’ombe amelazimika kubadili vijana mara tatu baada ya wote waliokuwapo kuomba kucha kazi.
“Sasa ukiacha hawa, yule wa duka la Tabata shule naye kaniambia anataka kuondoka kwa sababu mwanzoni aliomba nimpunguzie mshahara ili awe anafungua saa nne na kufunga saa moja usiku, ukiangalia muda anaosema duka liwe limefungwa ndiyo wateja wanakuja,” anasema.
Anasema hali hiyo ilimfanya kuwa mnyonge baada ya ombi lake kukataliwa hivyo kuandoka ikawa ndiyo njia sahihi kijana huyo mwenye miaka 23 pekee aliyeichangua.
Hali hiyo haijaonekana kwa Gilbert pekee, baadhi ya watu pia waajiri hususan wa maduka wanakiri kukutana na hali hiyo jambo linaloweka ugumu kuamini watu wasimamie biashara zao kiasi cha kuwalazimu wakae wenyewe.
“Kuna mwingine aliomba mwenyewe kazi, alipojua mshahara ni Sh300,000 akakataa akasema yeye amesoma na shahada hawezi kufanya kazi hiyo ya kubembeleza wateja labda nimfanye kuwa msimamizi mkuu, hana hata uzoefu,” anasema Mashaka Kazinja mfanyabiashara wa Kariakoo.
Ripoti ya Deloitte Global Gen Z and Millennial Survey 2026, iliyochapishwa Mei 13, 2026 inaonesha kuwa asilimia 31 ya Gen Z walioajiriwa wanatarajia kuondoka kwa mwajiri wao ndani ya miaka miwili ijayo, hali inayoashiria kwamba, uhamaji wa wafanyakazi bado ni mkubwa.
Utafiti huo uliohusisha zaidi ya Gen Z na Millennials 22,500 kutoka nchi 44 unaonesha ni asilimia sita pekee ndiyo walikuwa na lengo la kufikia nafasi za juu za uongozi.
Hata maofisini kazi
Tofauti na kile kilichosemwa na wafanyabiashara na namna wanavyopata shida katika usimamizi wa kikazi wa vijana hao, maofisini nako hali ni ileile.
Hiyo ni kutokana na kile kilichobainishwa ili vijana hao wadumu kwenye ajira kuna maeneo yanayopaswa kuangalia kuanzia kwenye uongozi, malezi na namna ya kumsimamia akiwa kazini, kazi anazopewa zisimzuie kufanya mambo yake.
Akizungumza na Mwananchi, Lugano Bwenda ambaye ni Ofisa Rasilimali Watu Mstaafu na Meneja Operesheni kutoka Kampuni ya Usafirishaji ya Simba anasema linapokuja suala la ajira, vijana kufanya uamuzi wa kuacha kazi ni kitu cha dakika moja.
Anasema katika hali za kawaida Gen Z akiwa kazini ukimgombeza baada ya kukosea anaichukia kazi na kushindwa kuifanya kwa utulivu na wanapofanya kazi hawataki kukaa chini kwa muda mrefu.
“Anataka kama ni saa tatu akija ofisini saa tisa aondoke, au akija saa moja, saa tano aondoke mambo mengine atayafanyia nyumbani au sehemu atakayokuwa, kazi isimbane kufanya mambo yake, waajiri wengi hawakubaliani na hili,” anasema
Hali hiyo imewafanya wengi kutafuta kazi za muda mfupi ili anapomaliza awe ameachana nazo.
Anasema katika utendaji kazi pia ni tofati kwani baadhi yao wanataka ndani ya miaka miwili au mitatu wawe wamepandishwa kutoka sehemu walizokuwa awali na si kuendelea kusalia katika daraja moja kwa muda mrefu.
“Ikiwa hivi labda kwenye ofisi yako kuwe na sherehe nyingi, mitoko ya kiofisi ya kutosha inaweza kumfanya akae kinyume na hapo hawezi,” anasema.
Akizungumzia upande wa utatuzi wa matatizo, Bwenda anasema kizazi kabla ya Gen Z mtu alipopata tatizo ofisini alivumilia au alitafuta mtu wa kuzungumza naye kinyume chake kizazi hiki kinataka bosi akae naye amuulize nini shida, nini kifanyike, anataka iweje.
“Kitu kingine kwa kizazi hiki ni mabadiliko ya kasi ya teknolojia huwafanya wengi wao kujikuta wanavujisha siri za kampuni bila wao kujua, kitu kikitokea ndani ya ofisi wanataka kuonekana kuwa wa kwanza kusema katika mitandao hata kama hawataji jina,” anasema.
“Au anaweza kugombana na msimamizi wake kazi akaenda kuposti hiki nini, au nachukia kazi au maneno ambayo si mazuri,” anasema.
Mwanasaikolojia wa kazi, Mashile Masanja anasema changamoto zinazoripotiwa kuhusu wafanyakazi wa kizazi cha Gen Z hazipaswi kutafsiriwa kuwa ni wavivu au hawapendi kufanya kazi, bali ni ishara ya mabadiliko ya mtazamo kuhusu ajira.
Anasema tofauti na vizazi vilivyotangulia, Gen Z wamekua katika mazingira ya teknolojia, upatikanaji wa taarifa kwa haraka na fursa nyingi za kujifunza, hali inayowafanya kuwa na matarajio makubwa kuhusu mazingira ya kazi.
"Wanataka kusikilizwa, kushirikishwa katika maamuzi yanayowahusu na kupata mrejesho wa mara kwa mara kuhusu utendaji wao. Ukitumia mtindo wa kuamuru bila mawasiliano mazuri, kuna uwezekano mkubwa wakapoteza motisha au wakaamua kuondoka," anasema.
Anasema viongozi wa taasisi wanapaswa kujenga utamaduni wa mazungumzo ya wazi badala ya kusubiri matatizo yatokee ndipo wayashughulikie.
"Kukaa na mfanyakazi mara kwa mara, kuelewa changamoto zake na kuweka malengo ya pamoja kunajenga hisia za kuthaminiwa. Hilo linaongeza uwezekano wa kubaki kazini," anasema.
Pia, anashauri waajiri kuweka wazi matarajio ya kazi tangu hatua ya mahojiano ili kuepusha matarajio yasiyolingana kati ya mwajiri na mwajiriwa.
Wenyewe wanasemaje
Brian Mwakalebela ambaye aliacha kazi aliyokuwa akifanya katika kampuni binafsi baada ya mwaka mmoja anasema uamuzi wake haukutokana na kutopenda kazi bali kutokuwa na matarajio ya kukua.
"Nilikuwa nafanya kazi kwa bidii lakini kila nilipouliza kuhusu mafunzo au kupandishwa cheo niliambiwa nisubiri. Baada ya muda niliona sina ninachojifunza kipya hivyo nikaanza kutafuta sehemu nyingine,” anasema.
Brian anasema mazingira ya kazi yana mchango mkubwa katika uamuzi wa kubaki au kuondoka.
Anasema tofauti na zamani, sasa mitandao ya kijamii na majukwaa ya kutafuta ajira yamewapa vijana taarifa nyingi kuhusu fursa zilizopo hivyo hawahisi kukaa chini ya mwajiri kama jambo la lazima na badala yake wanaweza kufanya kazi mtandaoni na kupata fedha.
"Zamani watu walikaa kwa sababu hawakujua kuna fursa nyingine. Sasa taarifa zipo kila mahali. Ukiona sehemu nyingine inaweza kukupa mazingira bora, unajaribu."
Nini kifanyike
Akizungumza Bwenda anasema miongoni mwa vitu vinavyoweza kuwafanya vijana hao kukaa kazini ni kuwapa motisha ikiwamo vitendea kazi kama kompyuta mpakato na simu ili waone kuwa ofisi inawajali.
“Pia, kuwatengenezea mazingira ya kazi waishi wanavyotaka, hii itasaidia kunufaika nao katika soko la ajira. Kuwapo kwa mpango wa matarajio na namna ambavyo wanaweza kupanda vyeo kila baada ya muda fulani nayo ni moja ya njia inayoweza kuwafanya wakae kazini,” anasema.