Waliofariki boti iliyozama Msumbiji wafikia 96

Muktasari:

  • Boti imezama nchini Msumbiji na kusababisha vifo vya watu 96 huku sababu ikitajwa kuzidisha abiria.

Msumbiji. Idadi ya watu waliofariki kutokana na kuzama kwa boti katika pwani ya Kaskazini ya Msumbiji, imeongezeka hadi kufikia 96, mamlaka za eneo hilo zimesema leo Jumatatu Aprili 8, 2024.

 Boti hiyo ilikuwa imebeba takriban watu 130, ilikuwa ikielekea katika kisiwa kilichopo karibu na mkoa wa Nampula, jana Jumapili.

Idadi hiyo imefikia baada ya miili mitano kupatikana saa chache zilizopita, amesema Silverio Nauaito, msimamizi wa kisiwa kidogo karibu na mkoa wa kaskazini wa Nampula ambako maafa hayo yametokea.

Taarifa zinasema miongoni mwa abiria walikuwa watoto na hadi sasa waokoaji wamepata manusura 11 na shughuli za kuwatafuta zinaendelea, japokuwa hali ya hewa baharini ni mbaya, hivyo kusababisha ugumu katika uokoaji.

AFP imeripoti jana Jumapili, boti hiyo ilizama baada ya kupata tatizo kwa vile ilikuwa imejaza watu wengi, huku ikiwa haifai kubeba abiria.

Aidha, watu watano wameokolewa na wawili kati yao wanaendelea na matibabu hospitalini, huku ikielezwa kuwa picha ambazo hazijathibitishwa zinazosambaa mitandaoni zikionyesha makumi ya miili ikiwa imelala ufukweni.