Waliokufa kwa mafuriko Pakistan wafikia 39

Pakistan. Mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini Pakistan zimesababisha vifo vya watu wanne na kufanya idadi ya waliokufa kutokana na mafuriko hayo kufikia 39.

Kwa mujibu wa mtandao wa Dawn, viongozi wa Serikali wametoa tahadhari kwa wananchi kuhusu mafuriko zaidi huku wakieleza juhudi mbalimbali za uokoaji zilizofanyika.

Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif amesema wamemuagiza mwenyekiti wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kudhibiti Maafa (NDMA) kuratibu majimbo yote yaliyokumbwa na mafuriko ikiwa ni pamoja na kuhakikisha misaada inawafikia waathirika.

Msemaji wa PDMA, Anwar Shahzad amesema walikuwa wakikusanya taarifa zaidi kuhusu hasara na uharibifu uliotokana na mvua hizo lakini akabainisha kuwa hadi Jumapili iliyopita nyumba 85 zilibomoka baada ya kujaa maji yaliyokuwa yakitoka katika mito mbalimbali ambayo pia ilikuwa haipitiki kwa njia za kawaida.

Mafuriko hayo yamesababisha baadhi ya shughuli kukwama zikiwemo za utalii ambapo mmoja wa watalii hao, Ahmad Ali alinukuriwa akieleza jinsi walivyokwama kwa siku mbili kutokana na barabara nyingi kutopitika.

‘’Nadhani juhudi zinapaswa kuongezwa zaidi kwasababu watu wamekwama na kuna hatari hata ya kutokea maporomoko ya udongo,’’ amesema Ahmad wakati akihojiwa na mtandao wa Dawn.