Wanafunzi wamshushia kipigo Mkuu wa Shule kisa uji hauna sukari
Muktasari:
- Polisi katika Kaunti ya Homa Bay Kenya wameanzisha uchunguzi wa tukio la wanafunzi wa kumpiga mkuu wa shule wakimshtumu kuwapa uji usio na sukari.
Kenya. Wanafunzi wa kidato cha nne Shule ya Sekondari God Bura iliyoko Homa Bay Kenya, wamemvamia mkuu wa shule hiyo kisha kumshushia kipigo katika kile kilichodaiwa amewapa uji hauna sukari.
Mwalimu huyo aliyetambulika kwa jina la Collins Omondi alivamiwa na wanafunzi hao alipokuwa nyumbani kwake Ijumaa mwishoni mwa wiki kisha kumpiga na kuahidi kumpeleka polisi.
Inasemekana wanafunzi hao walimtoa nje ya nyumba yake kisha kumpiga mateke na makofi huku wakimshtumu kwa kuruhusu wapishi kuwapa uji bila sukari.
Tovuti ya Tuko imesema, mwalimu Omondi alikimbizwa Hospitali ya Magunga kwa uchunguzi zaidi kutokana na majeraha ya kifua yaliyotokana na kipigo hicho.
Tukio hilo kwa sasa linachunguzwa na polisi wa Kaunti ya Homa Bay na Wizara ya Elimu, huku baadhi ya wazazi wakishukiwa kushiriki.
Pia, wanafunzi walimshutumu Omondi kwa kusimamia vibaya shule hiyo, huku wakisisitiza kumpeleka katika Kituo cha Polisi cha Magunga akaeleze jinsi fedha za shule hiyo zinavyotumika.
Mwenyekiti wa Chama cha Wakuu wa Shule za Sekondari, Paul Mbara amelaani tukio hilo, akiwataka wazazi na wanafunzi kutafuta mbinu nyingine za kutatua migogoro.
"Kumvamia walimu sio suluhu la matatizo yanayozikabili shule. Kuwe na njia mbadala za kutatua migogoro," amesema Mbara.