Wawili wapigwa risasi katika maandamano Kenya

Muktasari:
Watu wawili wamepigwa risasi na kupata majeraha katika maandamano dhidi ya Serikali yanayoendelea nchini Kenya katika Kaunti ya Migori.
Kenya. Watu wawili wamepigwa risasi na kupata majeraha katika maandamano dhidi ya Serikali yanayoendelea nchini Kenya katika Kaunti ya Migori.
Msimamizi wa hospitali ya moja huko Migori, Oruba Ochere amethibitisha kuwa wanaume wawili ambao wamejeruhiwa kwa risasi wanapokea matibabu katika hospitali hiyo.
Ochere amesema mmoja wa waathiriwa amepigwa risasi kwenye paja huku mwingine akipigwa risasi ya mguu.
Msimamizi wa hospitali hiyo pia amethibitisha kupokea mwanamke mmoja ambaye alifikishwa hospitalini hapo kwa kukosa hewa baada ya polisi kurusha bomu la machozi ambalo liliingia ndani ya nyumba yake.
Wakati huo huo, huduma za usafiri zimepungua kwa kiasi kikubwa na biashara kufungwa ndani ya mji wa Migori, hii inatokana na maandamano yanayoendelea maeneo mbalimbali katika Kaunti hiyo.
Hata hivyo Jeshi la Polisi katika Kaunti hiyo, limewazuia waandamanaji hao kuingia katika eneo la biashara la Migori.
Waandamanaji katika kaunti hiyo wanaendelea kukabiliana na Polisi katika maeneo ya Oruba, Osaka na Apida ambayo yako karibu na Mji wa Migori.
Waandamanaji hao wamewashutumu Polisi kwa kutumia nguvu kupita kiasi kwa waandamanaji.
Waandamanaji wamesema Polisi wanapaswa kuwaruhusu kushiriki maandamano yao kwa amani kwani kuingilia kwa Polisi ndio chanzo cha vurugu.