ACT Wazalendo wajipanga kumuenzi Maalim Seif, CCM yakemea siasa chafu

Hayati Maalim Seif Sharrif Hamad

Muktasari:

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar, Khamis Mbeto Khamis, amewasihi wananchi kuwa na tahadhari dhidi ya vyama vya upinzani alivyodai vinaendeleza siasa za choko choko

Unguja. Chama cha ACT Wazalendo kimesema njia pekee ya kumuenzi Maalim Seif Sharif Hamad na kufikia safari yake, ni kukiondoa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar.

Kwa upande wa CCM, imekemea siasa ilizodai ni za chokochoko, ikisisitiza ziwepo za utulivu na kulinda amani iliyopo.

ACT imebainisha hayo wakati wa duru ya pili ya mikutano ya hadhara maarufu bandika bandua baada ya kumaliza makongamano yaliyowakutanisha na viongozi wa mikoa sita ya kichama.

Akizungumza katika mkutano uliofanyika Bububu leo Jumapili Juni 2, 2024 Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Ismail Jussa amesema wameanza mikutano hiyo kwa lengo la kutuma salamu CCM kwamba uchaguzi ujao lazima wafungashe vilago. 

“Njia pekee ya kumuenzi mzee wetu Maalim Seif Sharif Hamad ni kukifungashia virago CCM katika uchaguzi 2025, na safari hii tayari tumeshaianza, vijana wote tunatakiwa kupeleka ujumbe huu,” amesema Jussa.

Amesema uwezo wa chama hicho kushika madaraka umeshafikia mwisho huku akidai upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Pemba na miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara za Unguja na Pemba, imekwama kutokana na migogoro ya kimkataba inayosubiri kuamuliwa mahakamani. 

“Mwaka jana, Serikali ya Muungano iliipa Zanzibar dhamana ya kujitawala kwa mara ya kwanza, ikituruhusu kukopa zaidi ya Sh1 trilioni kutoka Uingereza Export Finance (UKEF) ili kupanua Uwanja wa Ndege wa Pemba. Lakini, kama mlivyosikia, mradi huu umesimama kwa sababu ya kuingiliwa kwa kisiasa, kusubiri uamuzi wa Mahakama,” amesema.

Amedai kuwa ni mradi uliokusudiwa kufungua uwezo wa Pemba lakini unasimamiwa kwa manufaa binafsi, bila ya kuchungulia kwa kina nini kilijiri katika ubia kati ya kampuni mbili zilizopewa zabuni. 

Hata wakati wa kupitisha bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wiki iliyopita, hoja hiyo iliibuliwa katika Baraza la Wawakilishi na mwakilishi wa Ziwani, Suleiman Makame Ali akisema kuna changamoto ya miradi ya Pemba ukiwemo uwanja huo na barabara kukwama na kuitaka Serikali kuondoa mikwamo hiyo.

Januari mwaka huu, ziliripotiwa kampuni mbili zinazotekeleza mradi huo zilikuwa na mgogoro, huku Mahakama Kuu ya Zanzibar ikitia amri ya kusimamisha utekelezaji wa mradi huo.

Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Othman Masoud amesema katika harakati hizo, jambo la mwanzo wanalolitafuta na hawawezi kuacha kulitafuta ni kuikomboa Zanzibar.

"Nadhani ilikuwa Mungu kwa baadhi yetu kuondoka serikalini ili tuzungumze juu ya maovu haya ambayo yanaendelea kuchafua Zanzibar.”

Othman ambaye alikuwaa Mwanasheria Mkuu na Naibu Mwanasheria Mkuu wa SMZ kwa zaidi ya miaka 17, amesema iwapo wakiingia madarakani watahakikisha walioiba rasilimali wanachukuliwa hatua za kisheria.

 CCM yanena

 Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar, Khamis Mbeto Khamis, amewasihi wananchi kuwa na tahadhari dhidi ya vyama vya upinzani alivyodai vinaendeleza siasa za choko choko, fitna na uchochezi.

Amesema vyama hivyo havina sifa wala ujasiri wa kupigania maendeleo na kutetea maslahi ya umma. 

“Hao jamaa kwa sasa wamechanganyikiwa, hawana tena cha kwenda kuwaambia wafuasi wao 2025, mambo yote tayari Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi kashamaliza utekelezaji wake,” amesema Mbeto. 

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Amesema CCM itaendeleza siasa za uvumilivu, ustaarabu huku kikinadi sera zake kwa kueleza kwa kina mafanikio na mikakati endelevu ya kuwatumikia wananchi.