Dk Nchimbi aibeba falsafa ya maridhiano ya Rais Samia

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi  akizungumza na viongozi wa chama hicho mkoa wa Ruvuma.

Muktasari:

Asema siasa si ugomvi, ahimiza maridhiano miongoni mwa Watanzania.

Songea. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amesema siasa ya vyama vingi si ugomvi, akiwataka wana-CCM na Watanzania kutoacha kuzungumza na kusalimiana, ili kujenga mshikamano wa Taifa.

 Amewataka wanachama wa CCM kuishi katika misingi ya kutogombana, ili kutunza dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhimiza maridhiano na umoja wa kitaifa kwa sababu wote ni Watanzania.

Dk Nchimbi ameeleza hayo leo Jumamosi Aprili 20, 2024 akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Matarawe wilayani Songea mkoani Ruvuma.

Mkutano huo ulikuwa sehemu pia ya mapokezi, baada ya Dk Nchimbi kuteuliwa kushika wadhifa huo akichukua nafasi ya Daniel Chongolo aliyejiuzulu.

Kiongozi huyo pamoja na wengine wa Sekretarieti ya CCM wako ziarani mkoani humo.

Dk Nchimbi amesema Rais Samia amekuwa mstari wa mbele kuendeleza maridhiano ndiyo maana alihudhuria mkutano wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), uliofanyika Machi 8, 2023 mkoani Kilimanjaro baada ya kualikwa na chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

Amesema Makamu Mwenyekiti wa CCM- Bara, Abdulrahman Kinana alihudhuria mkutano mkuu wa nne wa ACT- Wazalendo uliofanyika Machi 5 na 6, 2024 mkoani Dar es Salaam.

"Sisi viongozi wa kitaifa tunaongoza kwa mifano kwamba hakuna ugomvi, mtu yeyote anayechochea ugomvi hana nia njema kwa sababu tunataka kila kitu katika Taifa letu kifikiwe kwa njia ya mazungumzo,” amesema.

"Kwa hiyo, kama kuna tatizo tuzungumze, tushindane kwa hoja, tusishindane kwa ugomvi, mwaka 1964 Baba wa Taifa (Julius Nyerere) alitoa waraka kwa mabalozi akiweka maneno ya kwamba  mtu anayechochea ugomvi katika jamii awe wa chama chochote hana msaada kwa nchi yetu," amesema Dk  Nchimbi akimnukuu Nyerere.

Amewataka wana-CCM wakiona watu wanajenga hoja wakae nao na kuwasikiliza, lakini wale wanaokuja kwa njia ya kuropoka na matusi wawapuuze.

Amesisitiza mtu yeyote anayechochoe ugomvi hana msaada katika Taifa.

"Ukimuona mwana-CCM anapita mtaani kuchochea ugomvi na mifarakano kwa jamii huyu hana msaada kwa nchi yetu, ukiona mwana-Chadema anapita huku na kule anachochea ugomvi huyu hana msaada kwa Taifa letu. Pia ukimuona mwana-ACT anapita kuchochoea ugomvi huyu hana nafasi kwa Taifa letu," amesema Dk Nchimbi.

Amesema CCM inataka kila kiongozi wa Taifa, wakiwemo wa Serikali na vyama vya siasa kutambua wajibu wao wa kuwaunganisha Watanzania, ili kushirikiana kufanya kazi pamoja.

"Chama hiki tawala kitaendelea kutimiza wajibu wake kwa uaminifu, kwa kutambua wana dhamana kubwa ya kuwaunganisha Watanzania," amesema.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla amesema lengo la ziara ni kukagua uhai wa chama hicho na kuzungumza na viongozi wa ngazi mbalimbali, wakiwamo mabalozi wa mashina ili kujua mwenendo wa chama hicho.

Wajumbe nyumba 10

Dk Nchimbi amesema chama hicho, kimeamua kurudi kwa wanachama kwa kuwezesha mabalozi, ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Amesema hivi sasa wameamua kuwapa heshima kubwa mabalozi kwa sababu ndiyo msingi na shina la chama hicho na ndiyo viongozi wanaokuwa karibu na wanachama wa CCM katika maeneo mbalimbali.

Alikuwa akizungumza katika kikao cha ndani na viongozi wa CCM kutoka wilaya mbalimbali za Mkoa wa Ruvuma.

"Hivi sasa tumeelekeze nchini nzima kuwatambua mabalozi kama ni viongozi wakuu katika chama chetu, tutaendelea kusisitiza jambo hilo bila kuchoka kila wakati,” amesema.

Dk Nchimbi amesema, "Kwa njia hiyo CCM itarudi kwa wanachama, tunataka wana-CCM watambue kuwa wana dhamana kubwa kuliko mtu yeyote katika uhai wa chama hiki na wengine waliobaki ni watumishi."

Makalla amewataka viongozi wa CCM kuanzia matawi na ngazi nyingine kuwa mstari wa mbele kusikiliza kero za Watanzania kwa sababu chama hicho tawala ndiyo kimbilio la utatuzi wa changamoto zao.