Aliaga anakwenda kuleta mke, akarudi na maiti za ndugu zake wawili aliowaua

Muktasari:

 Upande wa Jamhuri ukiongozwa na wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), Raphael Rwezaula akisaidiana na wakili wa Serikali, Grace Christopher uliita mashahidi saba na kuwasilisha velelezo vinne vilivyosaidia kuthibitisha shitaka hilo la mauaji

Babati. Ni ukatili uliopitiza. Ndivyo unavyoweza kuelezea tukio la Niima Kwaslema, mkazi wa Kijiji cha Gabadaw wilaya ya Babati, kumuaga shemeji yake kuwa anakwenda kumleta bibi harusi anayemuoa lakini akarudi akiwa na maiti mbili za ndugu zake aliowaua kikatili.

Marehemu hao ni Baha Kwaslema ambaye ni kaka yake na mshitakiwa waliozaliwa na baba mmoja ila mama tofauti na Baatael Bayi ambaye ni mpwa wake, ambao ndio alioondoka nao kwenye gari, kuwa anamfuata mke wake huyo katika Kijiji cha Mandegem.

Mauaji hayo yalitokea usiku wa manane wa Desemba 5, 2019; marehemu aliondoka na gari la baba yake ambaye alikuwa shahidi wa nne  Kwaslema Warey, Toyota Noah namba T446 DJN lililokuwa likiendeshwa na Baha ambaye ni kaka yake.

Moja ya ushahidi uliommaliza Kwaslema ni maelezo yake mwenyewe ya onyo ya kukiri kosa aliyoyaandika Polisi akieleza na kuwataja watu ambao aliwataja kushirikiana katika mauaji hayo na kutoa Sh1 milioni ili kumuu kaka yake aitwaye Baha.

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), Raphael Rwezaula akisaidiana na wakili wa Serikali, Grace Christopher uliita mashahidi saba na kuwasilisha velelezo vinne vilivyosaidia kuthibitisha shitaka hilo la mauaji.

Sehemu ya maelezo hayo ya kukiri kosa yaliyopokelewa na kusomwa mahakamani kama kielelezo yanaeleza kuwa:“Ilitokea siku nilienda kwa baba akanitukana na kunieleza kuwa sisi ni wauaji ndipo nilichukia nikaenda kumweleza Athanas (hajakamatwa).”

“Naye alinishauri tumuue Baha ili baba afadhaike. Athanas alichokifanya alimpa hela Jacob (naye hajakamatwa) Sh1 milioni ili atekeleze kazi ya kumuua Baha. Mimi nilichokifanya ni kwenda kumuomba Baba gari ambalo dereva ni Baha (marehemu)”

“(Shahidi-Baba yao) akatupa gari na hela ya mafuta na Baha (marehemu) akiwa dereva. Tulienda…. (hukumu haikutaja eneo). Baada ya hapo Jacob akamchoma kisu shingoni Baha,”anaeleza mshitakiwa katika maelezo hayo ambayo ni kielelezo cha kesi hiyo.

Jaji Gladys Barthy wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Manyara katika hukumu yake aliyoitoa Aprili 8, 2024 na nakala yake kupatikana katika mtandao wa mahakama leo Aprili 14, amemhukumu Kwaslema kunyongwa hadi kufa kwa mauaji hayo.

Ushahidi uliomtia hatiani

Mbali na maelezo ya kukiri kosa, shahidi wa tano ambaye ni mke wa Baatael Bayi (marehemu), Theresia Martin, aliieleza Mahakama kuwa alikuwa akiishi na baba wa mumewe, na siku ya tukio, mshitakiwa alimuaga anakwenda kuoa na kuleta mke.

Kulingana na ushahidi wake akiongozwa na mawakili wa upande wa mashitaka, shahidi huyo alieleza kuwa shemejie huyo aliondoka na Baatael (mumewe) na Baha wakitumia gari ambayo ni mali ya baba yao ambaye alikuwa shahdi wa nne, Kwaslema Warey.

Kwenye saa 7:00 usiku, alisikia mlio wa gari na alimuona mshitakiwa na aliweza kumtambua kwa kutumia mwanga wa sola, akiwa ameongozana na mtu asiyemjua.

Alitoka kwenda kumpokea mke huyo lakini hata hivyo, akiwa anaelekea kwenye gari alisita, lakini mshitakiwa alimtaka aendelee kwenda na alipomfikia alimtaka ampe simu, alikataa na ndipo mshitakiwa alimwambia ameshawaua Baha na Baatael.

“Alimweleza kuwa ameshachinja Baha na Baatael na kwamba mlengwa aliyebaki ni yeye (Theresia). Walianza kumpiga hadi akapoteza fahamu. Alipozinduka alijikuta akiendelea kupigwa na mshitakiwa na mshirika wake. Baadaye alifungwa kamba,”alieleza Jaji.

Akirejea ushahidi huo, Jaji alisema baadaye walimtupa na alifanikiwa kujifungua kamba mwenyewe na kurudi nyumbani wakati huo ikiwa imetimu saa 10:00 alfajiri.

Alipofika nyumbani, alimkuta mshitakiwa na mshirika wake wakiongea na shahidi wa nne ambaye ni baba yake akimuomba atumie simu yake wakidai wanafanya maandalizi ya kuchinja kondoo maalumu kwa ajili ya mke au mchumba aliyekuwa amekuja naye.

Shahidi huyo wa tano baada ya kufika hapo alimjulisha baba mkwe wake nini kimetokea, ambaye alipiga ukunga wa kuomba msaada na kwamba licha juhudi zao hizo hazikuzaa matunda kwa sababu hawakupata msaada wa haraka hadi saa 12:00 na 1:00 asubuhi.

Shahidi mwingine ambaye ni askari polisi E.8080 Sajeni Jimmy aliyekuwa mpelelezi wa kesi hiyo, alieleza kuwa Desemba 5,2019 saa 11:00 alfajiri, alijulishwa na mkuu wa upelelezi Babati (OC-CDI), Richard Mwaisemba juu ya mauaji hayo.

OC-CID na yeye walifika eneo la tukio katika nyumba ya shahidi wa nne saa 12:15 asubuhi  na kukuta umati wa watu nje, mwenyekiti wa kitongoji, Fabian Sanka aliwaonyesha gari lenye namba za usajili T446 DJN aina ya Toyota Noah rangi ya fedha.

Ndani ya gari hiyo waliona mwili wa mtu aliyekufa, OC-CID alifungua gari hilo na kuonyesha mwili uliokiwa umelala kwenye kiti cha abiria huku kichwa kikielekea upande wa mlango, na mwili huo ulikuwa ulikuwa na majeraha na kukiwa na dimbi la damu.

Mwili huo ulitambuliwa kuwa ni wa Baha Kwaslema ambaye ni ndugu na baada ya hapo walipelekwa kwenye mwili mwingine uliokuwa kama hatua 150 kutoka kwenye nyumba ya shahidi wa nne wa Jamhuri, ukiwa umefichwa kwenye kibanda cha kufugia ng’ombe.

“Walimtoa nje, kichwa chake kilikuwa kina jeraha la kukatwa na kitu chenye ncha kali na alikuwa amepoteza damu nyingi na alikuwa ameshakufa,”alieleza Jaji Gladys Barthy.

Waliichukua miili hiyo na kuipeleka Hospitali ya Misheni ya Dareda na Desemba 9, 2019 mwili huo ulifanyiwa uchunguzi na shahidi wa kwanza, Dk Astery Dangati, alichunguza mwili wa kwanza na ukiwa na jeraha kubwa la kitu kikali kwenye shingo.

Kuhusu mwili wa pili, Dk Dangati alisema katika ushahidi wake kuwa kama ilivyokuwa kwa marehemu wa kwanza, naye wa pili alikuwa na jeraha kubwa la kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni, na majeraha hayo ndio yalisababisha moyo wao kusimama.

Muuaji alivyonaswa Mto wa Mbu

Shahidi wa tatu, Sajini Jimmy alisema Desemba 20,2022 alipokea taarifa kutoka kwa OC-CID aliyemtaja kuwa ni Songalaeli Jwagu kuwa Kwaslema (mshitakiwa) ameonekana Mto wa Mbu, ndipo alipagizwa na mabosi wake kwenda eneo aliloonekana.

Baada ya kufika, shahidi huyo alifanikiwa kumbaini mshitakiwa akiwa kwenye baa moja na kufanikiwa kumkamata saa 8:00 mchana na walimpeleka Kituo cha Polisi cha Mto wa Mbu na siku iliyofuata saa 9 alfajiri walianza safari ya kumrejesha Babati.

Wakiwa njiani katika Hifadhi ya Manyara, mshitakiwa aliruka kwenye gari lililokuwa katika mwendo likiwa karibu na eneo la JK na shahidi alipiga kelele za kuomba msaada na baada ya kumtafuta kwa muda, alikamatwa saa 5 asubuhi akiwa na pingu.

Walipofika Babati, mtuhumiwa huyo alihojiwa na kuandika maelezo ya onyo na alikiri kufanya mauaji hayo akishirikiana na watu aliowataja kwa majina ya Qaray Kwasiema, Athanas Kwasiema na mwingine aliyetajwa kwa jina moja tu la Jacob.

Desemba 27, 2022, shahidi huyo alimpeleka mtuhumiwa huyo kwa mlinzi wa amani, Hafsa Anzuruni ambaye alitoa ushahidi wake kama shahidi wa pili ambako nako alikiri kufanya mauaji hayo na kwa ushahidi huo Mahakama ikamuona ana kesi ya kujibu.

Alivyojitetea kortini

Katika utetezi wake, mshitakiwa alikanusha kuwaua ndugu zake hao na kueleza kuwa Desemba 4 na 5, 2019 muda wote alikuwa akifanya shughuli za kilimo na alijulishwa tu kuwa kuna watu wameuawa nyumbani kwao na alirudi nyumbani.

Huko alikuta watu wakiimba nyimbo za maombolezo na Desemba 9, 2019 alishiriki katika mazishi ya ndugu zake hao lakini akakanusha madai kuwa  kutumia gari ya baba yake kwa ajili ya shughuli za harusi yake na alikuwa akiishi Bashnet na sio Gabadaw.

Alikanusha kutoroka baada ya mauaji hayo na kueleza kuwa alikamatwa Desemba 17,2019 akiwa Mto wa Mbu nyumbani kwa dada yake na kufungwa kitambaa na kufungwa pingu na kusema alipigwa na kulazimishwa na polisi kusaini nyaraka.

Hata hivyo, pamoja na utetezi wake huo, Jaji aliukataa akisema ushahidi wote uliotolewa na upande wa Jamhuri unamnyooshea kidole kutenda kosa hilo na kwamba upande wa mashitaka umeweza kuthibitisha shitaka la mauaji pasipo kuacha mashaka yoyote.

Hivyo Jaji alisema adhabu pekee ya mtu anayepatikana na hatia ya mauaji ya kukusudia ni kunyongwa hadi kufa hivyo naye anamhukumu adhabu hiyo kwa mujibu wa sheria kwa kuwa mikono yake imefungwa kutoa adhabu tofauti na hiyo.