Aliyewahi kuwa RPC Zanzibar akutwa amekufa nje ya nyumba yake

Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mohamed Hassan Haji, Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Juni 9, 2019,

Muktasari:

  • Aliyewahi kuwa RPC Mkoa wa Mjini Magharibi visiwani Zanzibar, amekutwa amefariki nje ya nyumba yake iliyopo Kijichi Zanzibar. Jeshi la polisi Zanzibar limesema kifo chake kina utata.

Unguja. Aliyewahi kuwa kamanda wa polisi mkoa wa mjini magharibi Unguja, Azizi Juma Mohamed amekutwa amefariki dunia asubuhi ya kuamkia leo nje ya nyumba yake Kijichi Zanzibar.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Juni 9, 2019, Kamishna wa Polisi, Zanzibar, Mohamed Hassan Haji amekiri kutokea kwa kifo hicho alichosema kina utata, kwa kuwa si cha kawaida.

Hata hivyo, amesema licha ya uwapo wa tetesi kuwa Azizi amejinyonga nje ya nyumba yake huko Kijichi, amesema hawezi kueleza kwa kina taarifa hizo kwa sasa.

Amesema bado ni mapema na wanaendelea na uchunguzi, baada ya kubainika sababu ya kifo chake watatoa taarifa zaidi.

“Naomba utosheke na hapo kwa sasa najua mnataka kujua kuhusu tukio hili na muda ukifika mtaelezwa kilichotokea,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi, Mkuu wa kitengo cha uchunguzi kutoka Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja mjini Unguja, Dk Msafiri Marijani, amesema ni kweli wamepokea mwili wa ofisa huyo wa polisi hospitalini hapo.

Amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa kifo cha askari huyo si cha kawaida ingawa taarifa zaidi watatoa wahusika.

Hata hivyo, amesema tayari wamechukua sampuli ya damu kwa uchunguzi zaidi huku baadhi ya maofisa wakiwa tayari wameshaelekea eneo la tukio kwa ajili ya uchunguzi.