Wakulima milioni 1.3 kunufaika na teknolojia ya kidigitali ya afya ya udongo
Mtafiti Mwandamizi wa Kituo cha Tari-Uyole, Dk Denis Tippe, akitoa elimu kwa wakulima wa Kijiji cha Uturo kuhusu matumizi ya mifumo ya kidigitali kupitia simu za mkononi ili kupata taarifa sahihi za matumizi ya mbolea na afya ya udongo. Picha na Hawa Mathias.
Muktasari:
- Mradi huo utatekelezwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari) katika mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa na Ruvuma kupitia mfumo wa kidigitali utakaowawezesha wakulima kupata mapendekezo sahihi ya matumizi ya mbolea kulingana na afya ya udongo.
Mbeya. Zaidi ya wakulima milioni 1.3 katika mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa na Ruvuma wanatarajiwa kunufaika na mradi wa kidigitali wa utambuzi wa afya ya udongo na matumizi sahihi ya mbolea, unaolenga kuongeza uzalishaji wa mazao ya kimkakati, yakiwemo mahindi, mpunga na viazi mviringo.
Mradi huo unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari), kupitia Kituo cha Uyole, na Fondation OCP Tanzania, utatekelezwa kwa awamu tatu ambazo ni uanzishaji wa mashamba darasa, upimaji wa afya ya udongo na utengenezaji wa ramani za udongo kwa ajili ya kutoa mapendekezo sahihi ya matumizi ya mbolea.
Akizungumza leo Ijumaa, Juni 26, 2026, jijini Mbeya, Mtafiti Mwandamizi wa Masuala ya Afya ya Udongo kutoka Tari-Uyole, Fredrick Mlowe, amesema mradi huo unalenga kuwainua wakulima kiuchumi kwa kuongeza tija ya uzalishaji na kipato kupitia matumizi ya teknolojia ya kidigitali.
Amesema teknolojia hiyo itawawezesha wakulima kupata mapendekezo sahihi ya aina na kiwango cha mbolea kupitia simu za mkononi kulingana na hali ya udongo katika maeneo yao.
Mlowe amesema kabla ya kuanza kutumika rasmi kwa mfumo huo, watafiti wamefanya majaribio katika zaidi ya maeneo 23 nchini kwenye mazao ya mahindi, mpunga na viazi mviringo, sambamba na kuanzisha mashamba darasa 25 kwa ajili ya kuonyesha matumizi sahihi ya mbolea.
"Tumeshafanya majaribio katika maeneo zaidi ya 23 nchini na kuanzisha mashamba darasa 25. Kwa sasa yako katika hatua ya mavuno, na matokeo yanaonyesha teknolojia hii ina uwezo mkubwa wa kuongeza uzalishaji," amesema.
Amesema lengo la mradi huo ni kuwafikia zaidi ya wakulima milioni 1.3 katika mikoa hiyo ili kuongeza tija ya uzalishaji na kuinua kipato chao.
Kwa upande wake, Mtafiti Mwandamizi wa Tari-Uyole, Dk Denis Tippe, amewahimiza wakulima kutumia mbegu bora na miche yenye umri unaoshauriwa kitaalamu ili kuongeza mavuno.
Amesema matokeo ya mashamba ya majaribio yanaonyesha wakulima waliotumia teknolojia hiyo waliongeza uzalishaji kutoka wastani wa magunia 30 hadi 46 kwa ekari, sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 50.
Naye mtafiti wa Tari, Watson Matamwa, amewashauri wakulima kupanda miche yenye umri wa siku 14 hadi 21 na kuweka mbolea ya kupandia ndani ya siku saba baada ya kupandikiza ili mimea iweze kufyonza virutubisho kwa ufanisi.
Bwana Shamba wa Fondation OCP Tanzania, Hemed Mayanda, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya kilimo na kushirikiana na Tari kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kupitia mashamba darasa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Uturo, Katekista Musa Kivambe, amesema elimu inayotolewa na watafiti imeanza kubadili mtazamo wa wakulima kutoka kilimo cha mazoea kwenda kilimo kinachozingatia matokeo ya tafiti za kisayansi.
"Tulikuwa tunatumia mbegu za zamani na mbolea ya Urea pekee bila kuzingatia muda sahihi wa matumizi. Elimu tuliyoipata kutoka Tari imetufungua, na tunaamini itachochea ongezeko la uzalishaji na kipato cha wakulima," amesema Kivambe.