‘Amani ni mbolea ya mafanikio’
Muktasari:
- Naibu Katibu Mkuu Misioni na Uinjilisti wa Kanisa la KKKT, Dayosisi ya kaskazini Kati Mchungaji Julius Tarakwa,amesema mwaka 2025 haukuwa mwepesi na kuwa amani inakuza mafanikio na ustawi.
Arusha/Manyara. Watanzania wametakiwa kuendelea kumuomba Mungu ili amani iendelee kudumishwa nchini, wakikumbushwa kuwa amani ni msingi muhimu unaochochea mafanikio na ustawi wa jamii.
Wito huo umetolewa leo Alhamisi, Januari Mosi, 2026 na Naibu Katibu Mkuu wa Misioni na Uinjilisti wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, Mchungaji Julius Tarakwa alipokuwa akihubiri katika ibada ya Mwaka Mpya kwa niaba ya Askofu wa Dayosisi hiyo, Dk Godson Mollel.
Akizungumza katika ibada hiyo iliyofanyika katika Kanisa Kuu la KKKT Usharika wa Arusha Mjini, Mchungaji Tarakwa amesema amani ni hitaji la msingi katika maisha ya binadamu na maendeleo ya jamii kwa ujumla.
“Tunahitaji amani na furaha ili tuweze kufanikiwa. Amani ni hitaji la msingi, ndiyo maana hata katika ibada za Krismasi tulisisitiza juu ya amani, kwa kuwa amani ni kama mbolea inayokuza na kutunza mafanikio na ustawi katika ngazi mbalimbali,” amesema.
Aidha, amewakumbusha waumini kuwa mwaka 2025 haukuwa mwepesi, hasa kutokana na matukio yaliyotokea mwishoni mwa mwaka na kusababisha baadhi ya watu kupoteza maisha, hivyo waliobaki hai wanapaswa kumshukuru Mungu kwa neema ya uhai.
“Tuendelee kuomba ili tupate majibu ya mahitaji yetu. Mwaka 2025 haukuwa mwepesi, na katika matukio ya mwisho wa mwaka tumepoteza wenzetu. Sisi tuliobaki hai tunapaswa kumshukuru Mungu kwa kuwa waliopata madhara ni watu kama sisi,” ameongeza.
Mchungaji Tarakwa amesisitiza mwaka 2026 unapaswa kuwa wa kubadili fikra katika kumtegemea Mungu, kujenga uhusiano wa karibu naye na kuimarisha maisha ya kiroho.
“Mwaka huu ni mwaka wa kuwa karibu na Mungu. Tunahitaji ulinzi wa Mungu ili majaribu na adui wanapojaribu kutuangusha wasiweze kufanikiwa,” amesema.
Amesema Mungu ana moyo wa huruma kwa wanadamu na kwamba, wale waliopata neema ya kuuona mwaka 2026 wanapaswa kutambua kuwa ni kwa huruma za Mungu pekee zilizowafanikisha kufika mwaka mpya.
Wakati huo huo, Paroko Msaidizi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Rozali Takatifu iliyopo katika mji mdogo wa Mirerani, wilayani Simanjiro mkoani Manyara, Padri Krisantus Assenga ameiasa jamii kuanza mwaka mpya wa 2026 kwa kuacha vinyongo na visasi.
Padri Assenga ametoa wito huo kupitia salamu zake za mwaka mpya, akisisitiza kuwa waamini hawapaswi kubeba chuki mioyoni mwao, bali waanze mwaka wa 2026 kwa kutafakari, kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo badala ya kuendelea kukumbatia makosa na maumivu ya yaliyopita.
Amesema kufanikiwa kumaliza mwaka 2025 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2026 ni neema kubwa inayopaswa kushukuriwa, akibainisha kuwa si kila mtu alipata fursa ya kufikia hatua hiyo.
“Nawatakia heri na baraka tele katika kipindi hiki cha mwaka mpya wa 2026. Uwe mwaka wenye neema, uzima, afya njema na mafanikio,” amesema Padri Assenga.