Askofu Nzigilwa awausia mapadre wapya

Muktasari:
- Mapadre hao wapya tisa pamoja na mambo mengine wametakiwa kuwa tayari kufanya kazi mahali popote watakapopangiwa na kutatua migogoro katika jamii.
Dar es Salaam. Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa amewapandisha mashemasi tisa kuwa mapadre katika ibada maalum iliyofanyika katika Kanisa la Msimbazi, Ilala jijini Dar es Salaam.
Ibada hiyo ilihudhuriwa na mamia ya waumini wa kanisa hilo wakiongozwa na Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo.
Mapadre hao ni Alfonce Ntakwezile, Danipaso Bitegeko, Francis Malele, Frank Mtavangu, Simon Shija, Conrad Mutayoba, Hermenegild Mushi, Patrick Ngomesha na Christopher Mapunda.
Akitoa mahubiri, Askofu Nzigilwa aliwataka mapadre hao kuwa karibu na waumini wao popote watakapopangiwa kufanya kazi.
“Msijifungie ofisini nendeni mkatoe huduma kwa waumini wenu, hamasisheni amani na kutatua migogoro iliyopo,” amesema.
Nzigilwa aliwataka mapadre hao kutochagua vituo vya kufanya kazi bali wawe tayari kufanya kazi mahali popote.