Prime
Uende haja kubwa mara ngapi kwa siku, wiki?

Muktasari:
- Kwa mujibu wa wataalamu wa afya upatikanaji wa haja kubwa hutegemea aina ya vyakula vinavyoliwa, kiwango cha maji mtu anachokunywa, mazoezi anayofanya na dawa anazotumia.
Dar/Geita. Kumekuwa na mitazamo tofauti kuhusu kwenda haja kubwa kwa siku. Wapo waendao mara tatu, huku wengine kwao ni tukio adimu na maalumu.
La muhimu la kujifunza ni kuwa, namna uendevyo msalani unaweza kufichua jambo kuhusu afya yako, wataalamu wa afya wakieleza uendaji haja kubwa hutofautiana kati ya mtu na mtu.
Uelewa wa jamii
Akizungumza na Mwananchi, Juma Said, mkazi wa Temeke jijini Dar es Salaam anasema hukaa hadi siku tano pasipo kupata haja kubwa.
"Nakaa siku nyingi bila kupata choo, nilienda kuonana na daktari, alinishauri niwe natumia vyakula vyenye kambakamba na maji mengi,” anasema.
Zainab Salum, mkazi wa Tabata jijini humo anasema: "Sina uhakika, lakini nadhani mtu anatakiwa kujisaidia mara moja kwa siku, inategemea aina ya chakula alichokula,” anasema.
Rehema Juma, mkazi wa Bomani mjini Geita, anasema hupata haja mara chache kwa wiki, jambo ambalo awali lilimpa shida, lakini sasa ni la kawaida kwake baada ya kupata ushauri wa kitabibu.
“Wakati mwingine nakaa zaidi ya siku tatu hadi tano bila kupata choo, lakini siumwi. Choo changu huwa cha kawaida. Nikimweleza mtu anapata mshangao, nimeshazoea na naona kawaida,” anasema.
Rehema anasema alishauriwa na familia kwenda hospitali, ambako baada ya vipimo alionekana hana tatizo, akatakiwa kula lishe bora na kunywa maji zaidi.
“Nikisafiri ugenini huwa sipati choo kabisa mpaka nirudi nyumbani au nizoee mazingira. Lakini sijawahi kuugua kwa sababu ya kukosa choo,” anaeleza.
Baraka Yusuph, mkazi wa mtaa wa Mission, Mjini Geita anasema: “Kila siku hupata choo asubuhi. Nisipokwenda siwi sawa, tumbo huvurugika, nahisi kuumwa.”
Madaktari wanasemaje?
Daktari bingwa wa upasuaji na mtaalamu wa uchunguzi wa mfumo wa chakula kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa, Ahmed Binde anasema kila mtu ana mfumo wake wa kupata haja kubwa.
"Kutopata choo kila siku si tatizo kwa kila mtu. Kila mtu ana mpangilio wake wa kawaida wa choo. Wapo wanaopata kila siku, na wengine mara tatu kwa wiki, na hiyo bado huchukuliwa kuwa kawaida,” anasema Dk Binde.
Anasema upatikanaji wa haja kubwa hutegemea aina ya vyakula vinavyoliwa, kiwango cha maji mtu anachokunywa, mazoezi anayofanya na dawa anazotumia.
Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa chakula na ini kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Swalehe Pazi anasema binadamu anapaswa kupata haja kubwa angalau mara moja kwa siku.
"Ikitokea siku moja imepita bila kupata haja kubwa, hiyo siyo hali ya kawaida. Ikijitokeza unatakiwa ujue shida ni nini na ushughulike nayo. Pia yapo maradhi yanayosababisha mtu asipate choo, hivyo ni vema kujua ni ugonjwa gani, wakati mwingine utumbo unaweza kuwa umejifunga hata kama ni kwa siku moja,” anasema na kuongeza:
"Siyo suala la kudharau, lazima ufanye uchunguzi, uchukue hatua. Lakini wapo wagonjwa ambao wanashauriwa wapate choo angalau mara tatu kwa siku. Kama hafanyi hivyo, tunampa dawa ili apate.
“Maradhi kama ini, mgonjwa asipopata choo, sumu zitatuama, zitapita katika utumbo, zitaingia kwenye damu, mwisho zitafika kwenye ubongo. Lakini akipata choo, zinatoka."
Hata hivyo, anasema kupata haja kubwa pia hutegemea mazingira, saikolojia ya mtu, akibadili choo au akiwa safarini.
"Mtu ambaye hapati choo, maana yake anashindwa kuondoa sumu katika mwili wake zinazoweza kutoka kwa njia ya mfumo wa haja kubwa. Haja kubwa ni matokeo ya tendo la usagaji wa chakula, hivyo husaidia kutoa sumu zinazoweza kusababishwa na bakteria kwenye utumbo au kwenye vyakula vyenyewe. Sumu zisizotoka zinaweza kuathiri figo, moyo na hata ubongo," anasema.
Dk Pazi anasema ni vyema jamii ikafahamu kuwa aina ya haja kubwa inaweza kutafsiri hali ya kiafya ya mtu husika.
"Choo cha majimaji au kigumu ni tatizo, kawaida kinatakiwa kutoka cha hali ya kati. Choo kama jiwe au kama karanga ni tatizo. Pia katika rangi yake, ukiona cheusi au cheupe, shtuka. Kwa hiyo, rangi na aina yake inatafsiri tatizo kama lipo au halipo,” anasema.
Anasema wakati mwingine ulaji wa mtu ndiyo huamua aina ya haja kubwa, akisisitiza ulaji wa vyakula vyenye nyuzi lishe kama vile mboga za majani, matunda na nafaka zisizosindikwa.
"Choo kinatengenezwa na ulaji. Ili upate kibaya, maandalizi yatakuwa mabaya. Mfano, kula chakula kichafu lazima utaharisha. Ukila supu na chapati, kula na mboga za majani peke yake, lazima upate choo kigumu,” anasema na kuongeza:
"Lakini kama hauli kwa wakati, usitegemee kupata choo kwa wakati. Mfumo wa kujisaidia utaenda kwa wakati sawa na wewe unavyojituma.”
Kwa upande wake, Dk Sadam Kimanga anayehudumu katika Hospitali ya Ilembula Lutheran mkoani Njombe anasema upatikanaji wa haja kubwa unategemeana na kiwango cha chakula anachokula mtu.
Hata hivyo, anasema kitaalamu mtu mzima hatakiwi kuvuka siku nne bila kupata haja kubwa.
"Anavyokula zaidi, tunategemea aende chooni mara nyingi. Japo tunategemea mtu mzima asivuke siku nne bila kupata choo. Watoto wanaonyonya, kwa kuwa ni chakula chenye kimiminika, kinachukua muda mrefu kutengeneza choo. Yeye anaweza akaenda hata siku saba bila ya kupata choo, inategemeana na kiwango cha maziwa ya mama na unyonyaji wa mtoto," anasema.
Anasema vyakula vinavyotumia muda mfupi kumeng’enywa husababisha mtu kupata haja kubwa mara kwa mara.
Dk. Kimanga anasema: "Kuna mazingira na hali ya mwili kama wasiwasi inaweza kusababisha mzunguko wa tumbo kuwa maradufu. Ndani vitu vinakuwa vinatembea kwa kasi, ndiyo maana wengi huwa wanapata hali ya kuharisha wanapokuwa na wasiwasi."
Anaonya kwamba kutopata choo kwa muda mrefu ni changamoto ambayo haipaswi kufanyiwa mzaha.
Dalili za hatari
Dk Binde anasema zipo dalili ambazo zikitokea zinaashiria kuna tatizo, hivyo ni vema mtu kutafuta msaada wa kitabibu mapema.
Dalili hizo anasema ni tumbo kujaa au kuuma mara kwa mara, kinyesi kutoka kwa shida au kuwa kigumu sana, kwenda haja chini ya mara tatu kwa wiki, kutapika au kupoteza hamu ya kula, kutokwa damu wakati wa kujisaidia, na wale ambao ili wapate haja lazima wameze dawa kuwasaidia.
Anasema kwa uzoefu wake, wagonjwa wenye matatizo ya kupata haja mara kwa mara ni wazee ambao uwezo wao wa kumeng’enya chakula hupungua.
Wengine ni wajawazito ambao hupata tatizo kutokana na mabadiliko ya homoni na shinikizo la mtoto, watoto wadogo hasa wanaoanza kula vyakula vigumu, watu wanaotumia dawa za maumivu au za akili, wagonjwa waliolazwa muda mrefu, na waliopata kiharusi au upasuaji.
Anasema kukosa haja kwa muda mrefu kunaweza kusababisha bawasiri inayotokana na kujikaza, mpasuko kwenye njia ya haja, na kuzuia njia ya haja hivyo kinyesi kigumu hukwama, upungufu wa hamu ya kula, na gesi tumboni.
Dk Binde anasema mtu anaweza kupata matatizo ya kibofu cha mkojo na mkojo kushindwa kutoka vizuri. Pia wengine hupata maradhi kama vile uvimbe wa utumbo au saratani.
Anasema wapo watu ambao wanapokosa haja kubwa hukimbilia dawa za kuharisha, jambo analosema si salama kwa afya.
"Hapana, si sahihi kutumia dawa za kuharisha bila ushauri wa daktari. Zinaweza kusababisha mwili kutegemea dawa, hivyo kuharibu utendaji wa kawaida wa utumbo,” anasema.
Anasema si kila dawa inafaa kwa kila mtu, bali hutolewa kulingana na chanzo cha tatizo na hutumika kwa muda maalumu.
Kwa mujibu wa Dk Binde, mtu anapaswa kutafuta ushauri wa daktari haraka anapogundua hajapata haja kubwa kwa siku nyingi mfululizo, anapata choo mara chache kwa wiki kadhaa, anapopata choo kigumu kwa kiwango cha kujikaza sana, na anapoona mabadiliko kwenye mfumo wa haja.
Anasema tatizo la kukosa haja kubwa lipo duniani kote, kiwango cha maambukizi kikiwa kati ya asilimia 10–20. Anasema wakati wastani wa dunia ukiwa na asilimia 14 ya tatizo, Afrika makadirio ni kati ya asilimia tano hadi 12.
Anasema kiwango hicho kiko chini ikilinganishwa na nchi za Magharibi, na hili linatokana na ulaji wa vyakula vyenye nyuzi lishe na maisha yenye shughuli nyingi, hususani vijijini.
Dk Binde anasema kwa Tanzania makadirio ni kati ya asilimia saba hadi 11, lakini hakuna takwimu za kitaifa zilizo wazi.
Anasema tafiti ndogondogo za hospitali na maeneo maalumu zinaonyesha idadi ya wagonjwa inaongezeka hasa maeneo ya mjini.
Usuli
Fahamu zaidi
Vigezo vinavyoonyesha afya ya haja kubwa ni pamoja na: Muda wa kawaida wa kuipata mfano kila asubuhi. Umbo na umbile la kinyesi kuwa kigumu kiasi (si kigumu sana wala chepesi sana). Kinaweza kufananishwa na umbo la ndizi. Hakuna maumivu au kuambatana na damu. Hakuna kuharisha au kufunga choo mara kwa mara.