Bashungwa awabana makandarasi wazembe

Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa, (kushoto) akizungumza wilayani Babati Mkoa wa Manyara, kwenye hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa barabara ya kilomita 60 ya Dareda - Dongobesh,  eneo la Dareda Centre hadi Dareda Mission. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

Makandarasi wazembe hawatapatiwa zabuni ya utengenezaji wa barabara nchini

Babati. Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameuagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), kutowapa zabuni ya utengenezaji wa barabara makandarasi wazembe.

Waziri Bashungwa amesema hayo leo Jumamosi Aprili 6, 2024 kwenye hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa barabara ya kilomita 60 ya Dareda - Dongobesh, eneo la Dareda Centre hadi Dareda Mission yenye urefu wa kilomita saba.

Amesema makandarasi wazembe na wababaishaji wasipewe zabuni ya utengenezaji barabara kwa sababu wanachangia kukwamisha na kuchelewesha maendeleo ya maeneo husika.

"Msicheke na makandarasi wazembe ambao hawafanyi kazi zao ipasavyo, kule Songea mkoani Ruvuma tulimuondoa mkandarasi mbabaishaji ambaye alifanya kazi kwa kusuasua," amesema Bashungwa.

Hata hivyo, amesema anatarajia mkandarasi aliyepewa zabuni ya ujenzi wa barabara ya kilomita saba ya Dareda Centre hadi Dareda Mission kukikamilisha kwa wakati.

"Barabara hii ya kilomita 60 kutoka Babati hadi Dongobesh wilayani Mbulu itajengwa kwa awamu mbili, tunaanza na awamu ya kwanza kilomita saba na kilomita 53 zilizobaki za kutoka Dareda hadi Dongobesh nazo zitajengwa," amesema Bashungwa.

Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mohamed Besta amesema barabara hiyo itajengwa na Kampuni ya M/s Jiangxi Geo Engineering (Group) Corporation ya China kwa gharama ya Sh9.88 bilioni.

Besta amesema zabuni kwa ajili ya ujenzi wa sehemu ya pili, Dareda Mission hadi Dongobesh wa kilomita 53 inatarajiwa kutangazwa mwaka wa fedha 2024/25.

"Natoa wito kwa mkandarasi kufanya kazi yake kwa weledi wa hali ya juu ili kazi zote zikamilike ndani ya muda uliopangwa na kwa viwango na gharama zilizokubalika," amesema Best.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga ameishukuru Serikali kwa kuipatia zaidi ya Sh600 bilioni ya miradi ya maendeleo mkoani humo.

Sendiga amesema Serikali imetoa Sh32 bilioni kwa Tanroads mkoani Manyara na kuwapongeza viongozi wake kwa namna wanavyosimamia ujenzi.

"Ujenzi wa barabara hii itachochea uchumi wa wakulima ila ni matumaini ya wana Manyara barabara zinazoungamisha mikoa ziwe za lami," amesema Sendiga.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo ambaye ni mbunge wa Babati vijijini amesema makandarasi wa barabara hiyo wafanye kazi kwa umakini, uadilifu na thamani ya fedha ionekane.

"Tunaishukuru Serikali kwa ujenzi wa barabara hii ambayo ikikamilika itakuwa na manufaa makubwa kwa jamii na wana Manyara kwa ujumla," amesema Sillo.

Mbunge wa Mbulu Vijijini, Flatei Massay amesema anatarajia ujenzi wa kipande cha kilomita 53 cha barabara kilichobaki hadi kufika Dongonesh, kitajengwa.

"Leo sipigi sarakasi tena kwa kuwa natarajia hivi karibuni ujenzi wa barabara hii hizo kilomita 53 zilizobaki na kuunganisha Mbulu zitajengwa," amesema Massay.

Mkazi wa Dareda Mission, Julius Salawe amesema ukamilishaji wa barabara hiyo utawanufaisha wakazi wa eneo hilo kwa kuwa watasafirisha mazao yao kwa urahisi.