Bashungwa ashangaa wingi wa makandarasi wazawa bila kazi

Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa.

Muktasari:

  • Waziri huyo amesema kwa idadi ya Makandarasi wazawa na kazi walizonazo hazitishi hata ukubwa wa punje ya mchele wakigawana kila mmoja.

Dodoma. Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa amesema licha ya wingi wa wakandarasi wazawa, tenda wanazopewa haizidi asilimia 46.

Kutokana na hilo, ameagiza haraka uitishwe mkutano wa wakandarasi wazawa ili wajifungie na kujadili pamoja namna wanavyoweza kutoka walipo sasa huku akisisitiza ushirikiano.

Kwa mujibu wa Waziri Bashungwa, idadi ya makandarasi waliosajiliwa nchi wako 14,800 ambapo wazawa wako 143,000 wakati wageni wapo 500.

Akizungumzia leo Jumatatu Novemba 6, 2023 kwenye uzinduzi wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Waziri amesema hali hiyo siyo nzuri.

Waziri amesema ipo haja kuangalia jambo hilo kwa mawanda mapana kwani haina tija kama watu ni wengi lakini kazi wanazozifanya ni kidogo ambazo zikigawanywa kwa mtu mmoja inakosa maana kabisa.

Bashungwa amesema ipo haja ya kuwaida pamoja wakandarasi wazawa ili wajadiriane na kuona namna gani wanavyoweza kuwasaidia.

"Kwenye mkutano huo nimewaita Waziri wa fedha Dk Mwigulu Nchemba na Waziri wa Mipango kaka yangu Profesa Kitila Mkumbo ili waje tusaidiane kwenye hili na tuone tunatokaje," amesema Bashungwa.

Waziri amesema habari za kulia na kunung'unika kuwa hazina hazi sasa zifike mwisho ikiwa watu hao watajiunga pamoja.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Makandarasi, Joseph Nyamahanga amesema kitakachowavusha wazawa ni bidii, weledi na umakini na kwamba ndiyo itakuwa kipaumbele chao.

Nyamahanga amesema wakandarasi wazawa wanao uwezo kama wataamua kusimama pamoja na kufanya kile wanachotamani lakini akasema suala la kujengewa uwezo ni muhimu sana.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Aisha Amuru amesema muundo wa Bodi hizo upo kwa mujibu mwongozo na kanuni kwa sheria namba 17 ya 1997 ambayo inataka wawepo wajumbe wasiozidi nane.

Aisha amesema baada ya Bodi hizo kuundwa, kazi kubwa mbele yao ni kufanya kazi kwa ushirikiano na kujiamini.