Uzembe kiini kutokamilika miradi umeme vijijini

Muktasari:

  • Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umetaja sababu ya baadhi ya vijiji nchini kutofikiwa na nishati ya umeme ambayo ni kichocheo cha maendeleo, kuwa ni uzembe wa Makandarasi wazawa ambao hadi sasa kazi zao ziko chini ya asilimia 50.

Dar es Salaam. Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umetaja sababu ya baadhi ya vijiji nchini kutofikiwa na nishati ya umeme ambayo ni kichocheo cha maendeleo, kuwa ni uzembe wa Makandarasi wazawa ambao hadi sasa kazi zao ziko chini ya asilimia 50.

Taarifa za Rea zinaonyesha kuwa mradi wao wa Rea III awamu ya pili wenye thamani ya 1.5 trilioni ambao ulianza kutekelezwa 2021 na kwamba ulitakiwa kumilika Juni mwaka huu, ukihusisha Makandarasi 21, kati yao 14 ni wazawa.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (Reb) Janet Mbene, mradi kampuni zilizoshinda tenda hiyo, saba zilikuwa za kigeni na kwamba tano kati ya hizo, zimekamilisha kazi kwa asilimia 100.

Akizungumza jijini hapa leo Juni 16, 2023 baada ya kukutana na Wakandarasi wote na kusaini mkataba wa kuwaongezea muda, Mbene amesema katika uchunguzi waliofanya wamebaini makandarasi wazawa wamegeuka kuwa mawakala wa kutafuta kazi na kugawa kwa wakandarasi wadogo.

“Jambo hilo linasababisha mradi kushindwa kukamilika kwa wakati na watu kuendelea kukosa huduma hiyo muhimu. Lengo la serikali kutoa kazi nyingi kwa wazawa ilikuwa kuwapa uzoefu na kujiinua kiuchumi lakini fursa hiyo wanaitumia vibaya,” amesema.

Janet aliyewai kuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara amesema mradi huo hadi sasa ulitakiwa uwe umekamilika lakini kutokana na hali hiyo viongozi wa taasisi hiyo wanapokea malalamiko mengi kutoka kwa wabunge wa maeneo ambayo shughuli hizo haziendi.

“Hii kazi ni ya kisiasa kutokana na umuhimu wake katika kuchochea uzalishaji na inaleta maumivu na manung’uniko kama haijakamilika kwa wakati, nimeishakuwa kiongozi wa kisiasa najua changamoto zake,” amesema.

Baada ya kuongezewa muda wa kutekeleza mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Rea Mhandisi Hassan Saidy amewataka wakandarasi hao kukamilisha kazi zao kwa ubora na wakati na kwamba hicho kitakuwa kigezo cha kuwapa kipaumbele kwenye mradi mwingine.

“Hapa mnasaini mkataba wa nyongeza kwa kilomita mbili mbili lakini kama unakubali saini ikiwa unaona hutokamilisha kwa kuzingatia misingi ya mkataba huu bora uache kwakuwa tutakuwa makini kufautilia,” amesema.

Kwa upande wake Mkandarasi Bridget Temba, kutoka kampuni ya Derm Group amekiri mapungufu waliyoelezwa huku akiitaka taasisi hiyo kuhakikisha malipo yao wanalipwa kwa wakati.

“Mikataba yetu inaelezwa malipo yetu tutapatiwa ndani ya siku 21 baada ya kusaini lakini zinachelewa kutufikia na tukifuatilia benki wanatuambia bado Rea hawajathibitisha, inaturudisha nyuma kupata fedha ya kununua vifaa,” amesema.

Hata hivyo sababu hii inathibitisha juu ya taarifa mbalimbali kuwa baadhi ya makandarasi huchukua kazi bila kuwa na fedha za kufanyia kazi na kwamba husubiri malipo ya awali ndipo waweze kuanza shughuli katika miradi husika.

Kuhusu kugeuka mawakala, Temba amejitetea kwa kusema: “Shughuli zetu haziwezi kwenda bila kuwahusisha wakandarasi wadogo na hata taratibu zinawataka kulitumia kundi hilo kuwaunga mkono ili wafikie daraja la kwanza,” amesema.