Bodaboda watofautiana kauli na Lema

Waendesha bodaboda wakiwa barabarani .

Muktasari:

  • Ikiwa imepita wiki moja tangu mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, Godbless Lema aseme biashara ya bodaboda ni umaskini na laana, baadhi ya madereva wa vyombo hivyo wamekuja na maoni tofauti, wakiwamo wanaounga mkono kauli hiyo na wanaopinga.

Dar es Salaam. Ikiwa imepita wiki moja tangu mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, Godbless Lema aseme biashara ya bodaboda ni umaskini na laana, baadhi ya madereva wa vyombo hivyo wamekuja na maoni tofauti, wakiwamo wanaounga mkono kauli hiyo na wanaopinga.

“Wakati ninyi mnanipokea kwa shangwe mimi moyo wangu ulikuwa unahuzunika, bodaboda sio ajira, ni umaskini uliopitiliza. Aah! Jamani tukae na Serikali vizuri sisi bodaboda, hiyo ni ajira ya laana ikemeeni, hamwezi kufanya ajira ya kukimbiza upepo kwa Sh7,000 kwa siku, no men. Hapana,” alisema Lema katika hotuba yake ya kwanza baada ya kurejea nchini akitokea Canada wiki iliyopita jijini Arusha.

Hata hivyo, mtaalamu wa tiba kwa njia ya mazoezi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu, Mihayo Thobias alisema kuendesha bodaboda kwa muda mrefu ni chanzo kimojawapo cha magonjwa yasiyoambukiza, ikiwamo maumivu ya mgongo kwa muda mrefu.

“Mitikisiko ya mara kwa mara huchangia maumivu ya mgongo kwa anayeendesha bodaboda, hivyo kuingia kwenye hatari ya kupata ugonjwa kutokana na kukaa muda mrefu. Mbali na athari hiyo, pia kutokana na upepo mkali wakati wa uendeshaji wa bodaboda dereva hupata matatizo ya kifua,” alisema Dk Thobias.


Bodaboda wanena

Wakizunguza jana kwa nyakati tofauti kuhusu kauli ya Lema, baadhi walisema kazi hiyo imewasaidia kuendesha maisha yao huku wengine wakisema wamekimbilia shughuli hiyo kwa kukosa ajira.

Rajab Machipi, bodaboda aliyefanya kazi hiyo zaidi ya miaka kumi alisema kwa kipindi hicho amefanikiwa kuishi kwa kulipia kodi ya nyumba Sh30,000 kila mwezi, kuhudumia familia ya watu watano kwa kipato cha Sh20,000 kila siku, sawa na Sh600,000 kwa mwezi.

“Bodaboda siyo umaskini, ila changamoto zinazoturudisha nyuma ni ushuru wa Sh36,000 kila mwaka za halmashauri kwa ajili ya maegesho, Sh27,000 inayokwenda Latra, Sh79,000 ya Bima isiyokuwa na msaada sana, pia gharama za mafuta zinaathiri mapato yetu,” alisema Machipi.

Dominik Mganga alianza bodaboda miezi miwili iliyopita baada ya kuachana na kazi ya kuuza miwa na sasa anaingiza wastani wa Sh15,000 kwa siku ya kibarua cha kuendesha tofauti na Sh5,000 aliyopata kwenye biashara ya miwa. “Ndoto zangu ni kumiliki bodaboda yangu hapo baadaye.”

Daniel Hilmali, mwenye uzoefu wa miaka 16 alisema mbali ya kuhudumia familia na kusomesha, bodaboda imemwezesha kusoma udereva Veta mwaka 2018 kwa ada ya Sh480,000, Chuo cha usafirishaji NIT ada ya Sh390,000 na ufundi bomba Dodoma mwaka 2021 ili kujiimarisha zaidi kiuchumi.

Kwa upande wake Gesaman (26) aliyenunua bodaboda ya kwanza kwa kibarua cha kusaidia ufundi ujenzi mwaka 2017, kwa sasa anamiliki bodaboda mbili, Toyota IST inayotoa huduma za usafiri mtandaoni (Bolt) huku akiendelea kuweka akiba benki.

Hata hivyo, Eliya Lichungula anatofautiana na kauli za wenzake kwa kubainisha changamoto, akisema kukosekana kwa usalama wao kumefanya baadhi yao kutekwa na kupoteza maisha, kupoteza vyombo baada ya kuibiwa, jambo ambalo wakati mwingine huwaacha na majeraha ya kudumu na madeni.

“Hii ndiyo changamoto kubwa ikifuatiwa na ajali, ukipata moja kati ya hili unaichukia hii kazi. Kuhusu usalama wetu ikiwa hautazingatiwa na hatua kuchukuliwa tunaweza kupoteza vijana wengi.”

Peter Makata, ambaye ni dereva wa bodaboda alisema moja ya changamoto anayokutana nayo katika kazi yake ni kudharauliwa na madereva wa magari, huku wakihisi wote wanaofanya kazi hiyo ni wavuta bangi.

“Hili limekuwa likifanywa barabarani, tunatukanwa hovyo, unaweza ukasukumwa na gari kwa kitu kidogo. Pia, usalama wetu uko hatarini, hususan wakati wa usiku, unampakia mtu humjui ni nani ametoka wapi, utajua uko salama pindi unapomshusha na kulipwa hela yako,” alisema Peter.

Kauli ya Peter ya kudharauliwa na wenye magari inaungwa mkono na Simon Maney, akisema hiyo imekuwa ni kitu kinachowafanya wasijue kesho yao ikoje.

“Wakati mwingine unaweza kuwa uko sawa upande wako, lakini unasukumwa bila sababu, madereva wengi wameshajenga ile fikra kuwa bodaboda ni wasumbufu,” alisema Maney.


Wataka kuombwa radhi

Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa bodaboda nchini walionekana kukerwa na kauli ya Lema, wakitaka waombwe radhi.

Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Bodaboda Jiji la Dar es Salaam George Mbwile, alisema wiki hii shirikisho hilo kwa mikoa yote litatoa tamko kuhusu kauli hiyo ya Lema.

“Tuna ajira za bodaboda 360,000 wanaendesha maisha yao Jiji la Dar es Salaam, mimi nimejenga Bunju, kwa hiyo atuombe radhi.” Hali hiyo ilisababisha mwanasiasa hiyo ajibu hoja hizo kupitia ukurasa wake wa Twitter jana kwa kusema akiwaona watoto wa viongozi kama Waziri Mkuu na Rais wanafanya kazi hiyo ndipo ataomba radhi.

“Bodaboda ni kazi ya mateso, imeumiza watu na kujeruhi watu wengi. Acheni kudanganywa na Serikali iliyokosa mbinu za kuokoa maisha yenu. Umasikini sio sifa.”

Lema, aliyekuwa mbunge kati ya mwaka 2010 hadi 2020 mfululizo, kabla ya kumbilia Canada mwaka 2020 akidai kutishiwa maisha yake, ni mwenyekiti wa Chadema kanda ya kaskazini na mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho.

Hata hivyo, wadau wa usafiri huo walidai kuwa msingi wa hoja ya Lema ilikuwa ni namna gani Serikali inatakiwa kuweka misingi ya kuondoa umaskini kwa Watanzania wengi kwa kile alichosema kazi hiyo imekuwa ikiwasababishia madhara makubwa kiafya.


Mfumo wa ajira ukoje?

Kauli ya Lema inashabihiana na taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu ya Serikali ya mwaka 2016 iliyoonyesha kuwa asilimia 80 ya watu nchini walioajiriwa katika sekta isiyo rasmi wanafanya kazi katika mazingira yasiyo rafiki.

Akizungumza katika mkutano uliokuwa umeandaliwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO), Aprili 2016, aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Ajira kwa wakati huo, Joseph Nganga alisema Serikali ilifanikiwa kupunguza kiwango cha ukosefu wa ajira kutoka asilimia 11.7 ya mwaka 2006 hadi kufikia 10.3 ya mwaka 2014.

Nganga alisema kwa vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 35 kiwango cha ukosefu wa ajira kilishuka kutoka asilimia 13.7 ya mwaka 2006 hadi kufikia asilimia 11.7 ya mwaka 2014, licha ya waajiriwa katika sekta isiyo rasmi kufanya kazi zisizokuwa za staha.

Hata hivyo, akizungumza juzi na Mwananchi kwa simu, Kamishna wa Kazi Msaidizi, Andrew Mwalwisi alisema kundi hilo lina mchango mkubwa katika uchumi.

“Wanafanya kazi za kujiajiri na zimekuwa na manufaa ya kuwawezesha kupata kipato kusaidia maisha yao,” alisema Mwalwisi.

Akizungumzia suala la umaskini, Profesa Jehovaness Aikaeli ambaye ni Mchumi Mwandamizi kutoka Idara ya Uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema pamoja na changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi, bodaboda ni ajira inayosaidia kupunguza changamoto za umaskini.

“Umaskini ni hali ya kutokuwa na uwezo wa kujimudu mwenyewe kwa mahitaji yako ya msingi, sasa bodaboda imesaidia vijana kujimudu, kwa hiyo sio umaskini, jambo la msingi ni kuhakikisha wanafanya kazi hiyo kikanuni na taratibu kama ilivyo kwa magari, Rwanda ni mfano mzuri,” alisema Profesa Aikael.