Lema aibua mpya, atangaza kumshitaki Gambo

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa mikutano yake katika eneo la soko kuu jijini Arusha.

Muktasari:

  • Lema aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini tangu mwaka 2010 hadi 2020, alikimbilia nchini Canada na familia yake baada ya uchaguzi mkuu wa 2020 akidai kutishiwa usalama wake.

Arusha. Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amesema anakusudia kumshitaki Mbunge wa Arusha Mjini kwa madai ya kutumia fedha zilizochangwa na wafanyabiashara na zaidi ya Sh400 milioni za chama cha Bodaboda Mkoa wa Arusha.

Lema aliyerejea nchini Machi Mosi akitokea nchini Canada alikokimbilia na familia yake mwaka 2020, pia amesema tayari amepokea nyaraka za Gamboatakazotumia katika kesi hiyo. 

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mikutano yake katika eneo la soko kuu jijini Arusha leo Machi 7, 2023 amesema tangu ameondoka kuwa mbunge, Jiji la Arusha limetawaliwa na migogoro mingi na kukwamisha maendeleo.

"Tayari nimempa kesi hii wakili Peter Madeleka ambaye anakamilisha taratibu za kulifikisha mahakamani kesi hiyo," amesema.

Kauli ya Lema imekuja wakati kukiwa na malalamiko ya Chama cha Bodaboda jijini hapa, wakiomba Serikali kusaidia kupatikana kwa fedha zao kutoka kwa mbunge huyo.

Hata hivyo, Gambo amekuwa akikanusha kuchukuwa fedha hizo na kueleza watafutwe waliokuwa viongozi wa chama hicho, ambao baadhi wametoweka jijini Arusha.

Mbali na kesi hiyo, Lema amesema kuwa viongozi wengi wa CCM na Serikali Mkoa wa Arusha wamefurahi kurejea kwake, kutokana na ushindani uliopo kati yao na Mbunge huyo na viongozi hao wamekuwa wakimtumia ujumbe.

"Gambo pia amegombana na baadhi ya viongozi sasa huyu ni mbunge wa aina gani anagombana na kila kiongozi mwenzake," amesema.

Akizungumzia ubadhilifu wa fedha zaidi ya Sh25 million za ujenzi wa mitaro katika Kata ya Meya wa jiji la Arusha hivi karibuni, Gambo alisema anachokifanya ni kupambana na wizi na ubadhilifu wa Mali za umma kwani Jiji la Arusha limegeuzwa shamba la bibi.

"Wanasema Mimi nimekuwa nikiwaandalia ajali, hapana mimi natetea fedha za Serikali ambazo zinaliwa," alisema.

Katika hatua nyingine, Lema ameeleza chama hicho, kinamuombea Rais Samia Suluhu Hassan. Mungu ambariki aendelee kuipenda haki na kuondoa chuki za kisiasa katika jamii.

"Sisi hatuna ugomvi na Rais na tutakosoa Serikali yake ili wajirekebishe na sisi sio chawa wa Rais na akisikiliza ushauri wetu atafanikiwa," amesema.

Katika mkutano huo wa Lema, wanachama kadhaa wa CCM ambao awali walikuwa Chadema walitangaza kurejea kwenye chama hicho.

Katika mkutano huo wajumbe wa kamati kuu Chadema, John Heche, Peter Msigwa na Ezekiel Wenje waliwataka wakazi wa Arusha kuunga mkono harakati za kupatikana Katiba mpya.