Mwanamke ajitosa dereva bodaboda

Rosada Massawe (32) mkazi wa Rombo, Mkoani Kilimanjaro, ni miongoni mwa wanawake wachache wanaojivunia kufanya kazi ya bodaboda. Picha na Janeth Joseph

Muktasari:

  • Ni kwa nadra kuona mwanamke akifanya kazi ya bodaboda lakini imekuwa ni jambo la kawaida kwa Rosada Massawe (32) mkazi wa Rombo ambaye anafanya kazi ya bodaboda. Kupitia kazi hiyo ameweza kufanya mambo mengi ya maendeleo.

Rombo. Imani iliyojengeka miongoni mwa wanajamii ni kwamba kazi ngumu na hatarishi zimekuwa zikifanywa na jinsi ya kiume, miongoni mwa kazi hizo ni kama vile uongozaji wa mitambo ya mashambani na viwandani  pamoja na uendeshaji wa vyombo vya usafiri.

Hata hivyo hali hiyo imekuwa ni tofauti kwa sasa, baada ya wanawake kuamua kujitokeza kufanya shughuli zinazofanywa na wanaume zikiwemo zile za kuendesha magari ya mizigo na hata pikipiki maarufu kama bodaboda zinazotumika kusafirisha abiria kutoka sehemu moja kwenye sehemu nyingine.

Rosada Massawe (32), mkazi wa Rombo, Mkoani Kilimanjaro  ni miongoni mwa wanawake wanaojivunia kufanya kazi ya bodaboda ambayo ameahidi hataiacha mpaka hapo atakapozeeka.

Anasema kazi hiyo imekuwa ikimwingizia kipato na kuweza kuihudumia familia yake ya watoto wawili ambapo kwa siku anasema kazi hiyo inaweza kumwingizia kiasi cha Sh30,000 na kwamba hutegemeana na siku.

Akizungumza na Mwananchi Digital katika mahojiano maalum, amesema licha ya kwamba yeye ni mwanamke amekuwa akiifanya kazi hiyo bila woga licha ya kubezwa na jamii kwamba anafanya kazi za kiume.

Anasema ndoto zake za kumiliki bodaboda zilitokana na  kufanya kazi kwa bidii kwa watu na kwa malengo bila kuchagua ni kazi gani, ambapo amewashauri vijana kufanya kazi kwa malengo na kwamba kazi ni kazi.

"Jamii imekuwa ikinichukulia kama mwanaume, baadhi ya watu wananiambia kwanini nafanya kazi za kiume lakini nawaambia ni kwasababu inaniingizia kipato na siombi fedha kwa mtu, nakula kwa jasho langu, hainisumbui, ilimradi nafahamu nafanya kitu gani," amesimulia.

Pamoja na mambo mengine, anasema kazi hiyo kwasababu anayeifanya ni mwanamke, amekuwa akiaminiwa na watu wengi na kwamba anaweza kupewa mizigo wenye thamani kubwa, ama fedha taslimu na kuzifikisha panapohusika bila shida yoyote.

"Nimekuwa nikiaminiwa na watu wengi kwenye jamii inayonizunguka, mtu anaweza kunipa fedha nyingi akanambia nipeleke mahali fulani na nikafikisha vizuri mzigo wake. Najivunia hii kazi yangu na nitaifanya hadi uzeeni," amesema Rosada.

"Nawashauri vijana wenzangu wapambane wafanya kazi, kazi ni kazi wasichague kazi ya kufanya kipato wanachokipata wakiweke vizuri na wafanye kazi kwa malengo. Ukiwa na malengo unaweza kufanikiwa kutokana na malengo yako uliyojiwekea," amesema.

Anasema kupitia kazi yake hiyo, licha ya kusomesha watoto, ameweza kujenga pamoja na kupata fedha kwa ajili ya kuanzisha miradi mingine mbalimbali kama mradi wa kufuga pamoja na kilimo ambayo manufaa yake ni makubwa.

Anasema licha ya mafanikio makubwa aliyonayo, kwa sasa amekuwa akikumbana na changamoto mbalimbali.

"Kuna siku unaweza kutoka barabarani ukamchukua abiria mkakubaliana atakulipa kiasi fulani cha fedha mkifika sehemu husika anakugeuka na kukupa kile ambacho hamjakubaliana.  Kwa hiyo kama mwanamke huwezi kufanya chochote hata kutukana huwezi, unamwacha unaondoka," amesimulia.