Bunge laanza na kishindo, wabunge wacharuka
Muktasari:
Hoja hizo ni pamoja na idadi ndogo ya wabunge na uhalali wa matukio yaliyofanyika jana ikiwamo kuchaguliwa kwa wenyeviti na kuapishwa kwa wabunge wawili.
Dodoma. Hoja nzito zimeibuliwa, ikiwa ni siku ya kwanza tu ya Mkutano wa Kumi na Moja wa Bunge la Bajeti unaofanyika mjini hapa.
Hoja hizo ni pamoja na idadi ndogo ya wabunge na uhalali wa matukio yaliyofanyika jana ikiwamo kuchaguliwa kwa wenyeviti na kuapishwa kwa wabunge wawili.
Mengine yaliyoibuliwa na wabunge jana ni Wimbo wa Taifa unaotumika bungeni wakati wa ufunguzi wa mkutano na unapoahirishwa kuonekana na kasoro na mkaa kusafirishwa nje ya nchi ikielezwa kuwa unapelekwa kwa makundi ya kigaidi ya Al-Shabaab.
Walioibuka na hoja hizo ni Mbunge wa Ulanga, Godluck Mlinga, Sixtus Mapunda wa Mbinga na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Januari Makamba.
Kutotimia kwa akidi
Akiomba mwongozo wa Spika, Mlinga alisema kwa hesabu alizopiga, ameona kulikuwa na idadi ndogo ya wabunge.
“Kama hesabu yangu ni sawa, tuliyoyafanya haya ni halali ikiwamo viapo vya wabunge? Ni hatua gani itachukuliwa kwa wale wabunge ambao hawapo kwa wakati huu kwa sababu walitakiwa wawepo?”alihoji.
Alihoji pia iwapo kikao hicho si halali inakuwaje kuhusu posho zitakazotolewa kwa wabunge waliokuwapo ndani ya Bunge.
Akijibu mwongozo huo, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alisema kanuni namba 77 ndiyo inayotoa mwongozo wa kuhoji uhalali wa shughuli, kwa kutumia akidi ya wabunge.
Alisema mbunge anapaswa kusimama na kusema kuwa akidi haijatimia na baada ya kauli hiyo, kiti kitatoa agizo kuwa wabunge walio ndani ya ukumbi wahesabiwe.
“Si mbunge anayefanya kazi ya kuhesabu wabunge wako wangapi. Alipaswa kuniambia mimi akidi haijatimia kwa jambo ambalo lipo mbele yetu. Ukisoma kanuni hizi, akidi si hoja kwa kila jambo linalofanyika hapa ndani,” alisema.
Hata hivyo, alisema suala la akidi lingeibuliwa wakati wa kuanza kikao na iwapo amepata taarifa kutoka ofisi ya Bunge kuwa akidi haikuwa sawa wakati wanaanza kikao hicho cha jana, basi angeweza kumsikiliza kinyume cha hapo, mwongozo aliouomba haukuwa sawa kikanuni.
Naibu Spika alisema kutoonekana kwa wabunge kunaweza kusababishwa na wao kuwa katika vikao vya kamati au wana kazi maalumu waliyopewa.
Kuhusu posho, alisema wameshatoa ufafanuzi kuwa itatolewa kwa wabunge waliohudhuria na kufanya kazi na si walioingia na kuondoka ndani ya ukumbi baada ya kujiorodhesha.
Alisema shughuli zilizofanyika za kuapishwa kwa wabunge wa CCM, Maulid Mtulia (Kinondoni) na Dk Godwin Mollel (Siha) ni halali kwa mujibu wa kanuni.
Alipoulizwa sababu za wabunge wengi wa upinzani kutoonekana, Mbunge wa Serengeti (Chadema) Chacha Marwa alisema akiwa katika Viwanja vya Bunge kuwa hakuna makubaliano ya kambi ya upinzani ya kutokuwapo bungeni jana lakini kutokana na viongozi wa juu wa Chadema kushtakiwa, wamejikuta wakiacha kuingia ndani ya ukumbi.
“Chama chote kiko magerezani, wabunge wanajikuta tu wanaacha kuingia ndani lakini sio kwamba kuna kukatazwa au kususia hapana,” alisema.
Wimbo wa Taifa
Wakati Mlinga akiibua hoja ya kutotimia kwa akidi na suala la posho kwa wabunge ‘watoro’, Mapunda, aliibua hoja akiuliza iwapo ni sahihi kuimba Wimbo wa Taifa usio rasmi bungeni.
Alisema wimbo unaotumika bungeni hapo, una makosa mengi kuanzia kwenye ala, mdundo na maneno.
“Wimbo ambao tumekuwa tukiuimba ndani ya Bunge lako tukufu sio wimbo rasmi uliokubalika na Baluta (Baraza la Lugha Tanzania), miaka ile ya zamani kabla ya kubadilishwa na kuwa Basata.
“Naomba mwongozo wako hivi ni sawasawa sisi kuimba wimbo usio rasmi bungeni?” alihoji.
Hata hivyo, mbunge huyo wa Mbinga Mjini hakufafanua kwa undani makosa yaliyomo katika wimbo huo.
Akijibu mwongozo huo, Dk Tulia alisema atatoa mwongozo wa Mapunda mara baada ya kujiridhisha kama kweli kuna makosa hayo.
“Ili niweze kutoa mwongozo ulio kamili lazima nijiridhishe na haya maeneo ambayo ameyataja kama ni kweli yamekosewa au la? Nitatoa maelekezo hapa bungeni kama nitaona maeneo hayo yana makosa,” alisema.
Uchaguzi
Shughuli nyingine iliyofanyika katika kikao cha jana ilikuwa uchaguzi na kwa mara nyingine, wenyeviti wa Bunge waliomaliza muda wao walirejeshwa kushika nafasi hizo.
Waliochaguliwa ni Najima Giga (Viti Maalumu kutokea Zanzibar), Mussa Zungu (Ilala) na Andrew Chenge (Bariadi Magharibi).
Uchaguzi huo hufanyika mara mbili katika kipindi cha uhai wa Bunge cha miaka mitano na wanaowania ni wenyeviti au makamu wenyeviti wa kamati za Bunge.
Azimio la Mabadiliko ya Tabia nchi
Mbali na hilo, kazi nyingine iliyofanyika bungeni ilikuwa ni kuridhia Makubaliano ya Paris (Ufaransa) chini ya mkataba wa Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu mabadiliko ya tabia nchi na kushauri kubanwa kwa nchi zilizoendelea ili kutekeleza mkataba huo.
Akichangia mjadala wa makubalinao hayo, Mbunge wa Nsimbo (CCM), Richard Mbogo aliomba maazimio yatakayofanyika siku za usoni kuhusu mkataba huo, yawekewe vipengele vitakavyohakikisha utoaji wa fedha kwa nchi zinazoendelea kwa ajili ya kutunza mazingira.
“Hili litakuwa ni jambo muhimu sana katika kuzibana hizi nchi na hasa zinazoendelea ambazo zinapinga kutekeleza maazimio haya,” alisema Mbogo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba alisema makubaliano hayo yanakabiliwa na changamoto mbalimbali tangu yaanze kutekelezwa mwaka 1996 hadi 2002.
Alisema changamoto hizo ni pamoja na nchi zilizoendelea kuogopa kupoteza nguvu za kiuchumi kwa sababu utekelezaji wa mkataba huo kwa kuwa utaathiri uzalishaji viwandani kwa kupunguza matumizi ya nishati chafu.
“Changamoto nyingine ni ushindani wa kiuchumi baina ya nchi zinazoendelea na zile zenye uchumi unaokuwa haraka unaosababisha kuongezeka kwa viwanda vinavyochafua mazingira,” alisema.