Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wakala amuibulia Baba Levo madai ya rushwa Sh1 milioni

Muktasari:

  • Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Clayton Chipando, maarufu, Baba Levo anakabiliwa na kesi ya uchaguzi ambayo imeendelea kusikilizwa ushahidi wa upande wa walalamikaji wanaopinga ushindi wake.



Kigoma. Luma Akilimali, shahidi wa nne katika kesi ya uchaguzi inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini, (CCM), Clayton Chipando, maarufu Baba Levo, ameieleza Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma alimuona mbunge huyo akitoa rushwa ya Sh1 milioni.

Shahidi huyo ambaye pia ni mmoja wa walalamikaji katika kesi hiyo, ametoa madai hayo wakati akitoa ushahidi wake katika kesi hiyo leo Jumatano Julai 8, 2026, wakati akihojiwa na wakili wa walalamikaji John Seka.

Katika maelezo yake ya ufafanuzi wa majibu yake aliyoyatoa wakati akihojiwa na mawakili wa walalamikiwa, amedai Baba Levo alitoa rushwa hiyo kwa mtu mmoja aitwaye Mwantumu katika mkutano wa kampeni akamtaka amuombee kura.

Baba Levo alitangazwa mbunge katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025,  akimshinda mpinzani wake mkubwa kutoka ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.

Shahidi huyo, Luma na wenzake watatu, Pendo Kombolela, Lumu Mwitu na Johary Kabourou wamefungua kesi wakipinga ushindi wake.

Kesi hiyo ya uchaguzi namba 28949 ya mwaka 2025 mbali na yeye Baba Levo ambaye ni mlalamikiwa wa pili katika kesi hiyo walalamikiwa wengine ni Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kigoma Mjini na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Walalamikaji hao wanadai uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki kwa kuwa uligubikwa na kasoro nyingi za sheria na kanuni za uchaguzi.

Wanabainisha kasoro hizo ni pamoja na ukiukwaji wa taratibu, kanuni na Sheria za Uchaguzi, vitendo vya rushwa na udini vilivyooneshwa na mlalamikiwa wa pili, Baba Levo.

Hivyo wanaiomba mahakama hiyo pamoja na mambo mengine iamuru ufanyike upekuzi na uhesabuji upya wa karatasi za kupigia kura na kisha ibatilishe na kutengua uchaguzi huo.

Awali, akiongozwa na wakili wa walalamikaji, John Seka, shahidi huyo ameieleza mahakama atatoa ushahidi wake kwa njia ya maandishi, ambayo tayari yalishawasilishwa mahakamani na akaiomba mahakama iupokee.

Jaji Victoria Nongwa anayesikiliza kesi hiyo katika uamuzi wake amesema kuwa mahakama ikaupokea, kisha akaanza kuhojiwa maswali ya dodoso na mawakili wa walalamikiwa.

Akihojiwa na Wakili wa Serikali,  Erigh Rumisha, shahidi huyo ameeleza wakati wa uchaguzi huo alikuwa wakala wa ACT-Wazalendo lakini amekiri kuwa katika ushahidi wake wa maandishi hajasema kuwa alikuwa wakala katika kituo gani.

Amekiri kuwa japo katika maelezo yake ametoa tuhuma za rushwa lakini yeye binafsi hakuziona moja kwa moja bali kupitia mitandao ya kijamii.

Shahidi huyo amesema katika ushahidi wake kama mawakala walizuiwa kukagua kituo, lakini alipopewa sheria ya uchaguzi wa madiwani, wabunge na Rais na kutakiwa kusoma majukumu ya wakala, amekiri kuwa kukagua kituo si miongoni majukumu ya mawakala.

Akihojiwa na wakili wa Baba Levo, Thomas Msasa, shahidi huyo amekiri katika maelezo yake ya maandishi kuhusu vitendo vya rushwa aliviona wakati wakiangalia mtandaoni na wanachama wenzake wa Kata ya Kasingilima.

Hata hivyo, amekiri hakusema walikuwa wangapi, walikuwa wakiangalizia wapi, wala kwamba video hiyo ilirekodiwa wapi na nani na kwa kutumia kifaa gani na kwamba hana utaalamu wa kujua kuwa video nyingine mitandaoni huwa si za kweli.

Wakati akihojiwa na wakili Seka, shahidi huyo amefafanua madai hayo ya rushwa kuwa siku ya tukio Baba Levo alimuita jukwaani Mwantumu akamtambulisha kuwa ndiye aliyemfanya arudi Kigoma kugombea ubunge.

Shahidi huyo amefafanua Baba Levo alieleza Mwantumu alimlilia sana kuwa anatakiwa arudi Kigoma kugombea ubunge kwa kuwa watu wa Kigoma wananyanyasika.

Hivyo alimpatia Mwantum kiasi cha Sh500,000 na akaahidi kiasi kingine atammalizia kisha akamvalisha sare za CCM kisha akamtaka amuombee kura na Mwantumu akapiga magoti na kumuombea kura Baba Levo.


Endelea kufuatilia Mwananchi