CCM yawateua Makalla, Mongella, Jokate na Hapi

Ali Hapi (kushoto), Amos Makalla na John Mongela

Muktasari:

 Hamashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC) chini ye uenyekiti wa Rais Samia Suluhu Hassan imefanya uteuzi wa viongozi wake wanne ambao ni wajumbe wa sekretarieti akiwemo Amos Makalla kuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo.

Dar es Salaam. Ni wenyewe, ndivyo unavyoweza kusema kuakisi uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC) wa kuwateua John Mongella, Amos Makalla, Ally Hapi na Jokate Mwegelo kuziba nafasi nne zilizokuwa wazi za wajumbe wa sekretarieti.

Uteuzi wa makada hao wanne, ulidokezwa kwa nyakati tofauti na gazeti la Mwananchi tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipofanya mabadiliko ya wakuu wa mikoa ya Arusha na Mwanza Machi 31, 2024.

Katika mabadiliko hayo, Rais Samia alimteua aliyekuwa Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Paul Makonda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Pamoja na Makonda, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi, Gilbert Kalima aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mkinga na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana CCM (UVCCM), Fakii Lulandala aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro.

Baada ya mabadiliko hayo, kitendawili kilikuwa ni nani watarithi mikoba ya nafasi hizo nne za sekretarieti ya CCM zilizoachwa wazi na hatimaye kikao cha NEC cha jana kimetegua hilo.

Taarifa ya uteuzi iliyotolewa na Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo ya CCM leo Jumatano, Aprili 4, 2024, imeeleza Makalla ameteuliwa kuwa Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, akimrithi Paul Makonda.

Kulingana na taarifa hiyo, Mongella ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, akipokea mikoba kutoka kwa Anamringi Macha ambaye kwa sasa anautumikia Mkoa wa Shinyanga kwa nafasi ya Mkuu wa Mkoa.

Kwa upande wa Jokate, amepokea kijiti cha nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana CCM (UVCCM) kutoka kwa Fakii Lulandala aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mkinga.

Safu hiyo inakamilishwa na Hapi aliyechaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi CCM, akimridhi Gilbert Kalima aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro.

Uteuzi huo wa NEC iliyofanyikia Ikulu ya Dar es Salaamna kuongozwa na Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan imeacha nafasi moja ya mjumbe wa sekretarieti. Nafasi hiyo ni ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT).

Nafasi hiyo ilikuwa ikishikiliwa na Jokate ambaye sasa ni Katibu Mkuu wa UVCCM.

Imeandikwa na Juma Issihaka na Bakari Kiango