‘Chini ya miaka mitatu atumikie kifungo cha nje’

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Kaspar Mmuya, amependekeza wafungwa chini ya miaka mitatu watumikie kifungo cha nje.

Lengo la pendekezo hilo ni kupunguza msongamano wa wafungwa na mahabusu magerezani.

Pendekezo hilo alilitoa juzi kwenye Tume ya Kuangalia jinsi ya kuboresha mfumo wa Haki Jinai ambayo inakusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali.

Katika wasilisho lake Mmuya alipendekeza kuanzishwa kwa Sheria Jumuishi itakayoelekeza wafungwa chini ya huduma uangalizi kutokwenda jela.

Hoja hiyo pia inafanana na mapendekezo yaliyotolewa na wanasheria waliojitokeza jana mbele ya tume hiyo.

Mmuya ambaye aliongozana na watumishi wa Idara tatu ambazo ni idara ya Huduma za Uangalizi inayoshughulika na wafungwa wenye kifungo chini ya miaka mitatu, Bodi ya Taifa ya Parole inayoshughulika na wafungwa zaidi ya miaka minne na Tume ya Nidhamu ya wizara.

Chini ya Idara ya huduma ya uangalizi, baadhi ya wafungwa wamekuwa wakihukumiwa kwenda kutumikia adhabu zao katika magereza na wengine kwenda kutumikia vifungo vyao katika jamii.

Msingi wa shughuli hiyo iliyofikia siku ya 23 unaakisi uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwateua Januari 6, mwaka huu kwa lengo la kuimarisha mfumo huo katika taasisi tano za Serikali; Jeshi la Polisi, Mahakama, Ofisi ya DPP, Magereza, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (Takukuru) na Uhamiaji.

Mapendekezo mengine aliyowasilisha Mmuya ni pamoja na kupokonya mamlaka ya waziri mwenye dhamana ya kuhakiki ripoti ya mapendekezo ya wafungwa wanaokidhi vigezo vya kutumikia vifungo vyao nje na badala yake mamlaka hayo yabakie kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole anayefanya kazi hiyo.

Pili, alipendekeza kuanzishwa kwa programu maalumu ya uangalizi wa wafungwa wanaotoka magerezani kwa ajili ya kutumikia vifungo vyao nje chini ya mfumo huo wa Parole.

Tatu, alishauri kuanzishwa sekretarieti itakayosaidia kuratibu kazi za Idara ya Huduma za Uangalizi hadi ngazi za wilaya, kata na vijiji pamoja na kuongeza bajeti ya kutosha kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake.

Alishauri kuangalia upya namna ya kushughulikia kundi la wafungwa waliohukumiwa vifungo visivyopata huduma za idara hiyo ya uangalizi pamoja na bodi ya Parole.


Hoja ya THRDC

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa, akizungumza na Mwananchi kuhusu hoja ya vifungo vya nje alisema, “walioko wengi magerezani ni mahabusu, Tanzania zaidi ya asilimia 60 ni mahabusu.”

“Hoja yake haiwezi kusaidia sana lakini ni nzuri kwani sehemu kubwa ya kupunguza changamoto ni kufanya makosa kuwa na dhamana na ikiwa hivyo asilimia 90 watakuwa nje na yale makosa madogo yawe ya kifungo cha nje, sijui mzururaji, mlevi ama kaiba kuku, katukana mtu na kuondoa mfumo wa mtu kupelekwa mahakama ambayo haina nguvu, apelekwe mahakama husika,” alisema

Ngurumwa alisema ni vema kama mtu hatakamatwa pasi na upelelezi kukamilika na ikifanyika hivyo msongamano utapungua.

Hoja hiyo pia inaakisi mapendekezo ya Gervas Yeyeye, Mhadhiri kutoka Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania(OUT), aliyefika mbele ya tume hiyo jana akisema ili kukomesha mrundikano magerezani kwa njia ya kuweka ukomo wa upelelezi na muda wa kesi chini ya marekebisho ya Sheria ya mwenendo wa Makosa ya Jinai.

“Lakini pia Serikali irejeshe uhuru wa mtu yeyote kumshtaki mtu aliyekandamiza haki za wengine na kusababisha kwenda jela, uhuru huo uliondolewa kwenye marekebisho ya Sheria ya Utekelezaji wa Haki Muhimu na Wajibu Tanzania sura namba 3. Hapo tutapunguza mahabusu na wafungwa,” alisema.

Juzi, Augustino Nanyaro ambaye ni Kamishna Jenerali mstaafu wa Jeshi la Magereza, alishauri wajumbe hao wa tume maeneo tisa yaliyojikita kuimarisha mfumo wa kisheria kwa ajili ya uwezekano wa kupunguza kiwango kikubwa cha mahabusu na wafungwaji gerezani.


Mapendekezo mengine

Jana, ilikuwa zamu wa watalaamu wa sheria kutoka vyuo vikuu nchini, wakipendekeza mageuzi makubwa ya kikatiba, kisheria na uimara wa taasisi kwa lengo la kuheshimu na kuchochea utoaji wa haki mapema.

Wanasheria hao wameshauri kuweka mazingira ya kuzuia Serikali kuingilia uhuru wa Idara zinavyohusika na haki jinai ili kuimarisha mfumo wa haki kwa jamii Tanzania, wakisisitiza umuhimu wa mabadiliko ya Katiba katika kujenga msingi huo uliodhoofishwa hatua inayoibua uadui na migogoro ya viongozi na raia.

Dk Victoria Lihiru, mhadhiri kutoka Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) alipendekeza mbele ya wajumbe hao umri wa kuolewa utambuliwe kisheria kuanzia miaka 18, ukeketaji uhesabike kuwa kosa la jinai kwa wanawake wote na sio chini ya miaka 18 pekee.

Dk Victoria alipendekeza marekebisho ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, sura ya 20 ili kumuwajibisha mume au mke atakayemlazimisha mwenzake kufanya tendo la ndoa. “Mara nyingi tunagusia wanawake tu ndio wanabakwa, sheria iangalie hata waume” alisema

Siku mbili zilizopita, Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) kilipendekeza kitendo cha mume kumbaka mke wake kitambuliwe kama kosa la jina katika sheria hiyo.

Aidha, Dk Victoria alipendekeza kuanzisha mbadala wa hukumu ya kifo kwa lengo la kulinda haki ya utu na kumfanya mkosaji kujutia.