Dakika 90 za mvua maandamano ya Chadema
Muktasari:
Tayari maandamano yamewasili katika viwanja vya Reli kusubiri taratibu za mkutano wa hadhara.
Arusha. Mvua kubwa iliyonyesha kwa dakika takribani 90 ndani ya Jiji la Arusha, haijazuia wafuasi na wanachama wa Chama cha demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuandamana.
Mvua iliyoanza kunyesha saa 6.50 mchana na kukatika saa 8.20 mchana haikusitisha maandamano hayo ya amani yaliyofanyika leo Februari 27.
Maandamano hayo yalifanyika kwa makundi, moja likipita barabara ya Arusha-Moshi walioanzia eneo la Tengeru, yakiongozwa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema. Pia alikuwapo kiongozi mkuu wa jumuiya ya sauti ya Watanzania, Dk Wilbroad Slaa.
Kundi lingine lilikutanisha wana-Chadema kutoka Kwa Mrombo, Sombetini, Sokon One, Majengo na Kisongo, wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho bara, Tundu Lissu na mjumbe wa Kamati Kuu, John Heche.
Tayari maandamano hayo yamewasili katika viwanja vya Reli kusubiri taratibu za mkutano wa hadhara.
Baadhi ya washiriki wa maandamano hayo wamesema mvua ni baraka, ikiwa ni ishara kuwa Mungu amepokea maombi yao.
"Kilio chetu kikubwa ni ugumu wa maisha wakati Serikali ikizidi kunyamaza juu ya mambo yanayoendelea ikiwemo bei kubwa ya bidhaa, ajira chache na hata mafuta ya petroli kupanda bei kila mwezi," amesema Mariam Said, mmoja wa waandamanaji.
Yanafanyika leo jijini hapa ikiwa ni hitimisho la maandamano ya amani ya chama hicho yaliyoanza Januari 24, jijini Dar es Salaam.
Lengo la maandamano hayo yaliyofanyika pia Mwanza na Mbeya yenye jina la 'Vuguvugu la haki ya Watanzania', ni kuishinikiza Serikali kushughulikia tatizo la kupanda kwa gharama za maisha.
Pia yanalenga kuitaka Serikali kusikiliza maoni ya wananchi kwenye miswada ya sheria za uchaguzi iliyopelekwa bungeni Novemba 10, 2023, kujadiliwa na kisha kupitishwa na sasa inasubiri kusainiwa na Rais kuwa sheria.