Maandamano Chadema katikati ya mvua Arusha

Muktasari:

  • Ni maandamano ya nne kufanywa na chama hicho, baada ya yale ya Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya.

Arusha. Licha ya mvua kunyesha jijini Arusha, maandamamo ya amani ya Chadema yanaendelea, yakiwahusisha viongozi wa ngazi ya juu wa chama hicho.

Hata hivyo, baadhi ya waandamanaji waliondoka na kwenda kujificha kwenye vibanda na baraza.

Yanafanyika leo Februari 27, 2024 jijini Arusha ikiwa ni hitimisho la maandamano ya amani ya chama hicho yaliyoanza Januari 24, jijini Dar es Salaam.

Lengo la maandamano hayo yaliyofanyika pia Mwanza na Mbeya yenye jina la 'Vuguvugu la haki ya Watanzania, ' ni kuishinikiza Serikali kushughulikia tatizo la kupanda kwa gharama za maisha.

Pia yanalenga kuitaka Serikali kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu miswada ya sheria za uchaguzi iliyopelekwa bungeni Novemba 10, 2023, kujadiliwa na kisha kupitishwa na sasa inasubiri kusainiwa na Rais kuwa sheria.

Maandamano hayo yanaongozwa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, Makamu wake (Bara), Tundu Lissu, na Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema.

Maandamano hayo yaliyoanzia maeneo tofauti jijini hapa yalipofika eneo la Mianzini kuelekea stendi kuu ya mabasi, mvua kubwa ilianza kunyesha.

Licha ya watu wachache kukimbia kwenda kujificha, wengi wameendelea kuandamana pamoja na askari wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha wanaosimamia usalama katika maandamano hayo.

Baadhi ya washiriki wa maandamano hayo wamesema mvua ni baraka, ikiwa ni ishara kuwa Mungu amepokea maombi yao.

"Kilio chetu kikubwa ni ugumu wa maisha wakati Serikali ikizidi kunyamaza juu ya mambo yanayoendelea ikiwemo bei kubwa ya bidhaa, ajira chache na hata mafuta ya petroli kupanda bei kila mwezi," amesema Mariam Said, ambaye ni mmoja wa waandamanaji.