Maandamano ya Chadema Mwanza yasogezwa hadi Februari 15

Muktasari:

  • Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Benson Kigaila (Bara) amesema sababu ya kubadilishwa maandamano hayo kutoka Februari 13 hadi 15 ni danadana za kupata kibali cha kufanya mkutano wa hadhara katika uwanja wa furahisha.

Mwanza. Maandamano ya amani yaliyoitishwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kupangwa kufanyika jijini Mwanza Februari 13, 2024 sasa yamesogezwa mbele hadi Februari 15, 2024.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza leo Februari 8, 2024, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Benson Kigaila (Bara) amesema mabadiliko ya tarehe yametokana na uwanja wa Furahisha wanakopanga kuhitimishia maandamano hayo kwa kufanya mkutano wa hadhara, kudaiwa kuwa na shughuli nyingine Februari 13 na 14, 2024.

“Tayari tumetoa taarifa ya maandamano kwa Jeshi la Polisi kupitia kwa OCD (Mkuu wa Polisi Wilaya) Ilemela na nakala kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza kama sheria inavyoelekeza kuwa taarifa itolewe Polisi saa 48 kabla ya siku ya maandamano,” amesema Kigaila.

Naibu Katibu Mkuu huyo amesema waandamanaji wanatarajiwa kutumia njia tatu tofauti katika wilaya za Ilemela na Nyamagana kabla ya kukutana eneo la Ghandi Hall, na kuhitimisha kwa mkutano wa hadhara katika uwanja wa Furahisha.

Ametaja njia hizo kuwa ni Ilemela-kanisani katika Barabara ya Makongoro, Pasiansi, Nyamanoro, kona ya bwiru, darajani mpaka kwenye bustani ya Ghandi Hall, huku njia ya pili ikianzia Buhongwa kupitia Kenyatta, Mkolani, Nyegezi, Butimba, Mkuyuni, Igogo, Nyamagana, Isamilo hadi Ghandi Hall ambapo watakutana na waandamanaji wengine kuelekea kwenye mkutano wa hadhara uwanja wa Furahisha.

“Njia ya tatu itaanzia Igoma center na itapita Barabara ya Nyerere, Mandu, mabatini, Natta, Nyerere plaza mpaka Ghandi Hall, maandamano ya sasa yataishia kwa wananchi… tunaenda kukutana na wananchi wa Mwanza ili tuzungumze nao kwa maana haya malalamiko ya Katiba na hali ngumu yanawahusu,” amesema.

Ajenda za maandamano

Kigaila amesema katika maandamano hayo kutakuwa na ajenda mbili ambazo ni kuitaka Serikali isikilize maoni ya wananchi kuhusu miswada mitatu ya sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, sheria ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani pamoja na ya vyama vya siasa na ajenda ya pili ni ugumu wa maisha.

“Tunaitaka Serikali ije na mkakati wa dharura na makusudi kwa ajili ya kupunguza gharama za maisha, kwa hiyo maandamano haya ya Februari 15 yanaandaliwa na Chadema lakini si ya Chadema peke yake, tunawaalika Watanzania wote wanaokerwa na maisha magumu,” amesema.

Ameongeza: “Rais ana uwezo wa kuacha kusaini sheria ambayo imepitishwa bungeni, akisaini maana yake atakuwa amekataa maoni ya Watanzania.”