Maandamano ya Chadema yaibua gumzo bungeni

Muktasari:

  • Chadema ilifanya maandamano ya amani Januari 24, 2024 jijini Dar es Salaam yaliyoongozwa na mwenyekiti wake, Freeman Mbowe wakishinikiza kuondolewa bungeni kwa miswada ya sheria za uchaguzi.

Dodoma. Wakati Bunge likiendelea na majadiliano ya miswada mitatu ya sheria za uchaguzi, baadhi ya wabunge wamejielekeza kwenye maandamano ya Chadema yaliyofanyika Januari 24, 2024 yaliyokuwa yakishinikiza miswada hiyo iondolewe bungeni.

Wabunge wamedai chama hicho cha upinzani kinashindwa kutambua jitihada zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kujenga mazingira mazuri ya kisiasa hapa nchini.

Mbunge wa Tarime Vijijini (CCM), Mwita Waitara wakati akichangia maoni yake kwenye miswada hiyo leo Februari mosi, 2024, amesema maandamano hayo yamechagizwa na upole wa Rais Samia Suluhu Hassan na yanaashiria ukomavu wa demokrasia nchini.

 “Wamempata Rais mpole amewaita amekaa nao, halafu wao wanakwenda kuandamana wakati kati ya mambo waliyopendekeza zaidi ya asilimia 60 yametekelezwa kwenye miswada hii iliyoletwa,” ameeleza Waitara ambaye miaka kadhaa iliyopita alikuwa mbunge kwa tiketi ya Chadema.

Mbunge huyo ameshauri kwenye sheria mpya zitakazotungwa na Bunge, ni vizuri ielezwe kwenye viti maalumu wabunge wanapatikanaje, ili kuepukana na changamoto za baadhi ya wabunge kufukuzwa na vyama vyao baada ya kuteuliwa.

“Kuna wabunge wenzetu 19 hapa, walifukuzwa sababu ya madhara ya kutokuwa na sheria inayoeleweka, uchaguzi ukiisha watu wanaamua tu kwamba huyo awe na huyu asiwe mbunge, lakini hakuna mahali utaratibu upatikanaji wao ndani ya vyama unaelezwa na sheria,” amesema.

Kwa upande wake, mbunge wa Geita Mjini (CCM), Constantine Kanyasu ameeleza hoja nyingi za Chadema na wadau wengine walizotoa kwenye kikosi kazi zimetekelezwa, isipokuwa hoja ambazo zinahitaji mabadiliko ya katiba kwa kuwa mchakato wake pengine ungechukua muda mrefu.

“Huwezi kuendeleza nchi kama hali ya kisiasa haieleweki, walitarajia kila wanachokitaka wao kitekelezwe, lakini Rais anafanya mambo ya Watanzania wote na si ya wachache,” amesema Kanyasu.

“Kikosi kazi kiliunda hoja na kilikuja na hoja 83 ambapo kati ya hizo hoja 64 zimefanyiwa kazi, huku hoja 12 bado zikiendelea kufanyiwa kazi kutokana na baadhi ya hoja hizo kugusa Katiba ambao ni mchakato mrefu,” amesema Kanyasu.

Kanyasu ameeleza kuwa malalmiko ya marekebisho ya Katiba na sheria za uchaguzi yameletwa mara nyingi bungeni, lakini hayakuwahi kutekelezwa mpaka sasa ambapo utekelezaji wake unakwenda hatua kwa hatua.

Naye mbunge wa Lupembe (CCM), Edwin Swale wakati akichangia maoni yake kwenye miswada hiyo, ameeleza kuwa maandamano ya Chadema ambayo yaliambatana na ulinzi wa Jeshi la Polisi pamoja na uwepo wa huduma za dharura, umeonyesha ni kwa jinsi gani maridhiano yamepiga hatua kubwa nchini.

Swale amesema kinyume na ambavyo wengi walitarajia, amani na usalama ulitawala zaidi kwenye maandamano hayo huku akieleza kuwa hoja nyingi zilizotakiwa na Chadema zimefanyiwa kazi na Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala Katiba na Sheria ambapo Bunge linaendelea kujadili hoja hizo.

Swale amekosoa hatua ya kuwepo kwa maandamano hayo ambayo amedai hayakuwa na umuhimu, kwani maoni ya chama  yalikuwa bado hayajafanyiwa kazi na Bunge lakini tayari chama hicho kilishakimbilia maandamano.

Miswada inayojadiliwa bungeni ni pamoja na Muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2023, Muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi wa Mwaka 2023 pamoja na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa wa Mwaka 2023 (The Political Parties Affairs Laws (Amendment) Bill, 2023.