Wanawake watinga maandamano ya Chadema wakivaa viroba

Baadhi ya wanawake wameibuka kwenye maandamano ya amani ya Chama cha Demokrasia ya Maendeleo(Chadema) wakiwa wamevaa viroba (magunia) vyenye ujumbe tofauti.

Muktasari:

Wanachama na wafuasi wa Chadema wanafanya maandamano ya amani leo Januari 24, 2024 lengo likiwa ni kupinga miswada ya sheria za uchaguzi zilizowasilishwa bungeni

Dar es Salaam. Baadhi ya wanawake wameibuka kwenye maandamano ya amani ya Chama cha Demokrasia ya Maendeleo(Chadema) wakiwa wamevaa viroba (magunia) vyenye ujumbe tofauti.

Wanawake hao wamejitokeza Kituo cha Mbezi Luis, Dar es Salaam leo Januari 24, 2024 ambako maandamano hayo yataanzia.

Wanawake hao wanaofanya biashara ya kuokota chupa, wamesema wamebuni vazi hilo wakilenga kufikisha ujumbe kwa Rais Samia Suluhu Hassan na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson.

“Tumevaa hivi kwa kuwa kitu ambacho ni rahisi kukipata kwa sasa ni kiroba, maisha yamekuwa juu na familia nyingi zinateseka tukiwamo sisi,” amesema mmoja wa wanawake hao.

Wamesema wao sio wanachama wala wafuasi wa Chadema, lakini wanashiriki maandamano hayo kama wananchi wa kawaida kutokana na kuvutiwa na ajenda za Chadema kwenye maandamano hayo.

Chadema imeweka bayana sababu za kufanya maandamano hayo kuwa ni kupinga miswada ya sheria za uchaguzi iliyowasilishwa bungeni, hali ngumu ya maisha wanayopitia Watanzania na kuishinikiza Serikali kusikiliza maoni ya wananchi.

Miswada hiyo ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa yote ya mwaka 2023.

Pia, Chadema wanataka Serikali itengeneze mpango wa dharura wa kukabiliana kwa kupanda gharama za maisha kwa Watanzania na mfumuko wa bei.

Maandamano hayo ya amani yanayoanzia Stendi ya Daladala ya Mbezi Luis yanaelekea ofisi za Umoja wa Mataifa  (UN)hapa nchini.