Chadema yatangaza ngwe ya pili maandamano

Muktasari:

  • Chadema imetangaza awamu ya pili ya maandamano yatakayofanyika katika majiji ya Mwanza, Arusha na Mbeya.

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetangaza ratiba ya awamu ya pili ya maandamano yatakayoanzia mkoani Mwanza Februari 13, 2024 kisha kuelekea katika majiji ya Arusha na Mbeya.

 Tayari Chadema wameshafanya awamu ya kwanza ya maandamano yaliyofanyika Januari 24, 2024 jijini Dar es Salaam yakilenga kushinikiza Serikali kuondoa bungeni miswada mitatu ya sheria za uchaguzi inayotarajiwa kupitishwa kesho.  Miswada hiyo inaendelea kujadiliwa na wabunge.

Pia wanaitaka Serikali kupeleka mpango wa dharura wa kukwamua hali ya ugumu wa maisha wanaopitia Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari mosi, 2024 jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika ametaja tarehe za maandamano hayo kwa jiji la Mbeya kuwa Februari 20, 2024 na Jiji la Arusha Februari 27, 2024 akisema maandalizi kuelekea maandamamano hayo yanaendelea.

Amesema msukumo wa maandamano hayo nchi nzima unaendelea kwa kuwa baada ya kufanya Dar es Salaam, hakuna kiongozi wa Serikali aliyetoka kutoa kauli yeyote.

"Kutokutoka kwa umma kwa kiongozi yeyote mwandamizi serikalini kuzungumza chochote tunachukulia ni muendelezo wa kupuuza maoni ya wananchi, ndiyo maana tumekuja kutangaza tena na safari hii tunakwenda kwenye majiji matatu hadi Serikali itakaposikiliza," amesema.

Mnyika ameutaka umma kutambua kuwa maandamano hayo ni msimamo wa chama hicho binafsi kutaka utawala wa kisheria na demokrasia ya kweli kutamalaki nchini.

Amesema baada ya kufanya maandamano hayo katika majiji hayo na mikoa mingine na ikaonekana Serikali inaendelea kukaa kimya, watatoka na msimamo mwingine wa kuwaeleza wananchi cha kufanya katika kudai haki.

"Maandamano tuliyofanya Dar es Salaam Serikali ilionyesha kupuuza na matokeo yake tumeona ikisoma tena awamu ya pili miswada mitatu bungeni bila kujali maoni ya wananchi," amesema.

Amesema wanajua miswada hiyo hijazingatia maoni na hawakubaliani nayo inapitishwa kesho na Bunge, lakini msimamo wao wataendelea na maandamo kushinikiza Rais asisaini kuwa sheria.

Amesema jambo moja ambalo Serikali imeonyesha kukifanyia kazi ni lile la kutoa bei elekezi ya sukari nchini, huku akieleza hata hivyo kumekuwa na sarakasi nyingi ndani yake.

"Serikali isijifiche kwenye kivuli cha sukari pekee kwamba inachangia ugumu wa maisha, kuna minyororo mingi inayochagiza kuongeza ugumu wa maisha ndiyo maana tunataka Serikali ipeleke bungeni mpango wa makusudi kukwamua ugumu wa maisha," amesema.