‘Dege’ la mizigo kutua nchini, kupokelewa na Rais Samia

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuhusu ujio wa ndege mpya ya mizigo, inayotarajiwa kuwasili June 3 2023. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Tangu Julai 2021, Serikali iliingia mikataba mbalimbali ya ununuzi wa ndege nne ikiwemo ndege ya mizigo aina ya Boeing 737 - 300F ambayo itakuwa ndege pekee ya mizigo kati ya ndege 12 zilizonunuliwa na Serikali.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuipokea ndege ya kwanza ya mizigo aina ya Boeing 737 - 300F itakayowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Jumamosi Juni 3, 2023.

Ndege hiyo ina uwezo wa kubeba mzigo wa tani 54 na inatumia mafuta kidogo ukilinganisha na ndege za aina hiyo. Inatarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi hapa Tanzania.

Akizungumzia ujio wa ndege hiyo leo Juni Mosi, 2023, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema ujio wa ndege hiyo utarahisisha usafirishaji wa bidhaa mbalimbali kwenda nje ya nchi kama vile mbogamboga, matunda, nyama na samaki.

Pia, amesema ndege hiyo itasaidia kusafirisha vifaa mbalimbali vinavyonunuliwa na Serikali kama vile dawa. Amesema ndege hiyo itakuwa ikikodishwa pia kwa wafanyabiashara wakubwa.

"Ujio wa ndege hii utawezesha mizigo hiyo kusafirishwa kwa gharama nafuu kwenda kwenye masoko. Huko nyuma wafanyabiasha walikuwa wakilazimika kusafirisha mizigo kwa gharama kupitia ndege za mizigo zinazopatikana katika nchi jirani," amesema Profesa Mbarawa.

Waziri huyo amebainisha kwamba jumla ya tani 24,941 za maua, mbogamboga, nyama na samaki zinazalishwa hapa nchini kwa mwaka, lakini Tanzania ilikuwa na uwezo wa kusafirisha tani 420 pekee, hivyo kiasi kinachobaki kilikuwa kikisafirishwa kupitia nchi jirani.

Kuhusu mapokezi ya ndege hiyo, Profesa Mbarawa amesema mapokezi hayo yatafanyika katika uwanja wa JNIA na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Samia.

"Shughuli na mapokezi ya ndege hii itafanyika uwanjani na itapokelewa na Rais Samia. Watanzania watapata fursa ya kufuatilia ujio wa ndege yao, kwa hiyo nawaalika pia waandishi wa habari muweze kuwafikishia habari hizi wananchi wengine," amesema Waziri huyo.

Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano wa Shirika la Ndege nchini (ATCL), Sarah Reuben amesema baada ya kuwasili nchini, ndege hiyo itaanza kutoa huduma Julai 2023 baada ya kukamilisha taratibu za usajili na kupata vibali vingine.

"Tunatarajia kwamba baada ya kutua nchini, ndege itaanza kutoa huduma Julai baada ya kukamilisha usajili na vibali vingine muhimu," amesema Reuben.