Rais Samia atoa ndege kusafirisha mwili wa Mkono

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Kamati ndogo ya Mazishi, Stephen Wasira amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa usafiri wa ndege kwa ajili ya kusafirisha mwili wa Nimrod Mkono kesho kuelekea Mwanza kwa ajili ya maziko.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Kamati ndogo ya Mazishi, Stephen Wasira amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa usafiri wa ndege kwa ajili ya kusafirisha mwili wa Nimrod Mkono kesho kutoka jijini Dar es Salaam hadi Mwanza.

Kada huyo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) aliyetumikia Serikali kwa muda mrefu amesema Rais Samia amechukua hatua hiyo kutokana na mchango wa marehemu Mkono serikalini enzi za uhai wake.

Wasira amesema mbali na heshima hiyo ya Rais Samia, kesho Waziri Mkuu Kassim Majaliwa atamuwakilisha Rais Samia katika kuongoza tukio la kitaifa la kuaga mwili wake ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.

“Baada ya kuaga mwili wake kitaifa kesho, safari itaelekea hadi Mwanza kwa ndege hiyo,” amesema Wasira leo Mei 27, 2023 wakati wa ibaada ya kuaga mwili wake nyumbani Masaki jijini Dar es Salaam.

“Siku hiyo hiyo tutaelekelea Butiama ambako maziko yatafanyika Mei 29, 2023 baada ya wapiga kura wake kutoa heshima za mwisho.

Watu mbalimbali waliopata msaada wake wa kielimu na kimaisha wamejitokeza nyumbani hapo kushiriki ibaada hiyo huku wakimuelezea namna alivyogusa maisha yao kwa namna tofauti.

Mkono aliyekuwa mbunge wa Musoma Vijijini (2005 - 2015) na baadaye Butiama (2015 - 2020) mkoani Mara kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) alifariki Dunia Aprili 18, 2023 nchini Marekani alikokuwa akitibiwa tangu mwaka 2018.

Mwili wake umewasili leo alfajiri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam (JNIA) kabla ya kuanza ratiba za ibada nyumbani kwake Masaki.