Diwani awatangazia hatari wanafunzi watoro

Diwani wa Kunduchi Michael Urio akisaidiana na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mtakuja  kubeba sehemu ya viti na meza  500 za wanafunzi wakati wa hafla ya  kukabidhi  vifaa hivyo iliyofanyika Kunduchi jana Alhamisi Machi 28 2024  jijini Dar es Salaam.Picha Said khamis

Muktasari:

Diwani wa Kata ya Kunduchi Michael Urio amesema amepata taarifa baadhi ya wanafunzi ni watoro hawafiki shuleni

Dar es Salaam. Baada ya kuwapo madai ya wanafunzi kutoroka shule na kwenda kufanya shughuli za uvuvi, Diwani wa Kata ya Kunduchi Michael Urio ametangaza msako mkali kuwabaini na kuwachukulia hatua.

Urio amesema msako huo utawagusa pia, wanafunzi wanaoshinda kwenye gereji na vibanda vya michezo ya kubahatisha katika muda wa masomo.

Akizungumza wakati akikabidhi madawati na viti katika Shule ya Sekondari ya Mtakuja iliyopo Wilaya ya Kinondoni jana Alhamisi Machi 28, 2024, Urio amesema anazo taarifa kuna wanafunzi watoro na wanatumia muda mwingi kufanya vitu visivyofaa.

Amesema wanafunzi wengi badala ya kwenda shule  wanaishia kwenye vibanda wakicheza michezo ya kubahatisha na wengine wanashinda baharini wakifanya vibarua vya kupaa samaki.

"Wale wote wenye tabia ya kutoroka tutawakamata, tutawachukulia hatua ikiwamo mzazi na mtoto watawajibika kufika kwenye ofisi ya diwani na mtendaji wa kata kuja kutoa maelezo kwa barua kwa nini hawafiki shuleni," amesema Urio.

“Nimepata taarifa kuna wanafunzi wengine wanakuja na simu shuleni wanatumiana vitu vya ajabu ikiwamo picha za ngono na kuangalia tamaduni za nje zisizofaa.”

 Urio amesema ametoa madawati 250 na viti 250 katika Sekondari ya Mtakuja pamoja na madawati 300 na viti 300 kwa Shule ya Sekondari ya Kondo ili wanafunzi waondokane na changamoto ya kukaa kwa kubanana.

Mkuu wa Sekondari ya Mtakuja, Projestus Barongo amesema shule hiyo ina wanafunzi 876 na walikuwa wana uhaba wa madawati, hivyo meza na viti walivyopewa na diwani huyo vitaondoa changamoto za watoto hao kukaa kwa kubanana.

"Wanafunzi wangu watakaa wawili wawili kwa kila dawati moja, itawasaidia wanapokuwa darasani watamsikiliza mwalimu vizuri na kukaa kwa uhuru," amesema Barongo.

Mwanafunzi wa kidato cha kwanza wa shule hiyo, Faraji Ramadhani amesema walikuwa wanakaa chini, hivyo meza na viti hivyo vitawasaidia kukaa kwa uhuru wakati wanapofundishwa na walimu wao.

"Wanafunzi tupo wengi wengine tulikuwa tunakaa chini wengine kwenye madawati, hivi viti na meza vitatusaidia kukaa kwa uhuru na kumsikiliza vizuri mwalimu anapofundisha," amesema mwanafunzi huyo.