Dk Biteko awasili Mbeya kukagua miradi ya maendeleo

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Songwe tayari kwa kuanza ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani Mbeya. Akiwa mkoani humo, mbali ya kazi ya kukagua miradi mbali mbali ya maendeleo, atakagua pia miradi ya Jotoardhi ya Kiejo-Mbaka na Ziwa Ngozi. Picha na ONWM.

Muktasari:

Tangu kuteuliwa nafasi ya Naibu Waziri Mkuu, Agosti 30, 2023, Dk Doto Biteko hii ndio ziara yake ya kwanza mkoani Mbeya.




Mbeya. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ametua mkoani hapa  kwa ajili ya ziara ya kikazi itakayodumu kwa siku mbili.

Biteko ambaye amewasili leo Jumatatu Februari 19, 2024, akiwa mkoani hapa atatembelea na kukagua kukagua miradi ya maendeleo.


Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi huyo kufanya ziara mkoani humo tangu alipoteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa wa Naibu Waziri Mkuu wa Tanzania, Agosti 30 mwaka jana.


Katika ziara hiyo, Waziri huyo ataanzia wilayani Rungwe ambapo atakagua mradi wa Joto Ardhi (Geothermal) kisha atazindua mradi wa umeme vijijini (REA) katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali na atakagua pia mirani mingine ya umeme.

Baada ya kuwasili katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe, Naibu Waziri Mkuu Biteko amepokelewa na mwenyeji wake ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera na viongozi mbalimbali wakiwamo wa dini.




Akizungumza katika kikao chake na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Homera, Dk Biteko ameeleza jitihada zinazofanywa na Serikali katika nyanja mbalimbali ikiwemo ya Elimu, Siasa na Nishati.

Hata hivyo, amesema anatambua kuwa Sekta ya Nishati ya umeme inakumbana na changamoto katika kipindi hiki.

Hivyo, amesema upungufu wa nishati hiyo uliopo hivi sasa ni kati ya megawati 300 hadi 190, lakini kwa sasa kuna matumaini makubwa kwa sababu mradi wa Julius Nyerere ( JNHPP) unatarajiwa kuingiza megawati 235 katika gridi ya Taifa mwezi huu.

Amesema matumaini mengine ni kutoka mradi wa umeme wa Rusumo ambao utaingiza megawati 27 katika gridi ya Taifa.


Amesema kiasi hicho cha umeme kitakapoingia kwenye gridi ya Taifa kitaondoa hali ya sasa ya upungufu yanayochangiwa na mahitaji makubwa ya umeme kuliko kiwango cha uzalishaji.

Dk Biteko amesema kiwango hicho pia kitaiwezesha Serikali kuendelea kufanya maboresho kwenye miundombinu ya umeme.

Amesema kwa Mkoa wa Mbeya ambao mahitaji yake ni kati ya megawati 70 na 74, kwa sasa wanapata umeme wa megawati 51 huku akisema jitihada zinazoendelea sasa zitasaidia  mkoa huo kupata umeme kulingana na mahitaji.

Katika hatua nyingine, Dk Biteko ameupongeza Mkoa wa Mbeya kwa kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato, utekelezaji wa miradi ya maendeleo sambamba na usimamizi mzuri wa sekta Elimu, watoto wanaostahili kwenda shule wameripoti kwa zaidi ya asilimia 70.


Lakini amesisitiza viongozi kufuata agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuwa, tofauti ya itikadi ya vyama vya siasa  isifanye wananchi kuwa maadui bali watu wabishane kwa hoja huku kipaumbele kikiwa ni maendeleo ya nchi.

Awali, akimkaribisha Dk Biteko, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amemueleza kuwa shughuli za kiuchumi mkoani humo zinaendelea vizuri na kwa mwaka 2023/2024 wamefanikiwa kukusanya mapato ya Sh49 bilioni ikiwa ni zaidi ya asilimia 105.

Homera amesema utekelezaji wa miradi ya umeme nao unaendelea vizuri ikiwemo ya upelekaji umeme vijijini, vitongojini na migodini.

Katika elimu mkuu huyo wa mkoa amesema Mbeya imekuwa na ufaulu mzuri huku watoto wanaopaswa kwenda shule, wakiripoti kwa zaidi ya asilimia 70.