Hatimaye mwili wa mwanafunzi Moshi wazikwa

New Content Item (1)

Mwili wa mwanafunzi wa darasa la kwanza, Jonathan Makanyaga (6) ukiwa umebebwa kuelekea nyumbani.

Muktasari:

  • Hata hivyo, taarifa za chanzo cha kifo chake bado hazijawekwa wazi.  

Moshi. Mwili wa mwanafunzi wa darasa la kwanza, Jonathan Makanyaga (6), ambaye kifo chake kilizua utata umezikwa, Polisi ikiitaka familia kuendelea kuwa na moyo wa subira.

Kutokana na utata wa kifo cha mtoto huyo, uchunguzi wa mwili ulifanywa na timu mbili za madaktari. Ilidaiwa alipigwa na mwalimu tarajali.

Maziko yamefanyika leo Machi 18, 2024 na kuhudhuriwa na mamia ya waombolezaji, vilio vikisikika wakati wa kuaga na mwili kuingizwa kaburini, mama yake Janeth Shayo akisema: "Jamani mwanangu bye, nishikie nafasi nitakufuata tu muda si mrefu."

Mwanafunzi huyo wa Shule ya Msingi Mrupanga, wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro alifariki dunia Machi 10, 2024 katika Hospitali ya KCMC.

Baada ya polisi kumaliza uchunguzi waliruhusu ndugu kuendelea na taratibu za maziko ambayo yalikuwa yafanyike Jumamosi Machi 16, 2024 lakini hayakufanyika licha ya maandalizi, ikiwamo kuchimba kaburi kukamilika.

Padri Albert Lashayo wa Parokia ya Mawela, aliyeongoza misa na maziko ya mtoto huyo, ameitaka jamii kuishi maisha ya ukamilifu ili mwisho iweze  kufika mbinguni.

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Moshi, Azizi Kalokola aliyehudhuria maziko hayo ameitaka familia kuendelea kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu.

Amesema kazi ya Jeshi la Polisi ni kuhakikisha haki inatendeka.

"Tuwaombe ndugu, wazazi na familia, kuwa na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu, kifo hakizoeleki lakini kila mtu ndiyo njia yetu. Naomba muwe wavumilivu, tumeshirikiana na familia tangu kifo kimetokea mpaka leo, tulikuwa nao bega kwa bega. Jukumu letu Jeshi la Polisi ni kuhakikisha haki inatendeka," amesema Kalokola.

Wasifu wa marehemu uliosomwa unaeleza Jonathan alizaliwa Aprili 7, 2017.

Ilivyokuwa awali

Machi 16, akizungumzia sababu za kutozikwa mwili wa mwanafunzi huyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alisema ni kutokana na shaka iliyoibuliwa na familia ya mwanafunzi huyo kuhusu kifo chake baada ya taarifa kurushwa mitandaoni zikionyesha mama yake akilalamika.

"Hatukuhitaji kuingia kwenye malumbano tumelazimika kuagiza mtaalamu (pathologist) kutoka Dar es Salaam aje afanye uchunguzi kwa pamoja walinganishe hicho kinachobishaniwa ili kuondoa mkanganyiko, tunafanya hivyo kujiridhisha ili kuondoa mashaka pande zote mbili," alisema.

"Ni kweli tulishaukabidhi mwili lakini ulikuwa haujaondolewa KCMC kwani waliandika maelezo yote, lakini kulipoibuka malalamiko mitandaoni ndipo tukaingilia kati kuiomba familia ili kuondoa shaka wavumilie tumlete huyo mtaalamu," alisema.

Mpaka sasa taarifa za chanzo cha kifo cha mwanafunzi huyo haijawekwa wazi ila Jeshi la Polisi lilieleza uchukuaji wa vipimo vya mwili wa mtoto huyo,  vilishirikisha wataalamu wa sekta mbalimbali na kwamba linawashikilia walimu tarajali watano.

Taarifa iliyotolewa na Kamanda Maigwa Machi 15, 2024, ilieleza ilidaiwa  mwanafunzi huyo aliadhibiwa na walimu hao Februari 28, 2024 kisha kupelekwa Hospitali ya KCMC bila ya kutolewa taarifa polisi na alifariki Machi 10, akipatiwa matibabu.