Polisi washikilia walimu 5 kifo cha mwanafunzi

Moshi. Jeshi la Polisi linawashikilia na kuwahoji walimu watano tarajali wa mafunzo ya ualimu (BTP) wanaofundisha katika Shule ya Msingi Mrupanga mkoani Kilimanjaro, kwa madai ya kuhusika na kifo cha mwanafunzi wa darasa la kwanza, Jonathan Makanyaga (6).

Mwanafunzi huyo, mkazi wa Kijiji cha Kimanganuni chini, Kata ya Uru Kusini wilayani Moshi, alifariki dunia Machi 10, mwaka huu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini, KCMC alikolazwa kwa matibabu, kwa kile kinachodaiwa alichapwa viboko na mmoja wa walimu hao baada ya kuchelewa shuleni.

Inadaiwa Februari 28, mwanafunzi huyo akiwa na wenzake wawili walichapwa na mwalimu huyo (jina halijatajwa) baada ya kuchelewa shuleni hapo na Jonathan alichapwa sehemu mbalimbali mwilini, kisha kuangushwa chini.

Inaelezwa wenzake wawili alikuwa nao wakati wanachapwa walijikinga na fimbo hizo kwa kutumia mabegi waliyokuwa wamebeba mgongoni na Jonathan alishindwa kujizuia na kuumizwa sehemu ya uti wa mgongo, mbavuni na sehemu ya mapajani na kisha kuangushwa chini.

Akizungumza na Mwananchi jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alisema mama na bibi wa Jonathan walikwenda shuleni kuhoji kwa nini mtoto wao amerudi nyumbani akiwa na hali hiyo na ndipo walimu waliwapoza na wakashirikiana nao kumpeleka hospitali bila kutoa taarifa polisi.

“Mtoto aliendelea na matibabu mpaka Machi 10 alipofariki. Tulichofanya, lilifunguliwa jalada la kifo cha mashaka kwa sababu hakuna taarifa iliyotolewa awali, ila tunawashikilia walimu wa mafunzo ya vitendo watano kwa mahojiano na kesho (leo) kutafanyika postmortem (uchunguzi wa kifo) ili kujua chanzo cha kifo chake,” alisema.
 

Mama afunguka

Janeth Shayo, mama wa mtoto huyo alieleza Februari 28 mwanaye alirudi nyumbani akiwa hana furaha na mdogo wa Jonathan alimweleza kuwa kaka yake anavuja damu mdomoni.

Alisema alipomwangalia alibaini ni kweli, mwanaye anavuja damu mdomoni na puani, na alipomuuliza alimweleza amechapwa viboko na mmoja wa walimu hao kwa sababu ya kuchelewa kushika namba saa moja kamili asubuhi.

“Jioni nilipakua chakula, nikamwambia baada ya kula apumzike kidogo kisha aende kulala, wakati nadeki mdogo wake akaniita akanambia Jonathan anatoka damu puani, nikimwangalia damu zinatoka bado nikamuuliza wapi panauma, akanambia kichwa kinamuuma, nilimpa dawa za maumivu (paracetamol) wakalala na mdogo wake,” alisema.

Alisema asubuhi ya siku iliyofuata aligundua mtoto huyo alikuwa na damu nyingi mdomoni, wakati anamuandaa ampeleke hospitali alibaini ana majeraha mgongoni.

“Nikamuuliza tena umejigonga wapi? Akasema hajajigonga, mgongo ulikuwa umevimba na eneo la chini ya uti wa mgongo kuna uvimbe umevilia damu na ni kweusi, pajani nako kuna alama ya fimbo na kumevilia damu, kwenye mguu nako kumevimba," alisema.

Alisema hali hiyo ilimfanya aende shule kujua sababu za mtoto wake kuadhibiwa kiasi hicho.

“Nilikutana na mwalimu mkuu msadizi ambaye baada ya kuona hali ya mtoto, akanipa Sh20,000 nikamtibu na itakavyokuwa niwaambie. Nilikwenda zahanati nikapewa dawa, daktari akanambia akizidiwa nimrudishe achomwe sindano, nilienda naye nyumbani lakini bado hali yake ilikuwa si nzuri,” alisema na kuongeza;

“Sikuweza kulala ilibidi nimrudshe zahanati, alipomwona na kumwangalia kwenye macho akanambia nimpeleke hospitali ya St Joseph.
"Nilipofika mapokezi walimwangalia mtoto hali yake ilivyo, nikaambiwa nikafungue faili, walivyomuona mtoto kadri siku zilivyokuwa zikienda, wakanishauri nimpeleke KCMC kwa vipimo vikubwa zaidi na Machi 8 tukawa tumeenda,"

Hata hivyo, alisema baadaye daktari aliyekuwa akimhudumia alimweleza kuwa mtoto ana changamoto ya seli sahani na kuna damu imevujia tumboni, hivyo atawekewa mirija.

“Kabla hilo halijafanyika mwanangu akawa amefariki tarehe 10," alisimulia mama huyo.

Alipotafutwa mwalimu mkuu wa shule, Florah Kahabi alisema hawezi kuzungumzia tukio hilo kwa kuwa lipo kwenye vyombo husika na kwamba yupo msemaji wa tukio hilo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Shedrack Mhagama alisema baadaye ya kupita taarifa ya mwanafunzi kufariki shuleni hapo walifuatilia kujua ukweli wake na kwamba taarifa walizonazo ni kuwa mwanafunzi huyo alikuwa anaumwa saratani ya damu.

“Nilipata hizi taarifa, nilifuatilia kule shuleni, mtoto alikuwa anaumwa saratani kwa muda mrefu na ndio maana amefariki," alisema mkurugenzi huyo.

Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya KCMC, Gabriel Chisseo alisema, “Baada ya kufanyiwa uchunguzi na madaktari wetu, waligundua alikuwa na upungufu mkubwa wa damu na baadaye vipimo vilionyesha alikuwa na saratani ya damu, kwa mfano chembe sahani pekee tu zikikutwa 11 kwa hiyo uwezekano wa kupata matatizo ni mkubwa zaidi".