‘House girl’ anavyopigana kwenda shule

Muktasari:

Haikuwa kazi rahisi kufanya vizuri darasani akiwa kwenye lindi la umaskini, lakini jitihada na hamasa kutoka kwa walimu wake zilimfanya Mariam Mchiwa kupata daraja la kwanza katika matokeo yake ya mtihani wa kidato cha nne kwa mwaka 2021.

Dar es Salaam. Haikuwa kazi rahisi kufanya vizuri darasani akiwa kwenye lindi la umaskini, lakini jitihada na hamasa kutoka kwa walimu wake zilimfanya Mariam Mchiwa kupata daraja la kwanza katika matokeo yake ya mtihani wa kidato cha nne kwa mwaka 2021.

Pamoja na ufaulu huo na kuchaguliwa kujiunga kidato cha tano katika Sekondari ya wasichana Songea, binti huyu kutoka mkoani Dodoma hana uhakika wa kwenda shule kutokana na familia yake kutokuwa na uwezo wa kumudu mahitaji na gharama za nauli kumfikisha shuleni huko.

Mariam ni mtoto wa tano katika familia ya watoto sita, pekee akiwa amepata elimu ya sekondari na kufika kidato cha nne akipata ufaulu wa daraja la kwanza na pointi 16.

Hali ya umaskini ilimsukuma Mariam kusafiri hadi jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya kazi za nyumbani na wiki moja baada ya kuwasili ndipo alipopata taarifa za kuchaguliwa kwake kujiunga na kidato cha tano.

“Baada ya matokeo kutoka nikaona niondoke kule kijijini kwetu Songambele, nilienda Dodoma mjini kwa ajili ya kutafuta kazi ambayo ingenisaidia kupata chochote kitu maana hali ya familia yangu si nzuri, hivyo nikaona nianze kujiandalia fedha ya ada nikienda shule.

“Mambo hayakuwa mazuri Dodoma mjini maana nilipata kazi ya mama ntilie ambayo nilikuwa nalipwa Sh2000 kwa siku, kazi yenyewe nilikuwa nafanya kuanzia alfajiri hadi saa tano usiku, ilifika wakati nikachoka nikaamua kuachana nayo na kurudi nyumbani,” alisema Mariam.

Kurudi kwake nyumbani kulimfanya azidi kupoteza matumaini ya kuendelea kupata elimu hivyo akajitosa kufanya shughuli za vibarua vidogo vidogo na kusaidiana na mama yake kutunza familia.

MwanzoniMei alikwenda mtu nyumbani kwao aliyekuwa anahitaji msichana kwa ajili ya kwenda kufanya kazi jijini Dar es Salaam, wazazi wake wakaridhia akafanye kazi hizo ili aweze kupata fedha wakiamini shuleni atatakiwa kwenda Septemba.

“Wazazi walijua shule zitapangwa mwezi wa tisa baada ya sensa, wakaridhia nije kufanya kazi mjini nitafute fedha ambayo itaniwezesha kwenda shule maana wao walishasema wazi kwamba hawana uwezo hivyo kama kuna njia inaweza kunisaidia nipate elimu wako radhi niitumie.

Nilipofika Dar, hazikupita siku nyingi Serikali ikatangaza shule kwa waliopangiwa kidato cha tano. Nakumbuka siku hiyo nilikuwa nazungumza na bosi wangu alikuwa ananiuliza kuhusu elimu nikamwambia nimemaliza kidato cha nne na kupata daraja la kwanza, alishangaa kwanini nipo hapo na ufaulu huo,”

Katika mazungumzo hayo Mariam ndipo alibaini kuwa siku hiyo lilitoka tangazo la kupangiwa shule na alipofuatilia alikuta amepangiwa shule ya wasichana Songea.

“Natamani nisome niwe nesi, nipunguze umaskini kwenye familia. Kwetu mimi ndiye nimesoma hadi kufikia kidato cha nne wengine hawakumaliza shule ya msingi au hata kugusa shule kabisa naomba Watanzania wanisaidie nipate mahitaji na ada ili niweze kujiunga na wenzangu, tunatakiwa kuripoti shuleni mwezi ujao hadi sasa sina chochote maana kazi nimefanya wiki mbili na hata nikilipwa haiwezi kutosha,”.

Mama anayeishi na binti huyo, Agnes Kosam anasema alizungumza naye ndipo alipobaini kuwa amefaulu na amechaguliwa kujiunga kidato cha tano.
“Ni kweli nilikuwa na shida ya msichana wa kazi lakini aliponielezea kuhusu hali yake, nafsi yangu ikaniambia siwezi kuendelea kumuacha afanye kazi wakati ana nafasi ya kuendelea kusoma.
Akizungumza na Mwananchi, Mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Songambele Mussa Ngauyapai, alisema wanafahamu changamoto anazopitia binti huyo na wamekuwa wakimtia moyo kila mara ili aweke nguvu kwenye masomo yake.