Hukumu ya kunyongwa ilivyobadili maisha ya Rose aliyekutana na mumewe aliyefungwa kimakosa

Moshi. Mkazi wa Moshi, Rose Yona Malle (25) aliyehukumiwa kunyongwa hadi kufa na baadaye kukata rufaa kupinga hukumu hiyo na kushinda amesimulia alivyojikuta akituhumiwa kwa mauaji na alivyopata mwenza aliyekuwa amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kimakosa.

Akizungumza na Mwananchi, Rose alisema mwaka 2012 alikamatwa akihusishwa na mauaji ya dereva bodaboda mjini Moshi baada ya kukodi usafiri huo wakati akienda katika majukumu yake ya kujitafutia riziki.

Alisema baada ya kushuka kwenye usafiri huo aliendelea na majukumu yake lakini siku iliyofuata alifuatwa nyumbani akielezwa kuwa dereva huyo wa bodaboda ameuawa na kwamba anahusishwa na mauaji hayo.

“Nilichukua bodaboda akanifikisha sehemu husika yeye akaondoka na mimi nikaendelea na shughuli zangu. Kesho yake walikuja maofisa wa polisi nyumbani kwetu wakanieleza kuna tukio la mauaji nahusika nalo.”

Alisema alifunguliwa kesi ya mauaji katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi na upelelezi ulipokamilika mwaka 2015 alifikishwa katika Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi kujibu mashtaka mbele ya Jaji Benedict Mwingwa.

“Nilifunguliwa kesi ya mauaji nikiwa na baadhi ya watu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi. Mwaka 2016 hukumu ilitolewa na nilihukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kukutwa na hatia ya mauaji. Tulirudishwa katika Gereza la Karanga na baadaye Gereza la Isanga Dodoma,” alisema.

Alibainisha kuwa hakukubaliana na hukumu iliyotolewa katika Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi hivyo aliamua kukata rufaa katika Mahakama ya Rufani Arusha ambayo Desemba 2017 ilithibitisha kuwa alihukumiwa kimakosa na kuachiwa huru.

“Namshukuru Mungu ilikuwa Desemba 16, 2017 mahakama ilithibitisha kuwa nilihukumiwa kimakosa na sikukutwa na hatia yoyote niliachiwa huru baada ya kukaa gerezani miaka sita.

“Miaka sita si mchezo, kwa maisha ya gerezani ni miaka mingi mno kutokana na changamoto zilizokuwepo huko. Imani ilikuwepo maana niliamini Mungu atanisaidia. Wakati naingia gerezani nilikuwa na miaka 18. Ndoto zangu zilipotea kabisa baada ya kuingia gerezani.

“Yapo mengi niliyokutana nayo siwezi kuyasema kwenye vyombo vya habari. Kimsingi ninamuomba Rais John Magufuli, Rais wa wanyonge ambaye ni msikivu anipe nafasi ya kuzungumza naye nina mengi ya kumueleza naamini atanisikia na kunielewa.”

Alivyokutana na mwenza wake

Akisimulia alivyopendana na Mohammed, Rose anaeleza kuwa walikutana wote wakiwa wafungwa kwa namna ya ajabu.

Alisema wakati wanafahamiana alikuwa ni mahabusu na walianza kuwa marafiki na walikuwa wakifarijiana kutokana na kupitia kipindi kigumu.

“Mohammed alikua ni sehemu ya faraja kwangu kipindi niko gerezani. Alikuwa akipita na gari akiwa na askari wa Magereza alikua akinisalimia na kunipa pole, alikuwa akiniambia pole mdogo wangu kuwa na amani ipo siku Mungu atakusaidia utatoka, basi tukaendelea kutiana moyo hivyohivyo.

“Kipindi mimi nafungwa yeye pia alikuwa mfungwa alikuwa hajatoka. Baadaye mimi nilipelekwa Isanga. Alipoachiwa (mwaka 2017) alikuwa akija mara kwa mara na alikuwa akifuatilia kesi yangu, mpaka nilipopelekwa Gereza la Arusha mwaka huo 2017, kwa kweli nilikuwa nikimwona nafarijika sana.

“Hata siku mahakama iliponiachia huru yeye alikuwa mtu wa kwanza kufika hata kabla ya ndugu zangu. Jambo la muhimu alilonieleza alinambia mshukuru Mungu na kuanzia sasa utulize akili kwani mambo ni mengi.

“Taratibu nyingine ziliendelea kwani tayari tulikuwa tumeshapendana, tukiwa gerezani hivyo alituma wazazi wake nyumbani kwetu, tukavishana pete ya uchumba na sasa tumeoana na tuna mtoto wa miezi sita.”