Huyu ndiye Dk Chrisant Mzindakaya

Huyu ndiye Dk Chrisant Mzindakaya

Muktasari:

  • Ni safari ya utendaji uliotukuka katika awamu ya kwanza, pili, tatu

Katika Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa chama kimoja cha siasa uliofanyika Septemba 30, 1965 Chrisant Mzindakaya aligombea ubunge kwa mara ya kwanza katika Jimbo la Ufipa Kusini na kushinda kwa kura 6,186 dhidi ya kura 6,075 za mpinzani wake, Eranus Nyangu ikiwa ni tofauti ya kura 111.

Katika Uchaguzi Mkuu uliofuata Oktoba 26, 1975 Mzindakaya aling’ara baada ya kushinda kwa tofauti ya takriban nusu ya kura zote katika jimbo la Sumbawanga Vijijini. Alipata kura 40,341 dhidi ya Mfupe Pangani aliyepata kura 22,735.

Mbio zake ziliingia doa mwaka 1981 baada ya ushindi wake kutenguliwa mahakamani kwa hoja kwamba alikiuka taratibu za uchaguzi. Uchaguzi uliporudiwa, aligombea lakini akashindwa katika kura za maoni na mpinzani wake, Gilbert Louis Ngua mwaka 1982.

Hata hivyo, Novemba 10, 1982 alirejea bungeni baada ya kuteuliwa na Rais Julius Nyerere kuwa mkuu wa Mkoa wa Mbeya kuchukua nafasi ya Kingunge Ngombale Mwiru ambaye aliongoza mkoa huo tangu 1977. Kingunge aliteuliwa kuwa mkuu wa Idara ya Itikadi na mafunzo ya siasa wa CCM.

Wakati huo wakuu wa mikoa walikuwa wanaingia bungeni moja kwa moja.

Mzindakaya hakukaa sana katika mkoa huo, Februari 12, 1983 alihamishiwa Morogoro kuendelea na wadhifa huo.

Aprili 12, 1984 wakati kifo cha aliyekuwa waziri mkuu, Edward Sokoine kinatokea, Mzindakaya ndiye alikuwa mkuu wa mkoa huo.

Mwaka 1986 alihamishiwa Kigoma kuchukua nafasi ya Profesa John Machunda hadi 1993.

Tuzo alizopata

Mwaka 1984 alipata Tuzo ya Mwalimu Nyerere kwa kufanikisha kwa vitendo utekelezaji wa Sera ya viwanda vidogovidogo nchini.

Miaka minane baadaye, 1992, alitunukiwa na Umoja wa Vijana Nishani ya Mlima Kilimanjaro kwa kutambua mchango wake katika kufanikisha maendeleo ya kilimo na viwanda nchini.

Mwaka mmoja baadaye, 1993, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi alimwandikia barua ya kumpongeza kwa kuwa mkuu wa mkoa aliyeonyesha utendaji bora wa kazi akiwa mkoani Kigoma na Rukwa.

Mwaka 2005, kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2005, Rais Benjamin Mkapa alimwandikia barua ya kutambua mchango wake katika mapambano dhidi ya rushwa kwa njia ya vitendo.

Mwaka 2010 aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta alimpa Dk Mzindakaya Hati Maalumu ya Kutukuka katika kulitumikia Bunge kwa muda wa miaka 45.

Katika historia ya Bunge, Mzindakaya hawezi kusahaulika, baada ya kujijengea umaarufu kama mzee wa mabomu, alipokuwa akifichua ufisadi mbalimbali ndani ya Serikali.

Dk Mzindakaya atakumbukwa zaidi alipomlipua aliyekuwa Waziri wa Fedha, Profesa Simon Mbilinyi kuhusu msamaha wa kodi kwa kampuni nne zilizoingiza tani 5,500 za mafuta ya kupikia yenye thamani ya Sh300 milioni.

Kamati ya Bunge iliyoteuliwa kuchunguza hilo, chini ya uenyekiti wa Iddi Simba, Septemba 24 mwaka huo iliwasilisha ripoti ikipendekeza Rais amchukulie hatua Mbilinyi, ambaye baadaye alitangaza kujiuzulu wadhifa huo.

Vilevile, Mzindakaya atakumbukwa zaidi alipomlipua aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Iddi Simba, kutokana na kashfa ya sukari iliyosababisha waziri huyo kujiuzulu pia.

Katika sakata la sukari Iddi Simba alitoa vibali kwa makampuni ya kuagiza sukari nje, lengo likiwa kukidhi mahitaji makubwa ya sukari na uamuzi huo ukaonekana kuwaumiza zaidi wananchi.

Agosti 10, 2001 Mzindakaya, akiwa Mbunge wa Kwela, akatoa hoja binafsi bungeni dhidi ya Simba. Alitoa taarifa kuhusu kile alichokiona ni kashfa, kisha akashinikiza Waziri Simba ajiuzulu na aliombe radhi Bunge kwa kulidanganya.

Pamoja na kwamba Simba awali aligoma kujiuzulu, shinikizo lilikuwa kubwa kiasi kwamba alijiuzulu.

‘Mabomu’ mengine ambayo yalimjengea umaarufu zaidi Mzindakaya ni pale alipomlipua aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Shamsa Mwangunga Januari 30, 2009 akidai kuwa alikiuka Azimio la Bunge. Mangunga alijishusha na kuliomba radhi Bunge.

Mbunge huyo alimfikisha waziri katika hali hiyo baada ya kueleza jinsi alivyokaidi azimio la Bunge na akapendekeza pamoja na kuomba radhi, akemewa na Bunge.

Hata hivyo, baada ya kuwalipua wenzake kwa muda mrefu, katika siku za mwisho naye alianza kugeukiwa akidaiwa kukopeshwafedha kwa ajili ya kujengea kiwanda cha kusindika nyama mkoani Rukwa na kudhaminiwa na Serikali, na fedha hizo hakuwa amerudisha.

Ijumaa ya Julai 16, 2010, Mzindakaya aliliaga Bunge baada ya kulitumikia kwa muda mrefu. Alisema haondoki bungeni kwa sababu ya uzee bali, “nataka kuondoka kwa upendo na amani, sitaki kuwa mbunge kwa kutumia pesa.”

Alito wosia kwa bunge linalofuata (2010-2015) liwe la uchumi badala ya kuendelea kuelekeza nguvu zaidi katika siasa kwa sababu sifa ya siasa nchi inayo tangu enzi za Mwalimu Nyerere.

“Ni aibu sisi kusaidiwa na nchi kama Uholanzi iliyobadilisha bahari kuwa eneo la kilimo. Tumieni sheria ya ubia kati ya Serikali na makampuni binafsi kupunguza mwanya kati ya matajiri na maskini,” alisema.

Julai 19, 2011, Rais Jakaya Kikwete alimteua Mzindakaya kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC), wadhifa aliodumu nao hadi Julai 20, 2016 baada ya Rais John Magufuli kumteua Dk Samuel Nyantahe kutumikia wadhifa huo.

Alhamisi ya Aprili 13, 2017 kulizuka taarifa kwenye mitandao ya kijamii zikieleza kuwa Dk Mzindakaya amefariki dunia akiwa kwenye matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Hata hivyo ilibainika kuwa habari hizo hazikuwa na ukweli wowote.

Hata hivyo, miaka minne baadaye, Jumatatu ya Juni 7, 2021, saa 9.15 alasiri, Dk Mzindakaya alifariki dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam alikokuwa amelazwa. Hayo ndiyo maisha ya kazi na siasa ya Dk. Chrisant Majiyatanga Mzindakaya.