Jela miaka 60 kwa kumbaka, kumpa mimba mwanafunzi wa darasa la sita
Muktasari:
- Mahakama ya Wilaya ya Serengeti imemhukumu kifungo cha miaka 60 jela Adamu Matera (22) mkazi wa kijiji cha Remung'orori kwa kosa la kumbaka na kumpa mimba mwanafunzi wa darasa la sita.
Serengeti. Mahakama ya Wilaya ya Serengeti imemhukumu kifungo cha miaka 60 jela Adamu Matera (22) mkazi wa kijiji cha Remung'orori kwa kosa la kumbaka na kumpa mimba mwanafunzi wa darasa la sita.
Katika hukumu iliyosomwa Julai 29 na Hakimu mkazi wa wilaya, Judith Semkiwa mshitakiwa ametiwa hatiani kwa makosa mawili la kubaka na kumpa mimba mwanafunzi huyo kinyume cha sheria.
Kataika kosa la kwanza la ubakaji, Matera amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na kosa la pili la kumpa mwanafunzi mimba nalo akihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.
Hata hivyo adhabu zote zinakwenda pamoja hivyo mshitakiwa huyo atatumikia kifungo cha miaka 30 gerezani.
Mwendesha Mashitaka wa Jamhuri, Faru Mayengela akiieleza mahakama katika kesi ya Jinai namba 264/2020 mbele ya Hakimu Semkiwa amesema mshitakiwa alitenda kosa hilo kati ya Machi na Mei 2020.
Amesem mshitakiwa mwenye wake wawili alianza mahusiano ya kimapenzi na mtoto mwanafunzi huyo kisha akampa mimba na kufikishwa mahakamani hapo kwa makosa mawili la kubaka na kumpa mimba mwanafunzi.