Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ndejembi azindua njia mpya ya umeme Newala

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 33 kutoka Masasi hadi Newala.

Muktasari:

  • Mradi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuendelea kuwekeza katika miradi ya kimkakati ya nishati ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma ya umeme.

Newala. Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amezindua rasmi mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 33 kutoka Masasi hadi Newala, akisema utaboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuchochea shughuli za kiuchumi katika Wilaya ya Newala.

Akizungumza leo Jumanne, Julai 21, 2026, wakati wa uzinduzi huo, Waziri Ndejembi amesema mradi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuendelea kuwekeza katika miradi ya kimkakati ya nishati ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma ya umeme.

Amesema njia hiyo ya umeme itaongeza uzalishaji, kuvutia uwekezaji na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi katika Wilaya ya Newala.

"Njia hii ya umeme ni msingi wa kukuza uchumi, kuongeza uzalishaji, kuvutia uwekezaji na kuboresha upatikanaji wa umeme kwa Wilaya ya Newala," amesema.

Waziri huyo pia amesema Serikali itaendelea kuimarisha upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Lindi na Mtwara, ikiwamo kuiunganisha kikamilifu na Gridi ya Taifa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya uhakika.

Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mkuu wa Wilaya ya Newala, Mwangi Kundya, amesema Serikali imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani humo, ikiwemo sekta ya nishati.

Amesema vijiji vyote 785 vya Mkoa wa Mtwara sasa vinapata huduma ya umeme, hatua aliyoeleza kuwa ni mafanikio makubwa ya Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi.

Kundya amesema pia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limepokea vitendea kazi mbalimbali kwa ajili ya kuboresha huduma kwa wateja, ikiwamo magari 11, bajaji nne na pikipiki tisa.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba, amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika uzalishaji na miundombinu ya umeme mikoa ya Lindi na Mtwara ili kukidhi mahitaji yanayoendelea kuongezeka.

"Mahitaji ya umeme katika Lindi na Mtwara yanaendelea kuongezeka na Serikali imewekeza katika uzalishaji. Kwa sasa Mkoa wa Mtwara unazalisha zaidi ya megawati 50," amesema.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Lazaro Twange, alisema mradi wa njia ya umeme ya kilomita 76 kutoka Masasi hadi Newala umegharimu Sh4.56 bilioni.

Amesema kabla ya mradi huo kukamilika, Wilaya ya Newala ilikuwa ikipata umeme kutoka Mtwara kupitia Nanyumbu kwa umbali wa kilomita 170, hali iliyosababisha kukatika kwa umeme mara kwa mara.

Twange amesema kukamilika kwa mradi huo kumeimarisha upatikanaji wa umeme na kupunguza changamoto ya kukatika kwa huduma katika wilaya hiyo.

Ameongeza kuwa Serikali kupitia Tanesco imetenga takribani Sh5.27 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kubadilishia umeme, kitakachoongeza uwezo wa mfumo wa usambazaji na kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye ya wananchi pamoja na wawekezaji wa Wilaya ya Newala.

Kwa upande wake, mbunge wa Newala Vijijini, Dk Yahaya Nawanda, kwa niaba ya wabunge wa Mkoa wa Mtwara, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika miradi ya umeme, akisema hatua hiyo itachochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika mkoa huo.