JNIA ya pili Afrika Mashariki kusafirisha abiria

New Content Item (1)
JNIA ya pili Afrika Mashariki kusafirisha abiria

Muktasari:

  • Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere, umeshika nafasi ya pili kati ya viwanja vilivyopo ndani ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kwa kusafirisha abiria wengi mwaka 2019.

Dar es Salaam. Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere, umeshika nafasi ya pili kati ya viwanja vilivyopo ndani ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kwa kusafirisha abiria wengi mwaka 2019.

Taarifa iliyochapishwa katika tovuti ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) inaonyesha kuwa abiria milioni 4.472 walitumia uwanja huo mwaka 2019, huku ukiishinda viwanja vya ndege vya Entebbe, Kigali na Bujumbura.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyata ndiyo ulioongoza kwa kusafirisha abiria wengi kuliko viwanja vyote Afrika ya Mashariki.

Zaidi ya abiria milioni 9.147 walipitia katika uwanja huo, idadi ambayo ni karibu mara mbili ya abiria waliopitia viwanja vinne vya ndege vilivyopo ndani ya umoja huo.Mbali na Tanzania, uwanja wa ndege wa kimatifa wa Entebbe ulipata abiria milioni 2.008, Kigali abiria milioni 1.144 na Bujumbura abiria 257,806.

Ili kushindana na uwanja wa Jomo Kenyata, Dk Abel Kinyondoa alishauri uwanja wa ndege wa JNIA utengenezwe na kuwa ‘HUB’ badala ya kuwa tu uwanja wa ndege wa kimataifa ambao watu wanautumia kuja nchini pekee.

“Jomo Kenyata wanapata abiria wengi kwa sababu uwanja wao ni kama Hub yaani mtu akifika pale anaweza kupata ndege za moja kwa moja kwenda mataifa mbalimbali duniani,” alisema.

Mchumi na mtafiti mwandamizi, Profesa Samwel Wangwe alisema kupungua kwa safari za ndege kunapaswa kufanyiwa utafiti ili kujua sababu ili itatuliwe jambo litakalofanya safari hizo kuongezeka badala ya kupungua.