'Karume aenziwe kwa viongozi kujishusha kwa wananchi'

Viongozi wakuu wa kitaifa wa Serikali na wastaafu wakisikiliza mawaidha wakati wa dua ya Kumbukizi ya kifo cha Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume iliyofanyika leo Aprili 7,2024 Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui Unguja. Picha na Jesse Mikofu

Muktasari:

  • Ujumbe uliotawala katika dua ya kumkumbuka kiongozi huyo ni uadilifu, nidhamu na viongozi kujishusha kutatua kero za wananchi, mambo yanayoelezwa kufanywa na Sheikh Abeid Amani Karume eniz za uhai wake.

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ameongoza viongozi na wananchi katika dua ya kumuombea Rais wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume.

Dua ya kumuombea Karume aliyeuawa kwa kupigwa risasi mwaka 1972, imefanyika leo Aprili 7, 2024, Makao Makuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kisiwandui Zanzibar, ikiwa ni hitimisho la wiki ya kuwakumbuka viongozi walioshiriki Mapinduzi mwaka 1964.

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango akiweka shada la maua katika kaburi la aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume lililopo i nje ya ofisi Kuu za CCM , Kisiwandui Zanzibar,  wakati wa kusoma dua ya kumbukizi ya kifo chake iliyofanyika leo Aprili 7,2024 mjini Unguja. Picha na Jesse Mikofu

Wiki ya kuwakumbuka viongozi hao ilianza Aprili Mosi, 2024. Makaburi 17 ya viongozi hao yalitembelewa na marehemu kuombewa dua ikiwa ni njia mojawapo ya kuwakumbuka.

Wakizungumza baada ya dua, baadhi ya viongozi na wananchi wamesema hayati Karume alikuwa mtu wa kujishusha kwa wananchi, aliyetaka kuwaondolea umasikini Wazanzibari, hivyo viongozi wanaoshika madaraka hawana budi kufuata nyayo zake.

Kiongozi wa mabalozi wadogo Zanzibar, ambaye ni Balozi wa Heshima wa Brazil, Zanzibar, Abdulsamad Abdulrahm amesema  Karume alibadilisha taswira ya mwonekano wa Zanzibar kuanzia nyumba na miundombinu.

Amesema hayo yalikuwa maono ya Karume ya zaidi ya miaka 100 ambayo wanayaishi hadi sasa, lakini wazee wengi walikuwa hawajui kusoma ila walipatiwa elimu maalumu ambayo imewaweka viongozi waliopo madarakani leo.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi  akiweka shada la maua katika kaburi la aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume lililopo nje ya ofisi Kuu za CCM Kisiwandui,  wakati wa kusoma dua ya kumbukizi ya kifo chake leo Aprili 7,2024 mjini Unguja. Picha na Jesse Mikofu

Amesema ameacha watoto wa kuzaa na wengine wa kulea ambao wanaendeleza hekima na busara kutokana na miongozo yake.

Ameeleza Karume alikuwa  mtu wa kujishusha, mtu wa watu, alikuwa hana kiburi; “wito wangu kwa viongozi waliopo madarakani kutambua wajibu wa kuwatumikia wananchi bila kujali rangi, dini, kabila na bila kujiona kama wao ni wakubwa, kwani Karume alikuwa hana ubaguzi huo.”

Karume alikuwa akishuka kwa wananchi anatatua matatizo; “hiyo ndiyo tunataka kuona viongozi waende chini watatue matatizo.”

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff amesema kiongozi huyo alijenga imani kwa Wazanzibari.

“Ukiachana na maendeleo makubwa aliyoyafanya ya miundombinu, ujenzi wa nyumba, afya, na mambo ya maji bure katika nchi hii, lakini aliweka misingi mizuri ya imani, upendo, kuheshimiana na kujali, tutamkumbuka muda mrefu,” amesema.

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrick Ramadhan Soraga, amesema walikuwa wakimsoma kwenye vitabu na kuhadithiwa, wanaona alivyokuwa mfano bora wa waasisi wa nchi.

“Sisi vijana ambao tupo kwenye uongozi wa Serikali tuna mengi ya kujifunza kutokana na misingi aliyoiacha, ukiwemo uzalendo, uadilifu na mtu kujitoa kuipenda nchi yake. Haya ni mafunzo ambayo tunayachukua moyoni. Mungu atujalie tuwe viongozi bora kupitia nyayo zake,” amesema.

Meya wa Jiji la Zanzibar, Mohamoud Muhammed Mussa amesema kimsingi yapo mambo mengi ya kujifunza katika kifo cha Karume, likiwemo suala la ulinzi na usalama katika Taifa.

Katika maendeleo, ameomba pamoja na jitihada zinazochukuliwa za kuwaenzi na kuwakumbuka waliosababisha Mapinduzi ya mwaka 1964, kuna wajibu na haki kuwaangalia wajane wa marehemu ambao bado wapo hai.

Pia amesema maadili na nidhamu haviwezi kupatikana bila kuwapo upendo na mshikamano, hivyo ni fursa kwa viongozi kushikamana kuhakikisha wanasonga pamoja katika utekelezaji wa majukumu.

“Tunao wajibu wa kushikamana, kuwa wazalendo na kutambua kwamba Zanzibar ni yetu wa kuweza kuitengeneza na kuijenga ni sisi Wazanzibari wenyewe si mtu mwingine kutoka popote nje ya Zanzibar,” amesema.

Asha Abdalla Chande, mkazi wa Unguja amesema wananchi wanatamani kuona wakisaidiwa kama alivyofanya Mzee Karume.

Naye Lelat Juma Othman, amesema amejifunza mengi kupitia wiki ya kuwaenzi viongozi hao, hivyo utaratibu huo uendelezwe kwa kuwa unasaidia wafahamike hata kwa vijana kama yeye.

“Tunasikia alikuwa ana msimamo, hakuwa mbaguzi, anapenda haki kwa hiyo viongozi wetu waige hayo,” amesema.

Faida Salum Juma, kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja ametoa rai kwamba viongozi waliojitoa kupigania nchi waendelee kuombewa dua.

Viongozi mbalimbali wa dini, Serikali na wastaafu walihudhuria dua hiyo  wakiwamo Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson.

Wengine ni Makamu wa Kwanza na wa Pili wa Zanzibar, Othman Masoud na Hemed Abdulla, marais wastaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na Dk Mohammed Shein, aliyekuwa Makamu wa pili, Balozi Seif Ali Idi na Waziri Kiongozi mstaafu, Shamsi Vuai Nahodha.

Viongozi wa dini waliongozwa na Sheikh Mkuu, Abubakary Zubeir na Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kabi.

Baadhi ya viongozi wa siasa waliohudhuria ni Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Dk Muhammed Said Dimwa.