Kilimo cha pilipili ‘mwendokasi gumzo kwa wakulima, sokoni

Sunday December 26 2021
pilipili pic
By Hadija Jumanne

Tayari watu wengi hivi sasa hapa nchini, wameanza kuchangamkia fursa ya kujiajiri kupitia kilimo na uuzaji wa mazao mbalimbali. Je, wewe ungetamani kuwa miongoni mwa hao walioona fursa?

Pius Budodi ni mkulima wa kilimo cha pilipili aina ya mwendokasi, kutoka kata ya Lwanhima, wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza.

Anasema ameona fursa katika kilimo hicho, licha ya awali kujihusisha na kilimo cha mazao mengine kama nyanya, lakini zao la pilipili anasema ndilo linalomweka mjini muda wote.

Anasema, kupitia kilimo cha umwagiliaji kimemsaidia kuinua uchumi na kujiongozea kipato maradufu.

Mkulima hiyo anabainisha kuwa pilipili hizo huziuza kwa wachuuzi waliopo katika soko la Buhongwa lililopo Manispaa ya Nyamagana, mkoani Mwanza, kwa bei ya Sh 20,000 kwa ndoo ya lita 20 na Sh 10,000 kwa ndogo ya lita 10.

Pilipili hizo mithiri ya ndulele, huwa na rangi ya njano huku nyingine zikiwa na rangi ya kijani inayofanana na jani la mgomba ambayo huvutia machoni.

Advertisement

Kimuonekano unaweza kuzifananisha na pilipili mbuzi ambazo hata hivyo tangu kuja kwa ‘mwendokasi’ zimeonakana kwua si mali kitu.

Sifa mojwapo kuu ya ‘mwendokasi ni kunukia na ndiyo inayowasukuma wateja wengi wa pilipili kuzikimbilia.

Budodi mwenye watoto saba, anasema alianza kilimo tangu mwaka 1991, baada ya kubaini nusu ya eneo lake lenye ukubwa wa heka tano, lina chemchemu iliyopo karibu bonde la mto unaelekea Nyashishi.

Mazao ya biashara anayolima Budodi, mbali na pilipili za mwendokasi ni nyanya, kabichi, hoho, matango, nyanyachungu na miwa.

Wakati Budodi akibainisha hayo, mkulima mwingine Saadan Diamond, ameamua kujikita katika kilimo cha pilipili za mwendokasi, kwa maelezo kuwa zao hilo lina fursa kubwa.

Diamond anasema alianza kulima mwendokasi tangu 2017 mkoani Morogoro na baadaye kuhamia mkoani Iringa na Mbeya, anakoendelea na kilimo kingine cha nyanya na parachichi.

“Kwa mfano, Mkoa wa Iringa debe moja la pilipili mwendokasi lenye ujazo wa lita 20, tunauza Sh45,000 hadi Sh50,000 na hii ni bei ya shambani, ukienda sokoni bei yake inakuwa juu kidogo na hata ukisafirisha kutoka Iringa kupeleka Dar es Salaam , bei yake inakuwa juu zaidi” anafafanua Diamond.

Mkulima huyo ambaye ana shahada ya kilimo cha mboga mboga na matunda, anasema amelima pilipili za mwendokasi kwa sababu aliona soko lake ni kubwa na lipo wazi, ukilinganisha na mazao mengine.

“ Mwanzoni Pilipili hazikuwa na soko kutokana na watu kutojua fursa iliyopo lakini kwa sasa soko ni kubwa”

Bei yake sokoni

Wakati debe moja lenye ujazo wa lita 20 la pilipili hizo likiuzwa kati ya Sh 45,000 hadi 50,000 mkoani Iringa, kwa Jiji la Dar es Salaam, debe moja la ujazo huo huuzwa kati ya Sh 35,000 hadi 40,000 katika soko la Ilala Boma na Buguruni, huku nusu debe ikiuzwa Sh 15,000 hadi 20,000.

Kwa upande wa mkoa wa Mwanza, pilipili za mwendokasi zinauzwa kati ya Sh 20,000 hadi 25,000 kwa ujazo wa debe lenye uzito wa kilo 20 katika soko la Buhongwa.

Lakini gunia moja lenye ujazo wa debe tano linauzwa kati ya Sh 240,000 hadi 250,000 kwa baadhi ya mikoa nchini.

Rehema Sultan ni mfanyabiashara wa pilipili hizo katika soko la Ilala Boma, lililopo wilaya ya Ilala, anasema yeye ananunua pilipili hizo kwa bei ya Sh 35,000 na kuuza kwa Sh 38,000 hadi 40,000 kwa debe moja yenye ujazo wa lita 20.

“Dada yangu bei ya pilipili kwa sasa ipo juu sana, kwa mfano leo tunanunua ile ndoo ya lita 10, kati ya Sh 22,000 hadi Sh 25,000, huku gunia moja lenye ujazo wa debe tano hadi sita tunauziwa kati ya Sh 240,000 hadi Sh 250,000 na pilipili hizi zinatoka Pwani, Rufiji, Tanga, Moshi na Morogoro, ” anasema Rehema.

Rehema ambaye yupo katika biashara hiyo kwa muda wa miaka sita, anasema mbali na kuuza kwa jumla, pia ana wateja wake wa rejareja ambao huwauzia kwa sado moja na mafungu kwa Sh 500 hadi 1, 000.

Idd Maleta ni mwenyekiti wa wafanyabiashara na wadau wa Soko la Ilala Boma anasema pia soko la zao hilo lipo mkoa wa Morogoro, Dar es Salaam, Pwani, Arusha na Moshi pamoja na kwenye migahawa mikubwa, hoteli na maduka makubwa.

Fursa tele

Budodi anasema mahitaji ya pilipili za mwendokasi ni makubwa hapa nchini kuliko uzalishaji wenyewe, hivyo anawashauri vijana na wanawake wachangamkie fursa hiyo ya kilimo cha zao hilo kwani soko lake ni kubwa.

Kwa upande wake, Diamond anasema:” Pia nimeweza kununua shamba, gari na kujenga nyumba, hivyo hayo ni mafanikio makubwa kwangu lakini niko mbioni kuongeza eneo la kilimo kutoka ekari tatu hadi kufikia tano.’’

Changamoto za kilimo

Ukiondoa mabadiliko ya bei ambayo wakati mwingine zao hilo huwa na bei isiyoridhisha, kilimo hicho kwa mujibu wa Diamond kinakabiliwa na magonjwa hasa ya mnyauko na ukungu.

“Wadudu hushambulia majani na mmea kutokana na kwamba wanavutiwa na harufu hivyo ni hasara kwa mkulima, hasa tunaolima kilimo hai yaani Organic farming” anasema Diamond.

Anaongeza; “ Kuingia kwa ugonjwa wa Uviko- 19, kumesababisha wateja wasije kununua mazao yetu shambani na hata wale waliokuwa wanakuja sokoni pale Buhongwa nao wamepungua.’’

Budodi anasema mazao ya bustani huuzwa kutegemea na msimu ulivyo, lakini kabla ya kuingia kwa ugonjwa huo, alikuwa anauza ndoo kubwa ya nyanya yenye uzito wa kilo 20 kwa bei ya Sh 30,000.


Upandaji mwendokasi

Tangu kupanda hadi kuvuna zao hilo, huchukua muda wa miezi mitatu na kwamba pilipili zina uwezo wa kuendelea kustawi kwa muda wa miezi mitatu hadi mitano mfululizo kama itatunzwa vizuri.

Diamond anafafanua kuwa yeye hutumia mbegu aina ya Habanero kwa ajili ya kilimo hicho na katika kila ekari moja, mkulima ana uwezo wa kuvuna kuanzia tani tano na kuendelea.

Anafafanua kuwa kila baada ya siku saba, mkulima anatakiwa kuvuna pilipili hizo.

Advertisement