LSF, Stanbic Tanzania kutekeleza miradi ya maendeleo

Muktasari:

 Lengo ni kuweka mazingira mazuri ya elimu na kuboresha afya ya uzazi pamoja na kuwawezesha wanawake kupata fursa za kiuchumi, elimu ya kifedha na mitaji

Dar es Salaam. Taasisi isiyo ya kiserikali ya The Legal Services Facility (LSF), kwa kushirikiana na Benki ya Stanbic Tanzania, zimesaini makubaliano ya ushirikiano wa kutekeleza miradi ya maendeleo yenye lengo la kuwainua wanawake na wasichana kiuchumi, kielimu na kiafya.

Mkataba huo wa miaka miwili unalenga kuweka juhudi na rasilimali za pamoja kati ya taasisi hizi ili kukabiliana na changamoto za kijamii, hasa zinazowakabili wanawake na wasichana.

Makubaliano hayo yanalenga zaidi kuweka mazingira mazuri ya elimu na kuboresha afya ya uzazi pamoja na kuwawezesha wanawake kupata fursa za kiuchumi, elimu ya kifedha, pamoja na kuwaunganisha kwenye fursa za kupata mitaji kwa ajili ya kuwawezesha kiuchumi.

Akizungumza wakati wa utiaji saini mkataba huo, Mkurugenzi Mtendaji wa LSF, Lulu Ng’wanakilala amesema lengo la taasisi hizo ni kushirikiana kuhakikisha fursa sawa, kukuza usawa wa kijinsia, na uwezeshaji wa wanawake, hivyo kuwawezesha kutimiza ndoto zao.

Amesema ushirikiano huo utachangia moja kwa moja katika kufanikisha kipaumbele cha Taifa na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs); 5 (Usawa wa Jinsia), 3 (Afya Bora na Ustawi), 4 (Elimu ya Ubora), na 16 (Amani, Haki, na Taasisi Imara.

“Tunajivunia kusaini mkataba huu leo ​​ambao unatilia mkazo dhamira yetu ya kuwakutanisha wadau hususani mashirika binafsi ili kuunga mkono juhudi za pamoja katika kutatua changamoto za jamii kwa njia inayoleta tija na matokeo endelevu,” amesema.

 “Makubaliano haya tunayoingia leo yatarahisisha utekelezaji wa miradi ya pamoja na kukuza fikra shirikishi katika kuweka miradi na mipango mipya pamoja na kuendeleza yale ambayo yalishawekwa kabla.”

Mtendaji Mkuu wa Benki ya Stanbic Manzi Rwegasira amesema, “tuna furaha kubwa kushirikiana na LSF ili kufanikisha miradi itakayowezesha vijana na wanawake katika jamii nchini, pamoja na kukabiliana na athari za mazingira kwa kupanda miti ili kuchangia malengo ya nchi yetu ya Tanzania katika kulinda mazingira.”

Amesema ushirikiano huo unalenga kuimarisha fursa za kiuchumi kwa wanawake na vijana kupitia mipango inayozingatia ujuzi wa kifedha na maendeleo ya biashara. Ili kuwezesha kuimarisha ujuzi kwa walengwa, “tunalenga kutoa rasilimali zinazohitajika katika kuleta uhuru na mafanikio endelevu ya kifedha.”

 “Tuna furaha kufanya kazi pamoja na LSF hasa katika kuendeleza mipango hii, inayochangia moja kwa moja mipango ya maendeleo endelevu ya nchi yetu. Tunatazamia kuleta matokeo chanya na endelevu kwenye maisha ya wanawake, vijana, na jamii zote za Tanzania.”