Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maalim Seif awajulia hali majeruhi Zanzibar

Muktasari:

Mwenyekiti wa ACT- wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad amefanya ziara maalum ya kuwatembelea na kuwafariji wafuasi wa chama hicho waliokumbwa na kadhia za vurugu za uchaguzi mkuu, huku naibu wake Nassor Ahmed Mazrui akidaiwa kuhamishiwa Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa ACT- wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad amefanya ziara maalum ya kuwatembelea na kuwafariji wafuasi wa chama hicho waliokumbwa na kadhia za vurugu za uchaguzi mkuu, huku naibu wake Nassor Ahmed Mazrui akidaiwa kuhamishiwa Dar es Salaam.

Ziara hiyo ni ya kwanza kwa Maalim Seif baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa Zanzibar, ambao Dk Hussein Mwinyi aliibuka na ushindi wa kiti cha urais.

Katika ziara hiyo ya kutembelea maeneo mbalimbali mjini Unguja, Maalim Seif ambaye alikuwa mgombea urais wa Zanzibar aliambatana na katibu wa itikadi, uenezi na mawasiliano kwa umma, Salim Bimani.

Maalim Seif aliwaomba waathirika wa vurugu hizo kuwa wavumilivu na kutokana na majeraha hayo ambayo wameyapata, akidai kuwa yamesababishwa na utawala usiofuata sheria.

Alitumia nafasi hiyo kulitaka Jeshi la Polisi Zanzibar, kufuata misingi yao kazi wakati wa utekelezaji wa majukumu yake badala ya kuwaonea raia wasiokuwa na hatia.

Mkazi wa Makadara aliyekumbwa na kadhia hiyo , Duni Ali Haji alimweleza Maalim kuwa madhila hayo yaliwapata kwa sababu wanataka haki na utawala bora huku akimhakikishia kuwa hatawarudi nyuma.

“Nilipata kipigo wakati nikieleke kupiga kura. Kipigo ambacho kimesababisha mguu wangu kuvunjika na kufungwa bandeji ngumu,” alisema Haji

Wakati huo huo huo, Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema Mazrui pamoja na wenzake saba wanaoshikiliwa na polisi wamehamishwa jijini Dar es Salaam baada ya kusafirishwa wakitokea kisiwani Unguja.

Mazrui ambaye alikuwa mgombea ubunge wa Mwera na wenzake hao walikamatwa Oktoba 28 mjini Unguja wakidaiwa kukutwa na vifaa vya kuingilia mfumo wa matokeo ya uchaguzi akiwa na wenzake.

Kauli hiyo ya Zitto ambaye alikuwa mgombea ubunge wa Kigoma Mjini, imekuja siku chache baada ya kamati kuu ya chama hicho iliyokutana Novemba 4 kuazimia kufuatilia kwa kina hatma ya Mazrui na wenzake ambao ni wanachama wa ACT.

Juzi, Zitto aliliambia gazeti hili akisema: “Nilikwenda makao makuu ya polisi lakini sikufanikiwa kuonana na DCI (mkurugenzi wa makosa ya jinai-Robert Boaz) bali nilimkuta naibu wake, Kenyela aliyenithibitishia kuwa Mazrui na wenzake wapo Dar es Salaam wakitokea Zanzibar.

“Hata hivyo Kenyela hakuniambia anashikiliwa kituo gani au kwa makosa gani kwa sababu yeye siyo msemaji. Kwa hiyo tunaendelea na jitihada za kumtafuta Boaz kuhusu suala hili.’’

Gazeti lilitamfuta kwa simu Boaz kuzungumza suala hilo, ambaye alisema polisi ina utaratibu maalumu wa utoaji wa habari huku akisema: “Kama upo Dar es Salaam nenda pale makao makuu ya polisi, kwa sababu kuna utaratibu maalumu wa kutoa habari.’’

Baada ya majibu hayo ya Boaz, gazeti lilimtafuta kwa simu msemaji wa polisi, David Misime ambaye hakupokea simu lakini baada ya muda alituma ujumbe akiomba aandikiwe ujumbe mfupi kwa kuwa yupo kwenye kikao.Hata hivyo, baada ya kutumiwa ujumbe msemaji huyo hakuujibu.

Juzi mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad alisema taarifa za Mazrui na wenzake kusafirishwa jijini Dar es Salaam, walizipata Novemba 4 lakini hawajui sababu za kupelekwa huko.