Madiwani waja juu mbunge kutoshiriki vikao, ajitetea

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Selemani Nampanye akiongea katika baraza maalum la bajeti. Picha na Florence Sanawa

Muktasari:

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara limehoji kitendo cha mbunge huyo kutoonekana katika vikao kwa zaidi ya mara 17.

Mtwara. Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara limehoji kitendo cha Mbunge wa Mtwara Vijijini, Shamsia Tamba (CUF) kutoonekana katika vikao.

Inaelezwa Tamba hajahudhuria zaidi ya vikao 17 vya baraza na vikao 30 vya kamati ya fedha.

Hata hivyo, Mwananchi Digital limezungumza na Mbunge Tamba kwa simu kuhusiana na malalamiko hayo.

Amekanusha kuwa si kweli,  huku akidai kuwa anapokuwa jimboni kwake Mtwara huwa anahudhuria vikao hivyo.

“Kwanza ananilalamikia kwa lipi? Sisi wabunge ni mara chache kuhudhuria vikao vya baraza la madiwani, mara nyingi huwa tunakuwa Dodoma, yaani ratiba ya vikao vya Bunge inafanana na ratiba ya vikao vya baraza la madiwani na huwa tunaomba ratiba ibadilishwe na sisi tuweze kuhudhuria lakini bado,” amesema Tamba.

Akizungumzia kutohudhuria vikao vya kamati ya fedha, mbunge huyo amesema mara nyingi ratiba ya vikao hivyo mara nyingi huwa inaendana na ile ya kamati ya fedha ya bunge na yeye ni mjumbe kule, hivyo mara nyingi vikao hivyo hufanyikia Dodoma analazimika kuwa huko.

“Lakini mbona mimi ni mchangiaji mzuri wa hoja za wananchi wangu bungeni, hata changamoto ninazopitia kupitia kwa wananchi, mara nyingi huwa namtuma katibu (Katibu wa mbunge) kuzishughulikia na kisha ananipa mrejesho na mambo yanaenda” amesema Tamba.

Akizungumza katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani la kujadili na kupitisha bajeti ya mwaka wa fedha 2024/25 jana jioni, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Selemani Nampanye alisema hakuna vikao muhimu kama vya kupitisha bajeti ambavyo mbunge pia anapaswa kuhudhuria, lakini Mtamba hashiriki.

“Sisi tunaamini mbunge ndio sauti kubwa zaidi kwetu, halafu mimi huwa nazunguka sana kwenye halmashauri za wenzetu, kuna vitu navikuta halafu unajikuta mpweke, yaani unakuta miradi mipya inaendelea lakini kwako haipo kwenye mgao.”

“Ile miradi inapatikana baada ya mbunge kukaa na madiwani na kusikiliza changamoto zilizopo lakini tangu tuangie madarakani,  hiki ni kikao cha 17 hajafika. Nakumbuka nilimuona kikao kimoja na hakumaliza na kwenye vikao vya kamati ya fedha zaidi ya vikao 30 nilimuona kikao kimoja tu nacho hakumaliza,” amesema Nampanye.

“Kwa staili hii anapaswa kubeba yatokanayo na vikao hivi na kuyapeleka bungeni, sasa tunapata hasara kwenye bajeti alipaswa kuwepo kwa kuwa yeye ndio mwenye jukumu la kuyabeba haya na kuyapeleka  huko juu,” amesema mwenyekiti huyo.

Ameongeza: “Mfano hili jambo la wawekezaji wetu kusaidia jamii, kama mnakuwa na mbunge anayeguswa na haya mambo ni rahisi kuwa yeye siku zote anakutana na mawaziri Kila siku anaweza kusemea hizi changamoto ni rahiisi kupata jibu la uhakika kutoka kwake yaani yeye anaweza kuwa na msaada mkubwa kwetu zaidi ya mwaka wa tatu hatujapata CSR nani atatusemea sisi?” amesema Nampanye.

Amesema haiwezekani mtu kuwa na dharura kila siku wakati ni mjumbe anayepaswa kubeba jukumu la kusimamia hayo mambo na kuyachukua na kupeleka bungeni.

Akizungumzia hilo, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Mtwara Vijijni, Hassan Mpoja amesema amepokea malalamiko hayo na ofisi yao inayafanyia kazi.

“Unajua jambo lililozungumzwa sio kificho, ni jambo ambalo lipo bayana, yaani liko wazi sio siri kweli hilo tatizo lipo siwezi kulikanusha nimepokea maelekezo ya mwenyekiti wa halmashauri nitayafanyia kazi,” amesema Mpoja.