Majaliwa: Serikali itaendeleza, kuenzi juhudi za Magufuli

Muktasari:

  • Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa amebainisha mambo muhimu ambayo Serikali itatekeleza kwa umuhimu wake ikiwa ni pamoja na kuenzi na kuendeleza jitihada, maono na juhudi za Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa amebainisha mambo muhimu ambayo Serikali itatekeleza kwa umuhimu wake ikiwa ni pamoja na kuenzi na kuendeleza jitihada, maono na juhudi za Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli.

Majaliwa ameyasema hayo leo Jumanne Aprili 13, 2021 bungeni Dodoma wakati akiwasilisha bajeti ya ofisi ya waziri mkuu pamoja na taasisi zilizo chini yake kwa mwaka wa fedha 2021/22.

Amebainisha mambo ambayo watayaenzi kutoka kwa Hayati Magufuli kuwa ni pamoja na ulinzi wa rasilimali za Taifa, kupambana na rushwa, kuendeleza miradi ya kimkakati, kuenzi lugha ya Kiswahili, nidhamu katika matumizi ya fedha za umma, kuwaunganisha na kuwajali wananchi wanyonge pamoja na kudumisha umoja wa kitaifa.

“Serikali itatekeleza kwa kasi miradi ya kimkakati ambayo inalenga kukuza uchumi, kuimarisha huduma za jamii na kuongeza fursa za ajira kwa kasi tuliyoanza nayo. Serikali itaendelea kuongeza nguvu zake kuendeleza na hatimaye kuikamilisha miradi hiyo,” amesema Majaliwa.

Amesema itaimarisha huduma za jamii za afya, maji, elimu pamoja na utekelezaji wa miradi inayoendelea na uanzishwaji wa miradi mipya.

Jambo jingine amesema ni kuimarisha makusanyo ya mapato kwa kutumia mifumo ya kielektroniki na mashine, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za umma.

“Katika hili la matumizi ya kielektroniki, hatua kazi zitachukuliwa dhidi ya taasisi ambayo tumeiagiza kutumia mifumo ya kielektroniki na bado haitumii mifumo hiyo,” amesema Majaliwa katika hotuba yake.

Pia, amesema Serikali itashirikiana na washirika wa maendeleo katika kutekeleza miradi na programu mbalimbali zinazolenga kuimarisha shughuli za kiuchumi na kijamii. Amesema itachukua hatua za kukabiliana na majanga ikiwemo magonjwa ya mlipuko.

“Natoa rai kwa Watanzania wote bila kujali itikadi za kisiasa, dini au kabila, waendelee kufanya kazi kwa bidii, kwa weledi kwa uadilifu kwa tija na ufanisi, uaminifu na kupiga vita rushwa ili tuweze kulinda mafanikio tuliyoyapata,” amesisitiza Majaliwa.