Majongoo bahari sasa dili

Tanga. Vijana wa Jiji la Tanga wametakiwa kuchangamkia fursa ya ufugaji wa matango bahari (majongoo bahari) ambayo soko lake ni kubwa ndani na nje ya nchi ili waweze kupiga hatua kiuchumi.
Ushauri huo umetolewa na Omari Mohamed, ofisa mfawidhi idara ya ukuzaji viumbemaji katika Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, wakati akizungumza na gazeti hili jana kuhusu fursa zilizopo katika Hahari ya Hindi jijini Tanga zinazoweza kuwaletea utajiri wa haraka vijana.
Alisema ameshatoa mafunzo yaliyoandaliwa na Botner Foundation kwa kushirikiana na asasi ya Tanga Yetu kuhusu ufugaji wa kitaalamu wa matango bahari ambayo yanahitajika kwa kiasi kikubwa.
“Ufugaji wa matango bahari ni rahisi na unavuna kwa muda mfupi, kwa sasa kilo moja inauzwa kati ya Sh80,000 hadi Sh120,000. Ina maana ukiwa na kilo 100 unajipatia Sh8 milioni au Sh12 milioni,” alisema Omar.
Mtaalamu huyo alisema fursa nyingine ni kilimo cha mwani mnene a mwembamba ambao unastawi ukanda wote wa Bahari ya Hindi kuanzia Wilaya ya Mkinga (Tanga) hadi Msimbati- Mtwara, ambao pia soko lake ni la uhakika.
“Pia vikundi vya vijana vikijikita katika uvuvi wa kamba miti na kamba kochi, pweza, ngisi, kaa na samaki mapezi unaweza kuwanufaisha haraka kwa sababu soko lake lipo mitaani na nchi za nje,” alisema Omar.
Hawa Msuya kutoka Botner Foundation aliwataka vijana wa Jiji la Tanga kuacha kukimbia vituo vya mabasi kupiga debe badala yake wajikite katika uzalishaji mali, ufundi, uvuvi na ufungaji wa viumbe maji ili wajikwamue kiuchumi.
“Fursa za Tanga kama zingekuwa mikoa mingine usingemkuta kijana akihangaika na kupiga debe, wengi wangekimbilia baharini kufuga matango bahari wajipatie dola,” alisema.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Sipora Liana alisema katika kuhakikisha vijana wanajikwamua kichumi, zimetengwa ekari 200 kwa ajili ya kilimo cha kisasa kwa vijana na mitaji itapatikana kupitia mikopo inayotolewa na halmashauri hiyo.
“Kuhusu uvuvi tunashirikiana na Botna pamoja na asasi ya Tanga Yetu katika kuwajengea uwezo vijana kuendesha uvuvi wa samaki, viumbebahari na kilimo cha mwani kwa sababu ndiyo ukombozi kwa vijana,”alisema Liana.